Wachunguzi wasema kuwa Urusi ilidengua ndege ya Malaysia
25 Mei 2018Hata hivyo Urusi, imekanusha kuhusika kwenye kisa hicho ambacho ndege aina ya MH17 ilisababisha vifo vya watu wote 298 waliokuwa wameiabiri.
Aidha wachunguzi hao walitambua washukiwa wawili wakuu ambao mazungumzo yao yalidukuliwa kabla na baada ya ndege hiyo kudunguliwa angani.
Siku iliyofuatia Uholanzi na Australia zilisema kuwa Urusi iliwajibika kwenye mkasa huo.
Yafuatayo ni baadhi ya matukio muhimu:
Julai 17, 2014 Ndege la Shirika la Malaysia Boeing 777 -- lililokuwa limepangiwa kutoka Amsterdam kuelekea Kuala Lumpur -- lilianguka Donetsk, mashariki mwa eneo hilo ambapo waasi waliojitenga wanaunga mkono Urusi walikuwa wakikabiliana na wanajeshi wa Ukraine.
Thuluthi mbili ya raia wa Uholanzi waliaga dunia pamoja na yumkini raia 30 wa Australia na 30 wa Malaysia, huku raia wengi wakiwa na uraia mara mbili.
Rais wa Ukraine Petro Poroshenko alikitaja kuwa "kitendo cha ugaidi".
Waasi wanaounga Urusi katika eneo hilo walidai kuwa ndege hiyo iliangushwa na ndege la jeshi ya Ukraine. Rais wa Urusi Vladimir Putin anasema kuwa Ukraine "inawajibika".
Siku iliyofuatia rais wa Marekani Barack Obama alisema kuwa kombora lililorushwa na waasi waliojitenga kwenye himaya hiyo walihusika na waasi hao hawangefaulu bila ya kuungwa mkono na Urusi.
Mwezi Septemba 2014 ripoti ya kwanza kutolewa na OVV inasema kuwa MH17 ilivunjika ikiwa angani baada ya kugongwa na chombo kilichokuwa kinakwenda kwa kasi angani.
Julai 2015 Urusi inapiga kura ya turufu kupinga Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lilikuwa limependekeza kuanzisha jopo maalum la kuwahukumu wale waliohusika. Mapendekezo hayo yalikuwa yametayarishwa na Australia, Ubelgiji, Malaysia, Uholanzi na Ukraine.
Agosti, wachanguzi walitambua vipande saba vikubwa ambavyo huenda vilitoka kwenye kombora ambalo linamilikiwa na Urusi.
Oktoba wachunguzi walihitimisha kuwa ndege hiyo iliangushwa na kombora kutoka Mashariki ya Ukraine anasema mweyekiti wa Bodi ya Usalama ya Uholanzi Tjibbe Joustra.
Septemba 2016 wachunguzi kutoka Uholanzi walisema kuwa wana ushahidi wa kutosha kwamba kombora lililotumika lilitoka katika himaya ya shirikisho la Urusi.
Moscow ilielezea uchunguzi huo kuwa ulioegemea upande mmoja na uliochochewa kisiasa.
Mei 24, 2018 wachunguzi walisema kuwa kombora ambalo lilirushwa na jeshi la Urusi liliko katika kambi ya Kursk. Hii ni baada ya kikundi cha wachunguzi kufanya uchunguzi wa kina kwa kutumia video na picha.
Mwandishi: Shisia Wasilwa, Afp, Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef