1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mhamiaji wa Syria ahusika na shambulio la Ansbach

25 Julai 2016

Mhamiaji wa Syria aliyekataliwa hifadhi ya ukimbizi Ujerumani mwaka mmoja uliopita amekufa baada ya kuripuwa bomu karibu na tamasha la muziki mkoani Bavaria ambalo limemuuwa yeye mwenyewe na kujeruhi watu wengine kadhaa.

Picha: picture-alliance/dpa/D. Karmann

Polisi imesema watu 12 wamejeruhiwa watatu kati yao wakiwa mahatuti katika shambulio hilo lililofanyika katika mji wa Ansbach mji wenye wakaazi 40,000 ulioko kusini magharibi mwa Nuremberg ambapo ndiko pia kuliko kambi ya jeshi la Marekani.

Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 27 inasemekana alikuwa akipatiwa matibabu ya akili baada ya kujaribu kujiuwa mara mbili na kwa mujibu wa polisi alikuwa amekusudia kushambulia tamasha hilo la muziki lakini alikataliwa kuingia ndani kwa sababu alikuwa hana tiketi na ndipo aliporipuwa bomu hilo nje ya mkahawa ulioko karibu.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari ulioitishwa kwa haraka Jumatatu (25.07.2016) waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la Bavaria Joachim Herrmann hakufuta uwezekano wa shambulio hilo kuwa na uhusiano na kundi la Dola la Kiislamu.

Hermmannn) amesema "Mripuko huo ulikuwa ni kifurushi kilichokuwa kimejazwa vipande vya vyuma ambao ungeliweza kujeruhi au kuuwa watu wengi zaidi mambo yanayosababisha kuwepo kwa tuhuma kwamba hili ni shambulio la Waislamu wa itikadi kali. Hata hivyo tunatakiwa kufanya uchunguzi wa kina kuyakinisha hilo. Tunataraji kutowa maelezo kwa wananchi hivi karibun."

Jaza ya kufadhiliwa

Herrmann amesema inatisha kwamba mtu aliyekuja katika nchi yao kutafuta hifadhi ametenda tendo hilo la kinyama na kujeruhi idadi kubwa ya watu baadhi yao wakiwa katika hali mahatuti.

Waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la Bavaria Joachim Herrmann.Picha: Reuters/M. Rehle

Tukio hilo litazidi kupalilia mashaka ya wananchi yanayozidi kuongezeka kuhusu sera ya Kansela Angela Merkel ya kuwacha milango wazi kwa wakimbizi ambapo kwayo zaidi ya wahamiaji milioni moja wameingia nchini Ujerumani katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita wengi wao wakikimbia vita nchini Syria, Iraq na Afghanistan.

Akizungumzia tukio hilo naibu mkuu wa polisi wa mji Ansbach Roman Fertinger ametilia mkazo kujumuishwa kwa vipande vya chuma katika bomu hilo.

Naibu mkuu huyo wa polisi amesema "Baadhi ya vipande vya chuma vilipatikana vimezagaa.Vipande vya aina hii kwa kawaida hutumika kwa shughuli za mbao.Itabidi tuchunguze kubaini iwapo vilitumika katika bomu hilo."

Mashambulizi yaliyoikumba Ujerumani hivi karibuni yanazusha masuala mazito kuhusu sera ya kuwapa hifadhi wakimbizi na usalama nchini kote hilo likiwa ni shambulio la nne la matumizi ya nguvu nchini katika kipindi kisichozidi wiki moja likiwemo lile la mauaji ya watu tisa yaliyofanwa na Mjerumani mwenye asili ya Iran Ijumaa iliopita.

Sera ya Merkel lawamani tena

Stephan Meyer mbunge kutoka chama cha kihafidhina cha Kansela Angela Merkel amesisitiza kwamba ni kosa kabisa kumlaumu Angela Merkel na sera yake ya wakimbizi kwa mfululizo wa matumizi ya nguvu katika kipindi cha moja lililopita.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.Picha: Reuters/S. Loos

Mayer ameliambia shirika la utangazaji la Uingereza BBC kwamba wahamiaji na wakimbizi milioni moja nukta moja walioingia nchini mwaka jana ni changamoto kwa wasimamizi ya sheria juu ya kwamba wimbi hilo la wakimbizi limepunguwa katika miezi ya hivi karibuni.

Mayer ambaye ni msemaji wa masuala ya ndani wa chama cha Christian Social Union cha jimbo la Bavaria ambacho ni chama ndugu cha chama Merkel cha CDU amesema hawawezi kusajili na kudhibiti wahamiaji wote wanaovuka mpaka na kuingia Ujerumani.

Mwandishi : Mohamed Dahman /Reuters/AFP

Mhariri:Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW