Mgogoro wa bajeti washtadi Marekani
29 Desemba 2012Baada ya kukutana na viongozi wa wabunge Obama amesema Democrats na Republican watapitisha juhudi kubwa mwishoni mwa wiki hii ili kuepusha mchakato wa kupanda kwa kodi na kukatwa kwa mfuko wa matumizi ya kijamii. Ikiwa suluhisho halitapatikana hadi mwishoni mwa mwezi huu,mchakato huo utaanza tarehe Mosi Januari.
Rais Obama ameeleza matumaini ya tahadhari kwamba makubaliano yanaweza kufikiwa.Amesema wajumbe wa chama cha Republican wamekuwa wanavutana kwa miezi kadhaa juu ya nini la kufanya kuhusu hatua ya kupunguza kodi kwa Wamarekani wote iliyochukuliwa kwanza na Rais wa hapo awali George Bush. Lakini mwisho wa kutekelezwa kwa hatua hiyo ni hapo tarehe 31.Desemba.
Mpango wa Obama ni kupandisha kodi kwa matajiri na kuwaepusha Wamarekani wa tabaka la kati. Kwa upande wao Republican wanataka vipenyo vyote vya kodi vizibwe ili kuweza kuingiza mapato na matumizi yakatwe kwa kiwango kikubwa. Ikiwa mapatano hayatafikiwa hadi Jumanne ijayo,kodi zitapanda kwa Wamarekani wote.
Wakati huo huo vyombo vya habari vimeripoti kwamba kiongozi wa Seneti inayodhibitiwa na wajumbe wa chama cha Democratic Harry Reid anatayarisha mswada juu ya kuepusha kupandishwa kodi kwa Wamarekani wa tabaka la kati.
Mswada huo unatarajiwa kupigiwa kura jumatatu ijayo, wakati mazungumzo yanaendelea baina yake na Seneta,Mitch McConnell wa chama cha Republican.
Mswada huo ni juu ya kuepusha kupandishwa kodi kwa watu wanaopata chini ya dola laki mbili na nusu kwa mwaka. Hatahivyo makubaliano yoyote baina ya wajumbe wa Democratic na Republican yatapaswa yaidhinishwe na Baraza la wawakilishi.Lakini bado haijawa wazi iwapo makubaliano yatafikiwa katika dakika za mwisho ili kuepusha kukata matumizi, au iwapo Reid na McConnell wataafikiana juu ya ombi mahsusi la Rais Obama juu ya kuongeza kiwango cha kukopa hadi kufikia dola Trillioni 16.
Seneta wa chama cha Republican Bob Cocker amelalamika kwamba Rais Obama na wajumbe wa chama cha Democratic wamekuwa wanalizuia pendekezo juu ya kukata matumizi yanayoilemea bajeti na kuizidisha nakisi.Seneta huyo amesema mwishowe "tutaishia katika mpango utakaosababisha kizungumkuti kingine cha bajeti" Wataalamu wa masuala ya uchumi wametahadharisha kwamba bila ya suluhisho kufikiwa Marekani inaweza kuingia katika mdororo wa uchumi na hivyo kusababisha kuongezeka kwa ukosefu wa ajira.
Mwandishi:Mtullya Abdu/DPEA/RTRE/
Mhariri: Sekione Kitojo