1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgonjwa wa kwanza Hamburg wa Corona ni daktari

28 Februari 2020

Waziri wa afya mjini Hamburg ameuambia mkutano wa waandishi habari kwamba mtu wa kwanza kuambukizwa virusi vya Corona Kaskazini mwa Ujerumani ni daktari anayefanya kazi katika hospitali ya chuo kikuu cha Hamburg.

Erster Coronavirus-Fall in Hamburg bestätigt
Picha: picture-alliance/dpa/G. Wendt

Waziri huyo wa afya wa Hamburg nchini Ujerumani Cornelia Pruefer-Storcks amesema wagonjwa takriban 50 waliokutana na daktari huyo wamejulikana  na kuwekwa karantini  kwa siku 14 huku idadi ya watu walioambukzwa ikipanda na kufikia zaidi ya 60.

Virusi hivyo vimethibitishwa kusambaa katika miji kadhaa nchini Ujerumani ikiwa ni pamoja na Hesse, Baden-Wuerttemberg na Bavaria Waziri wa afya nchini humo Jens Spahn amesema wiki hii taifa kubwa barani ulaya lipo hatarini kukumbwa na janga hilo kubwa la virusi vya Corona.

Serikali ya Ujerumani kwa sasa imetoa wito kwa majimbo yote 16 kutangaza mipango yao ya namna yalivyojitayarisha kukabiliana na janga hilo, huku maonyesho makubwa ya kimataifa ya utalii ITB yakitarajiwa kufutiliwa mbali siku kadhaa kabla ya kuanza rasmi mjini Berlin wiki ijayo.

Nchini Iran hali bado ni mbaya kufuatia watu 26 kufariki kutokana na virusi hivyo. Waziri wa afya wa taifa hilo Saeed Namaki ametangaza shule zote nchini humo kufungwa kwa siku tatu kuanzia kesho Jumamosi kufuatia wasiwasi wa virusi hivyo kusambaa zaidi katika Jamhuri hiyo ya kiislamu.

Mataifa mengi zaidi duniani yaripoti visa vya virusi vya Corona

Kwengineko wageni  katika hotel mbili mjini Abu dhabi walioingiliana na waendesha baiskili wawili kutoka Italia waliothibitishwa kuambukizwa virusi vya Corona wako karantini katika hoteli hizo kwa siku 14 ambapo ndio muda mtu anaeweza kugundua iwapo ameambukizwa au la.

Awamu zengine mbili za mashindano ya basikeli yanayofanyika katika nchi ya Umoja wa Falme za kiarabu zimefutwa baada ya washiriki wake wawili kuambukizwa virusi vya Corona.

Dunia bado inaendelea kukumbwa na kitisho hicho cha Corona. Belarus na Azerbaijan zimeripoti hii leo visa vya kwanza vya Corona pamoja pia na Nigeria ambayo imekuwa nchi ya kwanza katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara kukumbwa na virusi hivyo. Georgia nayo imeripoti kisa chake cha pili huku ikisema watu wengine walioko karantini huenda wakapatikana na virusi hivyo.

Nchini Mexico hali ni ya wasiwasi baada ya waziri wa afya kutangaza kwamba taifa hilo sasa lina wagonjwa wawili wa virusi vya Corona. Waziri Hugo Lopez-Gatell amesema mgonjwa mmoja yupo mjini Mexico city  na mwengine akiwa katika jimbo la Kaskazini la Sinaloa. 

Shirika la Afya Duniani WHO limesema idadi ya watu walioambukizwa virusi hivyo ulimwenguni ni zaidi ya 83,000.

Chanzo: AP/AFP/Reuters