1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro kati ya Uturuki na Iraq wazidi huku Iraq ikitaka mazungumzo

16 Oktoba 2007

Serikali ya Iraq imeitisha mazungumzo ya dharura na Uturuki baada ya nchi hiyo kutishia kulivamia eneo la kaskazini mwa Iraq kuwaangamiza waasi wakikurdi.

Tayari makamu wa rais wa Iraq amekwenda Uturuki kukutana na viongozi wan chi hiyo.

Iraq imeanzisha mikakati ya kidiplomasia yenye lengo la kuumalima mzozo uliojitokeza kufuatia vitisho vya Uturuki vya kutuma wanajeshi wake kaskazini mwa Iraq kuwaangamiza waasi wakikurdi.Waziri mkuu wa Iraq Nuri al Maliki ametangaza kwamba atatuma ujumbe wa ngazi ya juu nchini Uturuki kwa ajili ya mazungumzo ya dharura.Matamshi hayo ya bwana Maliki yamefuatia kikao cha dharura cha baraza la mawaziri kilichojadili juu ya mgogoro huu.Wakati waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan akitoa changamoto kwa serikali ya Iraq na wakurdi nchini humo ya kutaka wachukua msimamo dhidi ya waasi wa kikurdi wa kaskazini mwa Iraq au wakabiliane na matokeo yake Iraq kwa upande wake imeamua kutoa taarifa kadhaa za kutaka maridhiano.Imeitaka Uturuki ichukue njia za kidiplomasia badala ya kutumia nguvu katika kulitatua suala hilo.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa waziri mkuu Nuri al Maliki,Ali al Dabbagh pia imeitaka Uturuki kuitisha kikao cha dharura kuutatua mzozo huu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo waziri mkuu al Maliki amesema hatakubali matumizi ya nguvu kama njia ya kuyatatua masuala kati ya nchi hizo mbili licha ya kuwa wanatambua na kuelewa fika wasiwasi wa Uturuki.

Hii leo waziri mkuu wa Uturuki Tayyip Erdogan amesema bunge la nchi yake litakapoidhinisha hatua ya kuanzisha mashambulio dhidi ya waasi wa kikurdi kaskazini mwa Iraq haitamanisha hatua hiyo itafanyika mara moja bali watachukua hatua katika wakati unaofaa na kwa mujibu wa sheria sahihi.

Aidha amekiambia chama chake cha AK kwamba suala muhimu ni Ulinzi wa nchi yake na sio vinginevyo.

Baraza la mawaziri la Uturuki lilitaka bunge wiki hii kutoa idhini ya kuanzisha opresheni za kijeshi kaskazini mwa Iraq na uamuzi wa bunge unatarajiwa kutolewa kesho jumatano.

Matamshi hayo ya Uturuki yamezusha hali ya wasiwasi nchini Iraq jambo ambalo limeifanya serikali ya nchi hiyo leo kumtuma makamu wake wa rais Tareq al Hashemi mjini Ankara kufanya mazungumzo na utawala huo.

Itakukumbukwa kwamba mwezi uliopita Iraq na Uturuki zilikubaliana kupambana na waasi hao lakini walishindwa kukubaliana juu ya kipengele kinachoruhusu wanajeshi wa Uturuki kujihusisha na opresheni dhidi ya waasi hao kama ilivyokuwa inafanyika miaka ya tisini. Aidha Uturuki inazilaumu Marekani na Iraq kwa kushindwa kuchukua hatua za kutosha kupambana na waasi wakikurdi wapatao elfu 3000 wanaofanya mashambulio mashariki mwa Uturuki wakipigania kujitenga.

Marekani ikizungumzia juu ya mzozo huu mpya imeiomba Uturuki ijizuie kuchukua hatua ya kijeshi dhidi ya waasi hao wakikurdi.

Marekani inahofia ikiwa Uturuki italivamia eneo la kaskazini mwa Iraq kutakuwepo na mzozo mkubwa kwenye eneo hilo ambalo angalau limeepuka ghasia zinazotokea katika maeneo mengine ya Iraq.

Wanazuoni wakiislamu nchini Iraq pia wameitaka Uturuki kuwa na stahamala katika suala hilo wakisema wanasiasa wa Uturuki watafute njia mbadala ya kuutatua mzozo huu na sio vita.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW