1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgombea upinzani ashinda urais jimbo la Lagos

27 Februari 2023

Wakatu kura zikiendelea kuhesabiwa baada ya uchaguzi mkuu wa Nigeria, mgombea urais kupitia chama kidogo cha Labour ameshinda jimbo muhimu la Lagos, ingawa vyama vinalalamikia kasi ndogo ya utolewaji wa matokeo hayo.

Nigeria vor Präsidentschaftswahl Lagos | Kandidat Peter Obi
Picha: Sunday Alamba/AP/picture alliance

gombea urais wa chama cha Labour, Peter Obi, ambaye kampeni yake iliwavutia vijana na wapigakura wengi wa mijini waliochoshwa na ufisadi, alishinda kura nyingi kwenye jimbo muhimu la Lagos, mji mkubwa kabisa barani Afrika.

Obi alitangazwa kupata kura 582,454 akimshinda kwa karibu sana gavana wa zamani wa jimbo hilo, Bola Tinubu, ambaye alipata kura 572,606 kutoka chama tawala APC, kwa mujibu wa matangazo ya Tume ya Uchaguzi (INEC), huku Atiku Abubakar wa chama kikuu cha upinzani, PDP, akipata kura 75,750.

Soma zaidi: Matokeo yaanza kutangazwa uchaguzi wa Nigeria

Awali Lagos ilikuwa ngome ya Tinubu, ambaye pia ndiye mgombea urais kutokea chama tawala. 

Kampeni ya Obi kwa vijana 

Wafuasi wa Peter Obi wakati wa kampeni ya chama chao cha Labour mjini Lagos.Picha: Nyancho Nwanri/REUTERS

Obi alitumia kampeni yake kuwataka wapigakura kuvikataa vyama hivyo viwili ambavyo vimeitawala nchi hiyo yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika kwa robo karne sasa, na ambavyo chini ya utawala wao ufisadi umetamalaki na ukosefu wa usalama umesambaa kote nchini humo.

Mgombea huyo wa chama cha Labour alikuwa mashuhuri sana miongoni mwa vijana, hasa wa mijini, ambao wana kiwango kikubwa zaidi cha elimu na wenye fursa ya kutumia simu za mikononi na mitandao ya kijamii, lakini bado anakabiliwa na kibarua kigumu kwenye maeneo ya vijijini yenye wapigakura wahafidhina.

Kasi ndogo ya kuhesabu na kutangaza matokeo imekosolewa na vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi huo, ambavyo vinaikosoa Tume ya Uchaguzi kwa matayarisho dhaifu.

Uchaguzi wa amani

Takribani, watu milioni 90 waliandikishwa kupiga kura kwenye uchaguzi wa jana, Jumapili, kumpata mrithi wa Rais Muhammadu Buhari, wengi wakitarajia kiongozi wao mpya atayatatuwa matatizo ya ukosefu wa usalama, hali mbaya ya kiuchumi na kuenea kwa umasikini. 

Kwa sehemu kubwa, upigaji ulikwenda salama, ukiacha matukio machache ya washambuliaji waliovamia vituo vya kupigia kura, huku vituo vingi vikibakia wazi muda mrefu jijini Lagos na miji mingine.

Wapigakura wengi waliripotiwa kubakia vituoni usiku mzima kusimamia uhisabuji kura.

Soma zaidi: Zoezi la kuhesabu kura linaendelea nchini Nigeria
Nigeria yapiga kura kuchagua rais na bunge

Pamoja na kuibuka kwa chama kidogo cha Labour, bado kwa kiasi kikubwa, uchaguzi huu ni kinyang'anyiro baina ya gavana wa zamani wa Lagos, Bola Tinubu mwenye umri wa miaka 70, wa chama tawala cha APC, na makamu rais wa zamani, Atiku Abubakar, mwenye umri wa miaka 76, kutoka chama cha upinzani cha PDP.

Tume ya Uchaguzi ya  Nigeria ilianza kutangaza matokeo ya jimbo kwa jimbo kwa uchaguzi huo mkuu wa Jumamosi, lakini haifahamiki ikiwa itaweza kumtangaza mshindi rasmi wa uchaguzi ndani ya siku chache zijazo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW