Mgogoro washtadi Ukraine
22 Januari 2014Habari juu ya mkutano baina ya Rais Yanukovich na wawakilishi wa upinzani zimethitishwa na aliekuwa waziri wa uchumi wa Ukraine. Mmoja wa viongozi muhimu wa upinzani Arseny Yatsenyuk pia amezitihibisha habari hizo.
Watatu wauawa:
Wakati huo huo mapambano baina ya polisi na waandamanaji yameendelea katika mji mkuu wa Ukraine Kiev ambako kwa mujibu wa habari watu watatu wameuawa.
Katika hotuba yake kwa baraza la mawaziri Waziri Mkuu Mykola Azarov alionyesha msimamo mkali dhidi ya waandamanaji wanaoipinga serikali. Waziri Mkuu huyo amewaita waandamanaji kuwa ni magaidi. Waandamanaji hao walikusanyika tena leo kulalamika juu ya vifo vya watu watatu vilivyotokea katika usiku wa kuamkia leo.
Katika hatua inayoashiria uwezekano wa serikali kuchukua msimamo mkali dhidi ya waandamanaji Waziri Mkuu Azarov amesema "magaidi" wanaoandamana kwenye uwanja wa Uhuru wa Maidan wamewateka watu kadhaa na kuwapiga.
Waziri Mkuu huyo amesema anatamka rasmi kwamba "wahalifu" hao watawajibishwa kwa yale waliyoyafanya. Waziri Mkuu huyo pia amewalaumu viongozi wa upinzani kwa alichokiita kuchochea vitendo vya kihalifu, kwa kutoa miito ya kufanya maandamano ya kuipinga serikali.Bwana Mykola Azarov amesema kwamba maandamanayo yanayochochewa na viongozi wa upinzani yanaiyumbusha Ukraine.
Umoja wa Ulaya watoa mwito wa mazungumzo
Umoja wa Ulaya umetoa mwito kwa serikali ya Ukraine wa kufanya mazungumzo ya dhati na viongozi wa upinzani. Mkuu wa sera za nje wa Umoja huo Cathrine Ashton amelaani vikali matumizi ya nguvu yaliyosabisha vifo vya watu watatu.Ashton amesema vifo vya watu hao ni jambo linalotia wasiwasi mkubwa .
Marekani yabatilisha viza kwa maafisa wa Ukraine
Kuhusu hatua za matumizi ya mabavu zinazochukuliwa na serikali ya nchini Ukraine, ubalozi wa Marekani nchini Ukraine umeamua kuzibatilisha viza kwa watu kadhaa wa nchi hiyo wanaohusiana na polisi waliofanya ukatili dhidi ya waandamanaji katika miezi ya Novemba na Desemba mwaka uliopita. Hata hivyo ubalozi wa Marekani haukuyataja majina ya watu hao lakini Marekani inafikiria kuchukua hatua nyingine dhidi ya wale wanaohusika na matendo ya kutumia nguvu yanayoendelea sasa dhidi ya waandamanaji.
Katika kadhia nyingine, Poland imemwita balozi wa Ukraine mjini Warsaw ili atoe maelezo juu ya hatua zilichokuliwa na polisi dhidi ya waandamanaji. Waandamanaji nchini Ukraine wamekuwa wanaendesha harakati dhidi ya serikali tokea mwezi wa Novemba mwaka jana kuupinga uamuzi wa Rais Viktor Yanukovich wa kukataa kuutia saini mkataba wa biashara na Umoja wa Ulaya.
Mwandishi: Abdu Mtullya
Mhariri: Josephat Charo