Mhafidhina Ebrahim Raisi ashinda kura ya urais Iran
19 Juni 2021Maafisa wa uchaguzi wamesema Raisi ameshinda asilimia 62 ya kura baada ya kuhesabiwa takribani asilimia 90 ya kura kutoka uchaguzi wa Ijumaa, bila hata hivyo kutangaza takwimu kuhusu kiwango cha ushiriki wa wapigakura, baada ya wagombea wengine watatu kukubali kushindwa.
"Nawapongeza watu kwa chaguo lao," alisema rais anaemaliza muda wake Hassan Rouhani, ambaye amehudumu mihula miwili mfululizo na ataondoka madarakani mwezi Agosti.
Raisi mwenye umri wa miaka 60, anachukuwa madaraka katika wakati nyeti, wakati ambapo Iran inatafuta kuokoa makubaliano yaliosambaratika ya nyuklia iliyofikia na mataifa makubwa na kujitoa katika vikwazo vikali vya Marekani ambavyo vimesababisha kuporomoka vibaya kwa uchumi wake.
Kiongozi huyo wa mahakama nchini Iran, ambaye kilemba chake cheusi kinaashiria "nasaba ya moja kwa moja na Mtume Muhammad", anatazamwa kama mshirika wa karibu wa kiongozi wa juu kabisa wa Iran mwenye umri wa miaka 81, Ayatollah Ali Khamenei, ambaye ndiye mamlaka ya mwisho nchini humo.
Uchaguzi wa Ijumaa ulisogezwa mbele kwa masaa mawili zaidi ya muda wake wa awali wa usiku wa manane, katikati mwa hofu juu ya uitikiaji mdogo wa asilimia 50 ya chini.
Soma pia:Iran yaandaa uchaguzi wa rais
Wapigakura wengi waliamua kutoshiriki baada ya uwanja wa wagombea karibu 600 wakiwemo wanawake 40, kupunguzwa hadi wagombea saba, wote wanaume, na kumuondoa pia rais wa zamani na spika wa zamani wa bunge.
Watatu kati ya wagombea waliochujwa walijitoa kwenye kinyang'anyiro siku mbili kabla ya uchaguzi wa Ijumaa.
'Sitaki kuwa sehemu ya zambi hii'
Rais wa zamani mwenye itikadi kali, Mahmoud Ahmadnejad, mmoja wa waliozuwiwa kugombea na Baraza la Usimamizi la makasisi na wanasheria, alisema hangeweza kupiga kura, akitangaza katika ujumbe wa vidio: "Sitaki kuwa sehemu ya zambi hii."
Ushindi wa Raisi ulithibitishwa Jumamosi wakati alipopokea pongezi za rais wa sasa na wagombea wengine watatu -- wahafadhina wenye msimamo mkali Mohsen Rezai na Amirhossein Qazizadeh Hashemi, na mwanamageuzi Abdolnasser Hemmati.
Khamenei amesifu uchaguzi huo akisema kwamba "mshindi mkubwa...ni taifa la Iran kwa sababu limeinuka tena mbele ya propaganda za vyombo mamluki vya habari vya maadui."
Soma pia: Wahafidhina wanaongoza katika orodha ya wagombea urais Iran
Katika siku ya uchaguzi, picha za wapigakura ambao aghalabu wanapeperusha bendera zilihanikiza ripoti za televisheni, lakini mbali kutoka vituo vya kupigia kura, baadhi walielezea hasira dhidi ya kile wlaichokiona kama uchaguzi wa kupangwa.
"Nipige kura au nisipige, tayari mtu mmoja amechguliwa," alilalamika muuza duka mjini Tehran Saaed Zareie. "Wanapanga uchaguzi kwa ajili ya vyombo vya habari."
Shauku ilipunguzwa zaidi na mfumuko wa bei unaozidi na kupotea kwa nafasi za ajira, wakati ambapo janga la ugonjwa wa Covid-19 likionesha makali zaidi nchini Iran kuliko kokote kwingine katika kanda, likiuwa zaidi ya watu 80,000 kwa mujibu wa hesabu rasmi.
Miongoni mwa waliopanga foreni kupiga kura katika vituo vya shuleni, misikitini na vituo vya kijamii, wengi walismea walimuunga mkono Raisi, ambaye ameahidi kupambana dhidi ya rushwa, kuwasaidia maskini na kujenga mamilioni ya ghoroga kwa ajili ya familia zenye kipato cha chini.
Muuguzi kwa jina la Sahebiyan alisema alimuunga mkono kutokana na sifa zake za kupambana na rushwa na kwa matumaini kwamba angeipeleka mbele nchi ... na kuwanusuru watu kutokana na ukosefu wa kiuchumi, kitamaduni na kijamii."
Mrithi ajaye wa Khamenei?
Raisi ambaye ana mitazamo mikali ya kihafidhina kuhusu masuala mengi ya kijamii, ikiwemo jukumu la wanawake katika maisha ya umma, ametajwa katika vyombo vya habari kama mwenye uwezekano wa kumrithi Khamenei.
Kwa wapinzani na mashirika ya haki za binadamu lakini, jina lake linahusishwa na mauaji makubwa ya wafungwa wa kisiasa mnamo mwaka 1988. Serikali ya Marekani ilimuwekea vikwazo kuhusiana na safisha safisha hiyo, ambamo Raisi amekanusha kushiriki.
Alipoulizwa 2018 na tena mwaka uliyopita kuhusu mauaji hayo, Raisi alikanusha kushiriki kwa vyovyote vile, hata licha ya kusifu amri ambayo alisema ilitolewa na mwasisi wa taifa hilo Ayatollah Ruhollah Khomeini, kuendelea na safishasifasha hiyo.