1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaVenezuela

Mgombea urais wa upinzani Venezuela akimbilia Uhispania

9 Septemba 2024

Aliyekuwa mgombea urais wa upande wa upinzani nchini Venezuela Edmundo Gonzalez ameikimbia nchi hiyo na kwenda Uhispania kuomba hifadhi.

Aliyekuwa mgombea wa upinzani Venezuela, Edmundo González
Aliyekuwa mgombea urais wa upande wa upinzani nchini Venezuela Edmundo Gonzalez.Picha: Leonardo Fernandez Viloria/REUTERS

Hiyo inafuatia mzozo wa kisiasa na kidiplomasia ulioibuka baada ya uchaguzi wa mwezi Julai ambao matokeo yake yanazozaniwa.

Gonzalez - aliyechuana na Rais Nicolas Maduro ambaye alitangazwa mshindi wa uchaguzi huo - aliwasili Uhispania jana akiwa amefuatana na mkewe. Taarifa za kuwasili kwake zimetangazwa na Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Uhispania.

Baadaye mwenyewe alituma ujumbe kwa wafuasi wake akiwaarifu kwamba amelazimika kuondoka Venezuela kutokana na vitisho na ukandamizaji lakini amewahikishia ataendelea kupambana kurejesha demokrasia nchini humo.

Upinzani nchini Venezuela unasema matokeo ya uchaguzi wa Julai 28 yalimpatia ushindi Gonzalezna wamechapisha mtandao matokeo ya hesabu za kura wanazosisitiza zinaonesha ushindi wao.

Rais Maduro ameyapinga madai hayo na kusema kulikuwa na njama kutoka wanasiasa wa mrengo wa kulia kuihujumu serikali yake.

Machado: Gonzalez amekimbia vitisho na ulaghai wa mamlaka za Venezuela

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela.Picha: Jeampier Arguinzones/dpa/picture alliance

Uamuzi wa Gonzalez kuhamia Uhispania ni mtikisiko mwingine katika maisha ya mwanadiplomasia huyo wa zamani ambaye aliukacha ustaafu na kujitwika jukumu la kugombea urais wa Venezuela kwa tiketi ya upinzani mnamo mwezi Machi.

Alikubali kuchukua nafasi hiyo baada ya kiongozi wa upinzani Maria Corina Machado na mwanasiasa mwengine aliyeteuliwa na upinzani kugombea urais kuzuiwa kusimama kwenye uchaguzi huo.

Machado ameandika kupitia ukurasa wake wa X kwamba Gonzalez yuko Uhispania na kuongeza kwamba amelazimika kukimbia ili kulinda "uhuru, uadilifu na maisha yake".

"Ongezeko la vitisho, miito polisi, hati za kukamatwa na hata majaribio ya kutaka kumlaghai na kumshinikiza awe mtiifu vinaonesha jinsi utawala ulivyokosa mipaka wala haya katika shauku yao ya kumnyamazisha na kujaribu kumvunja moyo," ameandika Machado.

Mazungumzo ya Gonzalez kuhamia Uhispania yalifanyika kwa siku kadhaa

Waziri wa mambo ya kigeni wa Uhispania Jose Manuel Albares amekiambia kituo kimoja cha televisheni nchini humo kwamba alimweleza Gonzalez kuwa "mtu yeyote anayetishiwa kushambuliwa kimwili au kuvunjiwa haki zake anakaribishwa Uhispania na kwenye balozi zake."

Kiongozi wa upinzani nchini Venezuela, Maria Corina Machado.Picha: Ariana Cubillos/AP Photo/picture alliance

Amesema mipango ya kumruhusu kwenda Uhispania iliandaliwa kwa siku kadhaa na kwamba mchakato wa kumpatia hifadhi ya kisiasa unaanza mara moja.

Gonzalez alianza kutafuta hifadhi kwenye balozi za Uhispania na Uholanzi nchini Venezuela baada tu ya uchaguzi. Maafisa wa nchi hizo mbili wamefahamisha. Waziri wa mambo ya kigeni wa Uholanzi Caspar Veldkamp ameliambia bunge la nchi yake kuwa mwanzoni mwa mwezi Septemba, Gonzalez aliashiria dhamira yake ya kuondoka na kuendelea na mapambano yake nchini Uhispania.

Maafisa wa Uhispania ikiwemo Waziri Mkuu wa zamani Jose Luis Rodriguez Zapatero, aliyekuwa zamani na mahusiano mazuri ya kidiplomasia na Venezuela alihusika kwenye mazungumzo ya wiki nzima na watawala mjini Caracas ili zimruhusu Gonzalez kuondoka.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW