1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgomo wa madaktari waumiza wagonjwa Kenya

30 Aprili 2024

Wagonjwa wa maradhi mbalimbali pwani ya Kenya wameathirika sana kutokana na mgomo wa madaktari unaoendelea, huku mripuko wa magonjwa ya kuharisha na kutapika ukishuhudiwa kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Madaktari wakiendelea na maandamano na mgomo nchini Kenya.
Madaktari wakiendelea na maandamano na mgomo nchini Kenya.Picha: DANIEL IRUNGU/EPA

Katika Hospitali Kuu ya Pwani iliyopo kwenye Kaunti ya Mombasa, wagonjwa bado wanaendelea kuteseka huku wakipigania kupata huduma za matibabu wakati mgomo wa madaktari ukiendelea nchini.

Sasa hospitali hiyo haina zile pirika pirika zake za kawaida. Vyumba na vitanda ni vitupu na inadhihirika wazi kuwa hospitali hiyo inahudumia tu wagonjwa walio katika hali mahututi.

Kulingana na baadhi ya wagonjwa, mgomo huo, ambao umedumu zaidi ya mwezi mmoja sasa, umezilazimisha familia nyingi kuchukuwa jukumu la kuwatunza wenyewe wagojwa wao majumbani, kwani hawawezi kumudu huduma za afya za kibinafsi.

Uamuzi huo, hata hivyo, umesababisha machungu kwa familia nyengine kuwapoteza wapendwa wao.

Vifo vya majumbani

Miongoni mwao ni ile ya Mwanaisha kutoka Mtaa wa Kisauni, ambaye amepoteza mpendwa wake baada ya kukosa huduma za matibabu.

Madaktari wakiendelea na maandamano na mgomo nchini Kenya.Picha: DANIEL IRUNGU/EPA

Wifi yake, ambaye awali alikuwa na afya njema, alipatwa na mshtuko wa moyo na kupooza ghafla.

"Tulipompeleka hospitalini, hakuweza kupata matibabu kama kawaida kwa sababu ya mgomo wa madaktari, na hatimaye akafariki dunia, akiwa nyumbani." Anasema Mwanaisha, ambaye ni mmoja tu kati ya wengi wanaoendelea kutaabika, hasa kwa kupoteza wapendwa wao.

Patrick Ndegwa kutoka Changamwe yuko nje ya chumba cha kuhifadhia maiti akisubiri kuchukua mpendwa wao kwa mazishi, baada ya kuteseka kwa mwezi mmoja. Wakati huo huo, familia nyingine imeenda kutoa heshima za mwisho.

Haya yanajiri wakati mripuko wa magonjwa mbalimbali, yakiwemo ya kuharisha na kutapika hususani kwa watoto, unaendelea kuripotiwa, na hii imechangiwa sana na mabadiliko ya hali ya hewa.

"Hali hii imelazimisha familia nyingi zilizo na uwezo wa kifedha kutafuta matibabu katika hospitali za kibinafsi, ambazo gharama zake ni kubwa kuliko zile za umma," anasema Daktari Hemed Twahir, bingwa wa magonjwa ya daktari wa watoto mjini Mombasa.

Wananchi wanasisitiza kuwa kuna haja ya hatua za haraka kutoka serikalini ili kutatua suala hili la mgomo wa madaktari, kwani watu wengi wanazidi kupoteza wapendwa wao.