1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgomo wa kitaifa wa vyuo vikuu waanza Kenya

Shisia Wasilwa
17 Septemba 2025

Mgomo wa kitaifa wa vyuo vikuu nchini Kenya umeanza baada ya mazungumzo kati ya vyama vya wahadhiri na serikali kuvunjika.

Wanafunzi wa chuo kikuu wakiwa darasani
Wanafunzi wa chuo kikuu wakiwa darasaniPicha: Tafara Mugwara/Xinhua/imago images

Pande zote mbili zinailaumu Tume ya Kuratibu Mishahara na Marupurupu ya wafanyikazi wa umma kwa kukwamisha suluhu ya mzozo huo.

Wafanyikazi wa Vyuo Vikuu wanadai malimbikizi ya mishahara ya shilingi bilioni mbili za Kenya.

Matakwa ya vyama vya wahadhiri kutimizwa

Chama cha Wahadhiri wa Vyuo Vikuu nchini Kenya, UASU na Chama cha Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu nchini Kenya (KUSU) vimetangaza kuwa wahadhiri wamesitisha huduma zao hadi madai matatu ya msingi yatakapotimizwa:

Lango la chuo kikuu cha Garissa huko KenyaPicha: Imago/Xinhua

Kutolewa  kwa shilingi bilioni 2.73 kutoka Awamu ya Piliya mkataba wa maelewano ya pamoja wa mwaka 2021–2025 uliopaswa kulipwa Julai mwaka huu, kulipwa kwa deni la shilingi bilioni 7.9 la mkataba wa mwaka 2017–2021, na kuanza kwa mazungumzo na usajili wa mkataba mpya wa 2025–2029.

Katibu Mkuu wa UASU, Constantine Wasonga, ameilaumu Tume ya Kuratibu Mishahara ya Wafanyikazi wa Umma kwa kupuuza maagizo ya mahakama yaliyotaka fedha zitengwe kwa ajili ya mikataba hiyo ya CBA. Mgomo huo unatarajiwa kuvuruga masomo ya maelfu ya wanafunzi kote nchini, ikivihusisha vyuo vikuu takriban 45.

"Hatuwezi kusubiri kwa muda mrefu, lakini usishangae maanake tumeuzoea mchezo huu, hakuna mkataba wa maelewano katika vyuo vikuu ambao tumesaini bila kufanya mgomo. Sababu wanataka mgomo sasa tutacheza huo mchezo,” alisema Wasonga.

Dkt. Wasonga alikataa kikao cha mazungumzo kilichoitishwa Ijumaa na Jukwaa la Mashauriano la Baraza la Vyuo Vikuu vya Umma akikitaja kuwa ni mchezo wa kisiasa,wenye hadaa nyingi,  akisema hakukuwa na mapendekezo madhubuti yaliyowasilishwa.

Alisema kuwa wahadhiri hawali kauli za nia na kuongeza kuwa wahadhiri hawali ahadi zisizo na utekelezaji. Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu ya Juu, Beatrice Inyangala, kwa upande wake, ameonyesha matumaini kuwa kumekuwa na maendeleo katika mazungumzo hayo. 

Vyuo vikuu kufunguliwa kwa muhula mpya

Wakati huo huo Hazina Kuu imetoa shilingi bilioni 2.5 za Kenya kulipa sehemu ya malimbikizi ya mishahara ya wahadhiri katika juhudi za dakika za mwisho za kuzuia mgomo wa kitaifa. Katibu Mkuu wa KUSU, Charles Mukhwaya, aliunga mkono msimamo wa UASU, akiilaumu serikali kwa kuidharau sekta ya elimu ya juu.

Wanafunzi wakiwa ndani ya basi la chuo kikuu cha NairobiPicha: picture-alliance/AP Photo/Azim

"Leo tunaanza mgomo sababu ya serikali kushindwa kutekeleza mkataba wa maelewano wa malimbikizi ya mishahara awamu ya pili mwaka 2021-2025, katika kipindi cha mwaka 2025-2026, ya kima cha shilingi bilioni 2.7,” alisema Mukhwaya.

Mgomo huu unajitokeza siku chache baada ya vyuo vikuu kufunguliwa kwa muhula mpya wa masomo, hali inayozua hofu ya kuvurugika kwa mara nyingine kwa kalenda ya masomo. 

Mwaka jana, wahadhiri walilemaza shughuli za vyuo kwa mgomo wa wiki mbili uliositishwa baada tu ya  Wizara ya Leba, Shirikisho la Waajiri nchini Kenya na Vyama vya Vyuo Vikuu kuingilia kati.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW