1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa kibinadamu utazidi kuongezeka mwaka 2024?

27 Desemba 2023

Kamati ya kimataifa ya harakati za uokozi, IRC imesema katika ripoti yake kwamba migogoro inayowakabili binadamu itaongezeka mnamo mwaka wa 2024 kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, vita, na kupungua misaada.

Niger | Arbeit des International Rescue Committee (IRC)
Picha: IRC

Katika ripoti yake kamati hiyo yenye makao yake mjini New York nchini Marekani, imeeleza kuwa mataifa 20 barani Afrika yatakuwamo katika hatari kubwa ya kukumbwa na hali mbaya katika mwaka ujao wa 2024.

Kamati ya IRC imechapisha ripoti yake baada ya kuongezeka watu milioni 300 wanaohitaji misaada ya kibinadamu na kuongezeka kwa watu wengine milioni 110 waliolazimika kukimbia makwao.

Mkuu wa kamati hiyo David Miliband aliyekuwa zamani waziri wa mambo ya nje wa Uingereza, amesema dunia imo katika wakati mbaya na ametoa wito wa kuweka mkazo zaidi juu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa, kuwawezesha wanawake, kutoa huduma za benki kwa wote, kuwasadia watu waliopoteza makaazi yao na kuchukua hatua ili kukomesha tabia ya kuvunja sheria bila ya kuwajibishwa.

Soma pia:Kulingana na Umoja wa Mataifa, karibu watu milioni 2 hawatapata misaada kutokana na ukosefu wa ufadhili.

Katika orodha yake ya nchi zinazokabiliwa na hali mbaya kamati hiyo imesema Sudan na Sudan Kusini  zinaongoza. Nchi nyingine 9 za kusini mwa jangwa la Sahara zinafuatia. Nyingine ni Syria, Lebanon, Yemen, Ukraine, Ecuador na Haiti.

Nchi hizo kwa pamoja zinawakilisha asilimia 10 ya binadamu wote duniani, lakini zinahitaji asilimia 86 ya misaada ya kimataifa na pia zinawakilisha asilimia 70 ya watu wote wanaolazimika kukimbia makaazi yao.

Idadi kubwa ya watu hao ni masikini na ndiyo waliyomo hatarini kukumbwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Mabadiliko ya tabianchi yanachangia pakubwa

Juu ya Sudan kamati ya kimataifa ya uokozi imesema nchi hiyo iliyomo vitani inastahili kutiliwa maanani na jumuiya ya kimataifa. Wakati baadhi ya nchi za Afrika zinaboresha kwa haraka hali nzuri za maisha, migogoro, mapinduzi ya kijeshi na umasikini pia unaongezeka imeeleza kamati hiyo.

Mkulima akiwamwagilizia bustani ya mbogamboga huko Sudan KusiniPicha: Stefanie Glinski/Welthungerhilfe

Kamati ya kimataifa ya harakati za uokozi, IRC imesema hali ya hewa ya El Nino inatishia kuleta hali mbaya sana za hewa. Ecuador ambako kumekuwa nyumbani kwa wakimbizi wengi kutoka Venezuela iliingizwa katika orodha kwa mara ya kwanza baada ya kuongezeka kwa uhalifu wa kutumia nguvu, ambako serikali ya nchi hiyo inasema unatokana na biashara ya mihadarati.

Serikali ya Ecuador imeeleza kuwa hali hiyo inazidisha dhiki za kiuchumi kwa kiasi kikubwa.

Wakati huo huo nchini Haiti, kamati ya IRC inasema karibu nusu ya idadi ya watu wanahitaji misaada ya kibinadamu na kwamba hailekei iwapo juhudi za Umoja wa Mataifa za kusaidia polisi kupambana na magenge yenye silaha zitaifanya hali kuwa bora katika nchi hiyo ifikapo mwaka ujao.

Soma pia:UN yatoa fedha za msaada wa dharura Ethiopia

Wakati huo huo mashirika ya misaada yanatahadharisha juu ya kuzorota kwa hali ya kibinadamu nchini Afghanistan. Shirika la chakula la Umoja wa Mataifa WFP limesema wakati ambapo msimu wa baridi kali unakaribia nchini Afghanistan familia zitalazimika kuchagua kati ya kutia joto ndani ya nyumba au kuwalisha watoto.

Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Kimataifa la uokoaji Corina Pfitzner amesema hali nchini Afghanistan tayari ni ya maafa. Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa watu zaidi ya milioni 29 kati ya milioni 40 wa nchi hiyo kwa sasa wanategemea misaada.

Baada ya miongo kadhaa ya vita, Afghanistan bado haina miundombinu ya msingi kwenye sehemu nyingi za nchi hiyo.

Mataifa ya Afrika na vita dhidi ya taka za plastiki

01:36

This browser does not support the video element.