1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hezbollah yapinga pendekezo la Hariri.

Abdu Said Mtullya8 Septemba 2009

Hezbollah yapinga pendekezo la Hariri juu ya baraza la mawaziri.

Waziri Mkuu mteule wa Lebanon Saad Hariri na kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah.Picha: AP


Mgogoro wa kisiasa bado unaendelea nchini Lebanon baada ya Kiongozi wa Hezbollah, Hassan Nasrallah, kulikataa pendekezo la waziri mkuu mteule, Saad Hariri, juu ya baraza la mawaziri.Nasrallah amesema baraza hilo litatanisha hali zaidi.

Waziri mkuu mteule, bwana Hariri, amependekeza baraza la mawaziri 30.

Amewasilisha pendekezo la kuunda serikali kwa rais Michel Suleiman, yaani miezi zaidi ya mitatu baada ya muungano wake kushinda katika uchaguzi mkuu. Lakini muungano unaongozwa na Hezbollah umelipinga pendekezo hilo.

Kiongozi wa Hezbollah, bwana Nasrallah, amesema haamini kuwa pendekezo la waziri mkuu mteule bwana Hariri litaiwezesha Lebanon iondokane na mgogoro juu ya kuunda serikali mpya.

Akihutubia kwa njia ya televisheni, kiongozi huyo wa Hezbollah alisema kuwa Hezbollah itasimama kidete katika mshikamano thabiti dhidi ya hatua hiyo hafifu iliyopendekezwa na bwana Hariri.

Bwana Hariri aliteuliwa mwishoni mwa mwezi Juni kuwa waziri mkuu wa Lebanon, lakini bado hajaweza kukifia makubalino na upande wa upinzani juu ya kuunda serikali ya Umoja nchini Lebanon itakayoijumuisha Hezbollah inayoungwa mkono na Syria na Iran.

Rais wa Lebanon, Michel Suleiman, sasa anakabiliwa na mtanziko kwa sababu hatalipitisha baraza la mawaziri ambalo haliungwi mkono na upinzani.

Hata hivyo, rais huyo amemwambia waziri mkuu mteule Hariri kwamba atalizingatia pendekezo lililowasilishwa kwake.

Wakati huo huo, mjumbe mwandamizi wa upinzani amesema wao hawana habari juu ya pendekezo la bwana Hariri.

Bwana Hariri amependekeza kuundwa baraza la mawaziri 30. Kati ya hao 15 wanapaswa kutoka kwenye mfungamano wake, 10 kutoka upande wa upinzani na watano watakaoteuliwa na rais.

Kiini cha mgogoro ni matakwa ya chama cha Michel Aoun, Free Patriotic Movement ,chenye viti vingi bungeni kuliko chama kingine chochote cha kikristo nchini Lebanon.

Bwana Michel Aoun anataka mkwewe, Gebran Bassil, aendelee kuwa waziri wa mawasiliano. Bwana Auon pia anataka amteue waziri wa mambo ya ndani. Lakini waziri mkuu mteule, bwana Hariri anapinga matakwa hayo.

Kutokana na mvutano huo, waziri mkuu wa hapo awali, Fouad Siniora, ambae pia ni mwanachama wa chama cha Hariri, ataliongoza baraza la mawaziri katika kipindi cha mpito hadi hapo rais Michel Suleiman atakapotoa agizo la kuundwa serikali mpya.

Mwandishi/Mtullya Abdu AFPE

Mhariri/Othman, Miraji