1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa Sudan watu zaidi wauawa

12 Machi 2026

Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika jimbo la White Nile nchini Sudan yaliyolenga shule ya upili na kituo cha afya kwenye eneo la kusini mwa Sudan yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 17.

Sudan Tawila 2025 | Wakimbizi wa ndani nchini Sudan
Wakimbizi wa ndani nchini SudanPicha: STR/AFP/Getty Images

Daktari Musa al-Majeri, ambaye ni mkurugenzi wa Hospitali ya Douiem, kituo kikuu cha matibabu kilicho karibu zaidi na kijiji cha Shukeiri katika jimbo la White Nile,amesema watu wengine 10 walijeruhiwa katika mashambulio hayo. 

Kundi la madaktari limevilaumu vikosi vya RSF kwa mashambulio hayo ingawa RSF wenyewe hawakukubali kutoa maoni kuhusu swala hilo.

Mapigano makali yanaendelea kwa karibu miaka mitatu sasa katika eneo hilo.  Sudan imekumbwa na migogoro tangu mwezi Aprili mwaka 2023, kutokana na mzozo wa kugombea madaraka kati ya jeshi la taifa na vikosi vya RSF.

Sragiar Haroon mkimbizi wa ndani mbele ya ya kibanda chake katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Tiamushro huko Kadugli, jimbo la Kordofan KusiniPicha: Guy Peterson/AFP/Getty Images

Jimbo la Kordofan, lenye akiba ya mafuta na ardhi ya kilimo linayagawa maeneo kati ya washirika wa kijeshi na ngome za vikosi vya RSF katika eneo la Darfur na eneo la mashariki mwa Sudan linalodhibitiwa na jeshi la taifa.

Vikosi vya RSF vinavyodhibiti eneo la magharibi mwa jimbo la Kordofan kwa miezi kadhaa vimekuwa vikisonga mbele kuelekea upande wa mashariki katika majaribio ya kuuteka tena ukanda wa kati wa Sudan.

Jeshi la taifa kwa upande wake limefanikiwa kuvirudisha nyuma, vikosi hivyo vya RSF na kuuvunja mzingiro wa kijeshi katika miji miwili muhimu kwa lengo la kuukata mnyororo wa usambazaji wa vikosi vya RSF kuelekea Darfur.

Katika vita hivyo vya kugombea maeneo, pande zote mbili zimekuwa zikitegemea matumizi ya hali ya juu ya ndege zisizo na rubani, mashambulizi hayo yanayokosolewa mara kwa mara na Umoja wa Mataifa na kuwalaumu wafadhili wa kigeni wa vita hivyo.

Umoja wa Falme za Kiarabu umekanusha kwamba unawapa silaha wanamgambo wa RSF. Wakati huo huo jeshi linaloungwa mkono na Misri na Saudi Arabia, kihistoria limekuwa likitumia ndege zisizo na rubani kutoka Uturuki na Iran.

Kiongozi wa kijeshi nchini Sudan Jenerali Abdel Fattah Al-BurhanPicha: Sudanese Army/AFP

Kulingana na Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) pande zote mbili za jeshi linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhani na vikosi vya RSF vinavyoongozwa na Jenerali Mohammed Hamdani Daglo zinafanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika maeneo yote ya Sudan yanayosababisha vifo vya raia huku wengine wakijeruhiwa.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW