Mgomo kuendelea Afrika Kusini ?
2 Septemba 2010Taarifa kutoka Johannesberg, zinasema sehemu kubwa ya vyama vya wafanyikazi vyenye sauti kubwa ndani ya Shirikisho la COSATU,imepiga kura kukataa nyongeza ya 7.5% ya mishahara iliopendekezwa jana na serikali.Hatahivyo, viongozi wa vyama hivyo wamepanga kukutana na wajumbe wa serikali leo na wanaozungumza nao licha ya kukataa nyongeza hiyo.
Sehemu kubwa ya vyama vya wafanyikazi milioni 1.3 waliogoma kwa wiki 3 sasa , ikidai nyongeza ya mishahara ya hadi kima cha 8.6 asili-mia na posho la nyumba la kiasi cha Rand 1.000, wamepiga kura kukataa nyongeza iliopendekezwa na serikali ya Rais Jacob Zuma.Hivyo, mgomo huu wa watumishi serikalini unaoathiri hasa sekta ya afya na elimu, unaonesha kuendelea na kuigharimu serikali hadi dala milioni 150 kwa siku-hii ni kwa muujibu wa makisio ya mtaalamu mashuhuri wa wa kiuchumi nchini Afrika Kusini.
Mgomo huu umeodosha ile shauku iliokuwapo nchini kutokana na kuandaa kwa ufanisi Kombe la dunia la FIFA,Juni hadi July, mwaka huu.Umesababisha kufungwa kwa mashule,umeoongoza maiti kurundikana katika Majumba ya kuhifadhia maiti na kuchafua pia nia ya wawekezaji.
"Nyuma ya pazia kuna mazungumzo ya kisiasa yanaendelea na siwezi kutoa maelezo zaidi ,lakini viongozi wataendelea kusaka ufumbuzi." Katibu Mkuu wa Shirikisho la vyama vya wafanyikazi nchini COSATU, Zwelinzima Vavi , aliliambia shirika la habari la Reuters.
Kikao rasmi cha mapatano baina ya vyama vya wafanyikazi na serikali, kimepangwa kufanyika leo .Serikali iliojitolea kutoa nyongeza ya 7.5 % na Rand 800- sawa na dala 110 kwa mwezi ikiwa ni posho kwa nyumba, imearifu kwamba haimudu kuzidisha nyongeza iliopendekeza.Serikali, inadai, italazimika kubana matumizi na kusaka mikopo ili kugharimia hiyo nyongeza iliopendekeza.
Vyama vya wafanyikazi , vinavyowakilisha askari wa magereza, walimu wa shule,wauguzi wa hospitali na maafisa wa Idara ya Uhamiaji, wakidai nyongeza ya hadi 8.6 asili-mia ambayo, inapindukia mno kima cha mfumko wa bei cha 3.7 asili-mia.
Kitisho cha mgomo wa wafanyikazi kuweza kuungwamkono na wanachama wote milioni 2 wa Shirikisho la COSATU,kilizimwa kwa muda jana na hivyo, kuondosha hofu ya mgomo mkubwa zaidi ambao ungeathiri shughuli za migodi na za viwandani-shina kuu la uchumi wa Afrika Kusini.
Viongozi wa vyama vya wafanyikazi ,wamearifu kwamba, wataendelea kushauriana na wanachama wao na duru za vyama hivyo zinahisi kwamba, pendekezo la nyongeza la serikali, halikuelezwa barabara kufahamika kwa wanachama hao ili kuliridhia. Hii ni dalili kwamba, wanajaribu sasa kuitia-munda kura ya jana ya wafanyikazi.
Mwandishi: Ramadhan Ali /RTRE
Uhariri: Abdul-rahman