1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgomo wa wafanyikazi Ujerumani watishia kuvuruga usafiri

15 Februari 2023

Mipango ya safari huenda ikaharibika kutokana na mgomo wa wafanyakazi wa viwanja vya ndege hapa Ujerumani, ikiwa ni siku nne tu baada ya mgomo wa vyombo vya usafiri wa umma katika jimbo la North-Rhine Westphalia.

Deutschland Berlinb | Streik der Deutschen Bahn
Picha: Michael Sohn/AP/picture alliance

Viwanja vikubwa vya ndege vya Frankfurt, Munich, Hamburg, Stuttgart, Hannover na Bremen ni miongoni mwa vile vitakavyoshuhudia mgomo huo mkubwa wa wafanyakazi siku ya Ijumaa, na tayari wasafiri wameshatumiwa onyo la uwezekano mkubwa wa kufutwa na ama kucheleweshwa kwa safari zao.

Shughuli pekee ambazo zitaruhusiwa kuendelea na waandaaji wa mgomo huo ni zile zinazohusiana na utumaji wa misaada kwa waathirika wa tetemeko la ardhi nchini Uturuki na Syria.

Soma pia: Safari za ndege zafutwa Ujerumani kutokana na mgomo

Mgomo huu unazidisha mtafaruku kati ya vyama vya wafanyakazi na serikali kuu ya Ujerumani na za majimbo wakati kukitazamiwa duru mpya ya majadiliano juu ya mkataba wa miezi 12 ya mapatano kwa wafanyakazi wa sekta ya umma hapo tarehe 22 na 23 mwezi huu.

Chama cha wafanyakazi, Verdi, na Jumuiya ya Huduma za Anga, DBB, vinataka ongezeko la asilimia 10.5 au kima cha chini cha euro 537 kwa takribani wafanyakazi milioni 2.5 wa umma.

Mbali na mazungumzo hayo juu ya sekta ya umma, makubaliano ya mapatano ya pamoja yanaendelea kujadiliwa kwa ajili ya walinzi wa viwanja vya ndege walioajiriwa na serikali kuu na wenzao walioajiriwa na serikali za majimbo.

Shughuli za uchukuzi wa umma zatatizika North-Rhine Westphalia

Picha: Daniel Bockwoldt/dpa/picture alliance

Hii si mara ya kwanza kufanyika kwa migomo kwenye sekta ya usafiri katika siku za hivi karibuni. Katika jimbo lenye watu wengi zaidi la North-Rhine Westphalia, hapo jana kulifanyika mgomo mkubwa wa vyombo vya usafiri wa umma, kwa madai hayo hayo ya ongezeko la mishahara kwa wafanyakazi. Mwezi uliopita, kulikuwa na migomo pia kwenye viwanja vya ndege vya Berlin na Dusseldorf.

Naibu Mwenyekiti wa chama kikuu cha wafanyakazi cha Verdi, Christine Behle, amesema kwenye taarifa yake, "Kupanda kwa gharama za maisha, bei za juu za nishati na vyakula kumewaweka wafanyakazi wengi kwenye hali mbaya kabisa kuwahi kushuhudiwa, kiasi cha kwamba wengi wao hawajui vipi walipie nyumba wala chakula chao. Wanahitaji pesa zaidi ili kujikimu maisha yao." 

Ujerumani inakabiliwa na upungufu mkubwa wa wafanyakazi wa viwanja vya ndege, na Verdi inasema njia pekee ya kulitatuwa tatizo hilo ni kupandisha mshahara.

Soma pia: Lufthansa yafuta karibu safari zote za ndege sababu ya mgomo

Wachambuzi wa masuala ya usafiri wa anga wanasema mgomo wa siku ya Ijumaa unatazamiwa kuathiri pakubwa shughuli za usafiri wa ndani na njia zenyewe za angani, kwani kutahitajika wahudumu wengi zaidi kuzifanya njia za angani kubaki salama.

Chama kikuu cha wafanyakazi cha Verdi kina dhima kubwa kwenye miundombinu ya njia za safari za angani kwani wanachama wake wanawakilishwa chini ya makubaliano ya mshahara wa wafanyakazi wa umma.

Mwezi Aprili 2018, safari zinazokaribia elfu moja za ndege zilifutwa kote Ujerumani baada ya majadiliano juu ya mapatano ya pamoja kufeli. Makumi kwa maelfu ya wafanyakazi kwenye majimbo manane waliacha kazi. Mbali na viwanja vya ndege, huduma za usafiri wa umma, vituo vya kulelea watoto, kliniki na mabwawa ya kuongelea pia ziliathirika.