1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgombea urais wa upinzani Cameroon ajitangazia ushindi

14 Oktoba 2025

Mgombea urais wa upinzani nchini Cameroon Issa Tchiroma Bakary, amejitangazia ushindi dhidi ya Rais aliyeko madarakani Paul Biya, baada ya taifa hilo kushiriki uchaguzi siku ya Jumapili (12.10.2025).

Cameroon, Yaounde 2025 | Issa Tchiroma Bakary mgombea urais wa upinzani
Mgombea urais wa upinzani nchini Cameroon, Issa Tchiroma Bakary Picha: Daniel Beloumou Olomo/AFP

Katika chapisho kwenye mtandao wa Facebook, Tchiroma alitangaza kwamba ushindi wao uko wazi na unapaswa kuheshimiwa.

Ameihimiza serikali kukubali ukweli wa matokeo ya uchaguzi  ama kuitumbukiza nchi kwenye machafuko.

Tchiroma ameahidi kuchapisha matokeo ya kina kulingana na mikoa na akaongeza kusema watu wamefanya chaguo lao.

Picha za karatasi za kujumlisha kura zasambazwa mitandaoni

Picha za karatasi na ubao wa kujumlisha matokeo zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii, na kuchochea madai ya ushindi kati ya kambi za Biya na Tchiroma.

Ingawa karatasi hizo za kujumlisha kura zinaruhusiwa kuchapishwa, matokeo rasmi ya mwisho lazima yatangazwe na Baraza la Kikatiba la nchi ambayo kulingana na serikali ni hatua isiyopaswa kukiukwa.

Biya alikabiliana na wapinzani 11, akiwemo Tchiroma, ambaye alijiuzulu kutoka serikalini mwezi Juni na kujiunga na upinzani baada ya miaka 20 ya kuwa upande wa Biya.

Kabla ya zoezi hilo la kura, mwanasayansi wa siasa wa Cameroon Stephane Akoa, aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba hawapaswi kuwa wajinga na akasema wanajuwa vyema mfumo unaotawala una njia za kutosha za kujipatia matokeo bora ya kura hiyo .

Mafisa wa uchaguzi nchini Cameroon tayari kwa zoezi la kuhesabu kura mjini YaoundePicha: Wang Ze/IMAGO

Lakini alisema kampeni ilikuwa imechangamka katika siku za mwisho kuliko ilivyo kawaida ya hatua hiyo hivyo basi uchaguzi huo una uwezekano mkubwa wa kuwashangaza watu.

Wengi wa raia milioni nane wa nchi hiyo walioruhusiwa kupiga kura katika uchaguzi huo wa Jumapili, wamemjua mtawala mmoja tu katika maisha yao.

Katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2018, mgombea wa upinzani Maurice Kamto alijitangazia ushindi siku moja baada ya kupiga kura.

Baadaye alikamatwa na mikutano ya wafuasi wake ikatawanywa kwa mabomu ya machozi na maji ya kuwasha, huku baadhi wakikamatwa.

Biya ameongoza Cameroon kwa mkono wa chuma

Biya, Rais wa pili wa nchi hiyo tangu ilipopata uhuru wake kutoka kwa Ufaransa mwaka 1960, ametawala kwa mkono wa chuma, akiwateua binafsi na kuwafukuza kazi maafisa wakuu pamoja na kuwakandamiza bila huruma wapinzani wote wa kisiasa .

Amefanikiwa kushikilia mamlaka kupitia misukosuko ya kijamii, tofauti za kiuchumi na vurugu za kujitenga.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW