Miaka 10 baada ya Saddam Hussein
29 Desemba 2016Desemba 30, 2006, Saddam alionyongwa katika makao makuu ya idara ya upelelezi katika jeshi katika wilaya ya Kadhimiyah kaskazini mwa Baghdad. Maafisa ambao walishuhudia kuuwawa kwa Saddam Hussein aliyekuwa na umri wa miaka 69 mapema alfajiri, aliendelea kuwa mkaidi hadi mwisho wake, akipambana na maadui zake wa Iran na Marekani na kuwasifu wapiganaji ambao wameipeleka Iraq katika ukingo wa vita vya wenywe kwa wenyewe.
"Sikuona hata chembe ya hofu," mshauri wa zamani wa usalama wa taifa Mowaffak al-Rubaie, ambaye aliratibu hatua ya kunyongwa, aliliambia shirika la habari la AFP mwaka 2013.
"Sikusikia hali yoyote ya kujuta kutoka kwake, sikusikia ombi lolote la msamaha kutoka kwa Mungu .. ama ombi la kusamehewa," alisema.
Rubaie alisema alivuta ubao kumnyonga Saddam, lakini hakuna kilichotokea. Mtu ambaye hakutambuliwa kisha alivuta ubao huo kwa mara ya pili, na kumuua.
Muda mfupi kabla ya kuuwawa , Saddam alianza kusoma dua , lakini hakuweza kuimaliza.
Vidio ya dakika mbili na nusu iliyochukuliwa kwa njia ya simu ya mkono ilimuonesha akianguka kupitia katika mlango wa chini ya ardhi na kufariki huku kukiwa na shangwe kutoka kwa watu waliokuwapo.
Picha iliyoonesha kwa karibu ilionesha kichwa chake kikielemea upande mmoja katika kitanzi, na shingo yake ikiwa imekatika.
Mtu huyo aliyekuwa na madaraka makubwa aliuwawa baada ya kupatikana na hatia ya uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa mauaji ya mwaka 1982 ya watu 148 washia katika mji wa Dujail. Mauji hayo yanafuatia jaribio la kuuwawa dhidi yake katika eneo hilo.
Utawala wa kikandamizaji
Utawala wake uligubikwa na ukandamizaji wa kinyama , vita na vikwazo vilivyoumiza vya kimataifa.
Saddam alipinga uhalali wa mahakama maalum ya Iraq iliyoundwa kwa msaada wa marekani kumshitaki, na kuieleza kesi yake iliyofanyika kuanzia Oktoba 2005 hadi Julai 2006 kuwa ni "dhihaka".
Baadhi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia , ambao waliteseka katika utawala wake, walicheza mitaani baada ya kunyongwa. Lakini kuuwawa huko, ambapo Marekani ilisema haikushiriki , kulilaaniwa na Wairaq wa madhehebu ya Sunni na serikali kadhaa duniani -- licha ya sio na mahasimu wakubwa wa Saddam Hussein Israel na Iran.
Siku moja baada ya kunyongwa, Saddam alizikwa katika kijiji cha Awja, alikozaliwa karibu na Tikrit , kilometa 160 kaskazini mwa baghdad.
Ilikuwa pia karibu na Tikrit ambapo katika usiku ambao haukuwa na mbalamwezi Desemba 13, 2003, dikteta huyo wa zamani alikamatwa na majeshi ya Marekani. Washington ilitoa kiasi cha dola milioni 25 kama zawadi kwa mtu atakayetoa taarifa za kukamatwa kwake.
Baada ya kupinduliwa na majeshi ya uvamizi ya Marekani , Saddam Hussein alikimbia kwa muda wa miezi minane kwa msaada wa walinzi wake wa karibu kutoka katika familia yake, kwa mujibu wa viongozi wa kikabila wa eneo hilo.
Lakini mmoja alimsaliti, na kuwaelekeza wanajeshi wa Marekani kufika katika maficho yake baada ya yeye binafsi kukamatwa. Tofauti kabisa na maisha ya kifahari katika jumba la rais , Saddam alipatikana amejificha katika shamba katika kile ambacho wanajeshi wa Marekani walikiita "tundu la panya" , maficho ya chini ya ardhi ambapo kuna nafasi ndogo kwa ajili ya mtu mmoja kujilaza , akiwa na vifaa vya kujipatia hewa na feni ya kumpepea.
Mwandishi: Sekione Kitojo / Afpe
Mhariri: Grace Patricia Kabogo