1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa Ethiopia watishia uthabiti wa kikanda-UN

19 Septemba 2023

Makubaliano ya amani ya Tigray yashindwa kumaliza ukiukaji wa haki za binadamu na mauaji

Wakaazi walioachwa bila makaazi kijiji cha Kibet wakabiliwa na matatizo mengi ya kijamii
Watu walioachwa bila makaazi katika kijiji cha Kibet,EthiopiaPicha: Shewangizaw Wegayehu/DW

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamesema kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaoendelea kufanyika nchini Ethiopia licha ya kufikiwa makubaliano ya amani kuhusu mgogoro wa Kaskazini mwa nchi hiyo. Wataalamu hao wanaonya kwamba mgogoro unasambaa kote nchini humo na unautumbukiza uthabiti wa eneo zima katika hatari.

Taarifa ya wachunguzi wa Umoja wa Mataifa imesema mauaji, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu bado yanafanyika ndani ya Ethiopia na makubaliano ya amani yaliyosainiwa kumaliza vita katika jimbo la Tigray,hayajaleta amani ya kweli.

Mohamed Chande Othman mkuu wa tume ya Umoja wa Mataifa  ya wataalamu wa haki za  binadamu kuhusu Ethiopia,anasema pamoja na kwamba makubaliano hayo huenda kwa kiasi kikubwa yamenyamazisha milio ya risasi bado kwa bahati mbaya yameshindwa kutatua mgogoro wa jimbo hilo la Kaskazini la Tigray.

''Ni vigumu kutia chumvi ukubwa wa machafuko yaliyotokea Ethiopia tangu Novemba 2020.Tumeorodhesha matukio ya mauaji,ubakaji,njaa,uharibifu wa shule na hata majengo ya hospitali na watu kuondolewa kwa nguvu kwenye makaazi yao na matukio ya watu wengu kutiwa jela,ambayo yanafikia kuwa ni uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.''

Hali inatisha mtaalamu huyo amesema,na zaidi ya Tigray ripoti ya tume anayoiongoza imeonya kwamba vita na uhasama nchini humo sasa vimefikia katika ngazi ya kitaifa huku ukiukaji mkubwa ukiongezeka na hasa katika jimbo la Amhara lakini pia kwenye jimbo la Oromia na kwengineko.

Mji mkuu wa Tigray MekellePicha: Millionen Hailesilassie/DW

Imeweka wazi kwamba kitisho  kinachoikabili nchi hiyo pamoja na uthabiti wa eneo zima na hali ya haki za binadamu katika Afrika Mashariki,kiko wazi na  hakiwezi kutiwa chumvi.

Afisa mwingine kwenye tume hiyo ya Umoja wa Mataifa Radhika Coomaraswamy amewaambia wanadishi habari kwamba kuna viashiria vya uwezekano wa kutokea baadae uhalifu wa mauaji huku mivutano ikionekana kujitokeza kati ya makundi ya makabila mawili.

Tume hiyo kimsingi inajiandaa kuwasilisha ripoti yake mbele ya baraza la haki za binadamu la Umoja huo wa Mataifa baadae wiki hii na imeshasema kwamba kinachohitajika katika kufanikisha amani ya kweli na ya kudumu kwenye mgogoro huu ni kushirikishwa  kwenye mazungumzo kwa Waethiopia wote.

Historia ya migogoro Ethiopia

Tukumbushe kwamba Ethiopia ni nchi kubwa yenye makabila tofauti zaidi ya 80 na kwa muda mrefu nchi hiyo imekuwa ikijikuta ikihangaika na migogoro ya kimaeneo ndani ya mipaka yake.

Wanajeshi wa jeshi la Ethiopia wakiwakumbuka wenzao waliouwawa na TPLF mwanzoni mwa vita vya Tigray mwaka 2020Picha: AP/picture alliance

Mgogoro huu wa Tigray uliozuka Novemba mwaka 2020 ulihusisha wanajeshi wa serikali ya mjini Adis Ababa wakiungwa mkono na jeshi la nchi jirani ya Eritrea pamoja na vikosi vya wanamgambo kutoka mkoa jirani  wa Amhara dhidi ya jeshi la chama cha ukombozi wa watu wa Tigray TPLF.Vita hivyo vilisababisha mauaji ya watu wengi kutoka pande zote,lakini yalikuwepo matumaini kwamba mauaji hayo yatasitishwa baada ya kusainiwa makubaliano ya amani mwaka jana.

Kwa bahati mbaya kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa lakini bado hali sio nzuri.Wanajeshi wa Eritrea na wanamgambo kutoka jimbo la Amhara wamekuwa wakiendelea kufanya matukio ya ukiukaji mkubwa katika jimbo la Tigray ikiwemo,kuwabaka na kuwanyanyasa kingono wanawake na wasichana.

''Hali ilikuwa ikizidi kuwa mbaya kadri inavyoendelea,ikijumuisha ubakaji,pamoja na ukatili mkubwa sana.Lakini lazima nikiri kwamba hali matukio mabaya zaidi ni yale yaliyofanywa na wanajeshi wa Eritrea katika jimbo la Tigray japo bila shaka pia wanajeshi wa Ethiopia wanahusika.''

Mjumbe huyo wa tume ya wataalamu wa Umoja huo,Coomaraswamy anasema vurugu za unyanyasaji wa kingono zinatisha.Lakini pia imeelezwa kwenye ripoti ya waatalamu hao kwamba kuna mtindo ulioongezeka wa kutangazwa hali ya dharura nchini humo ikiambatana na hatua za ukiukaji mkubwa na tayari tume hiyo imeshapata ripoti za ukiukaji unaofanywa dhidi ya raia wa Amhara tangu kulipotangazwa  amri ya hali ya dharura mwezi uliopita.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW