1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro watokota kati ya India na Pakistan

Zainab Aziz Mhariri: Saumu Yusuf
27 Februari 2019

Katika kadhia nyingine jeshi la anga la Pakistan limezitungua ndege mbili za kijeshi za India baada ya ndege hizo kuruka na kuvuka mpaka unaoyatenganisha mataifa hayo mawili katika jimbo la mzozo la Kashmir.

Indien, Kaschmir, Budgam: Indische Soldaten stehen neben den Trümmern des IAF-Hubschraubers
Picha: Reuters/D. Ismael

Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa jeshi la Pakistan marubani wawili wa India walitekwa. Kuzidi kwa uhasama baina ya mataifa hayo mawili yanayomiliki silaha za nyuklia kulitokea muda mfupi baada ya

Pakistan kusema kuwa India ilifanya mashambulio ya mizinga na kuwaua raia sita kwenye mpaka unaolitenganisha jimbo la utatanishi la Kashmir. Kwa mujibu wa msemaji huyo raia wengine kadhaa walijeruhiwa katika mashambulio hayo.

Msemaji wa jeshi la Pakistan Meja jenerali Ghafoor pia amefahamisha kwamba moja ya ndege za India iliyoangushwa na majeshi ya Pakistan iliangukia katika ardhi ya Pakistan na nyingine iliangukia katika upande wa Kashmir unaodhibitiwa na India.

Wizara ya mambo ya nje ya Pakistan imesema ndege za jeshi la nchi hiyo zimefanya mashambulio kutokea ndani ya anga ya Pakistan na kwamba mashambulio hayo siyo ya kulipiza kisasi kutokana na ilichokiita ushari wa India unaoendelea. Wizara hiyo imesisittiza katika tamko lake kwamba mashambulio yaliyofanywa leo na ndege za Pakistan yaliepuka kusababisha vifo vya raia.

Waziri Mkuu wa Pakistan Imran KhanPicha: picture-alliance/AP Photo/Yam G-Jun

Waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan anatarajiwa kuitisha kikao cha mamlaka ya kitaifa inayosimamia silaha za nyuklia ili kujadili jinsi ya kujibu mashambulio yanayoafanywa na ndege za India.China imezitaka India na Pakistan kujizuia kuingia katika mgogoro zaidi. Marekani pia imetoa wito sawa na wa China wa kuzitaka pande zote mbili zijizuie. Wakati huo huo India imevifunga viwanja vyake vinne vya ndege kutokana na wasiwasi wa usalama. Maeneo ya mipakani yamewekwa katika hali ya tahadhari.

Waziri wa mambo ya nje wa Pakistan Shah Mahmood Qureshi amesema anawasiliana na mawaziri wenzake duniani kote kujadili alichoita uchokozi wa India. Waziri huyo  amesema India inahatarisha amani katika  eneo lao kwa kufanya mashambulio ya ndege dhidi ya Pakistan.

Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa India  Sushma Swaraj amesema nchi yake haitaki  kuendelea kwa mgogoro na Pakistan na kwamba itaendelea kuchukua hatua za busara na kujizuia. Waziri Swaraj ameeleza kuwa mashambulio yaliyofanywa na ndege za nchi yake kwenye kambi ya mafunzo ya magaidi ndani ya Pakistan yalikuwa na lengo la kuchukua hatua kali ili kuiteketeza miundombinu ya kigaidi ya kundi la Jaish-e-Mohammad.

Vyanzo: /AP/DPA/AFP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW