Mgomo wa kitaifa Ugiriki
6 Oktoba 2011Safari zote za ndege ziliahirishwa na treni zilisita kusafiri, wakati shule na mahakama zilifungwa.
Serikali imetangaza kupunguza nafasi za ajira na mishahara, pamoja na kuongeza kodi, ili iweze kupata awamu nyengine ya mkopo wenye thamani ya euro bilioni 8.
Wakaguzi wa hesabu wa wakopeshaji wa kimataifa kwa Ugiriki, ambao ni Umoja wa Ulaya, Shirika la fedha la kimataifa, IMF, na benki kuu ya Ulaya, siku ya Jumanne waliahirisha uamuzi wa kutoa mkopo huo mwingine wakisisitiza kuwa Ugiriki itekeleza hatua zote zilizokubaliwa mwaka uliopita, ili iweze kupewa mkopo wa euro bilioni 110.
Iwapo Ugiriki haitopokea mkopo huo wa euro bilioni 8 kufikia mwezi ujao, itashindwa kuwalipa wafanyakazi wa serikali na malipo ya pensheni.
Mwandishi Maryam Abdalla/alle