1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 10 baada ya shambulizi la kemikali Ghouta nchini Syria

22 Agosti 2023

Muongo mmoja baada ya shambulizi baya la kemikali dhidi ya raia, hakuna yeyote ambaye amewajibishwa hadi sasa.

Kati ya watu 480 na 1500 walifariki dunia wengi wao wakiwa watoto kwenye shambulizi la kemikali Ghouta mwaka 2013.
Kati ya watu 480 na 1500 walifariki dunia wengi wao wakiwa watoto kwenye shambulizi la kemikali Ghouta mwaka 2013.Picha: AMMAR AL-ARBINI/SHAAM NEWS NETWORK/AFP

Miaka 10 baada ya shambulizi la kemikali dhidi ya mji wa Ghouta nchini Syria, raia nchini humo wanasema hawawezi kusahau picha za watoto wakifariki. Kulingana na chunguzi mbali mbali na vyanzo tofauti, kati ya watu 480 na 1500 walifariki dunia wengi wao wakiwa watoto waliokufa wakiwa usingizini ama kwa kukosa hewa kutokana na athari za shambulizi hilo. 

Alaa Makhzoumi ambaye sasa ana umri wa miaka 30, ameiambia DW kwamba kumbukumbu ya saa za alfajiri za Agosti 21 bado hazijaondoa uoga miaka kumi baadaye. Makhzoumi anasema wengi wao walikuwa bado wako macho kwasababu kulikuwa na joto sana kulala na kuwalazimu kubarizi katika eneo la juu la nyumba yao.

Ujerumani inaweza kumshtaki Assad kwa uhalifu wa kivita

Hata hivyo, mwendo wa saa nane na nusu usiku, shambulizi baya zaidi la kemikali nchini Syria lililenga eneo la Ghouta katika mji mkuu Damascus, ambao wakati huo lilikuwa ngome ya upinzani.

Makhzoumi anakumbuka kwamba waliposikia mlipuko huo, walidhani ni mashambulizi ya kawaida. Mumewe ambaye ni daktari, aliotoka nyumbani mara moja kuona iwapo kuna mtu anahitaji usaidizi.

Shambulio la gesi ya sumu Syria linahitaji jibu la haraka

Makhzhoumi ameiambia DW kwamba kelele ziliongezeka kutoka barabarani na kupumua kwao kukaanza kuwa kwa shida. Familia yake ikafunika nyuso zao kwa tishu zenye unyevu huku wakihofia kwamba huenda ni shambulizi la kemikali. Makhzhoumi anasema ijapokuwa hawakufahamu kinachoendelea, walisimama karibu na madirisha.

Picha iliyotangazwa na shirika la habari la upinzani Shaam, ikionyesha moshi uliodaiwa kuwa wa sumu ya gesi kali ukitanda juu ya majengo mashariki ma Ghouta. (Agosti, 21, 2013)Picha: Ammar al-Arbini/Shaam News Network/AFP

Syria yaialika OPCW kuchunguza shambulizi la sumu

Ripoti ya wakaguzi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa, ilithibitisha mwezi mmoja baada ya shambulizi hilo kwamba sampuli ya kimatibabu, ya kemikali na mazingira walizokusanya, zilionesha ushahidi wa kuridhisha kwamba roketi za masafa zilizokuwa na kiambati cha sumu ya sarin zilitumika.

Sumu ya Sarin

Sumu ya Sarin ni nzito kuliko hewa na huzama chini, hii ikiwa sababu kwanini watu wengi walikufa walipotafuta hifadhi katika vyumba vya chini.

Ripoti ya kina zaidi ya shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, HRW, ilihitimisha kuwa ushahidi kuhusu aina ya roketi zilizotumika katika mashambulizi hayo, unapendekeza pakubwa kwamba hii ni mifumo ya silaha inayojulikana na kuorodheshwa kuwa chini ya umiliki wa na mazumizi ya vikosi vya kijeshi vya serikali ya Syria.

Hata hivyo, rais wa Syria Bashar Assad, alikataa shtaka lolote kwa kuwa litakwenda kinyume na mantiki ya kimsingi kulingana na moja ya ripoti za kwanza kuhusu shambulio hilo iliyotolewa na shirika la habari la serikali ya Syria SANA. Badala yake, Assad aliushtumu upinzani.

Idadi ya watu waliouawa Ghouta Mashariki yafika 40

Kulingana na shirika hilo la SANA, waziri wa habari wakati huo Omran al-Zoubi pia alisema kuwa yote yaliosemwa ni ya kipuuzi, yaliopitwa na wakati ya uzushi na yaliokosa mantiki.

Licha ya madai ya uhalifu wa kivita ambayo yamemtenga kwa muda Assad kikanda na kimataifa, rais huyo wa Syria amekuwa akikubaliwa tena katika jamii ya kimataifa na ya kiarabu.Picha: Syrian Presidency/APAimages/IMAGO

Lina Khatib, mkurugenzi wa taasisi ya SOAS ya Mashariki ya Kati yenye makao yake mjini London, ameiambia DW kwamba Assad anategea akitumaini kwamba dunia hatimaye itasahau kuhusu uwajibikaji na kumrejesha katika jumuiya ya kimataifa kama kiongozi halali wa Syria. Khatib ameongeza kuwa ni muhimu kwamba ufuatiliaji wa uwajibikaji wa vitendo vya kikatili vya Assad unaendelea hata kama mkondo wa kisiasa wa mchakato wa amani utakwama.

Jamii ya kimataifa na Kiarabu yaanza kumkubali Rais Assad

Kelly Petillo, mtafiti kuhusu Mashariki ya Kati katika baraza la Ulaya kuhusu mahusiano ya nje, ameiambia DW kwamba inaonekana kuwa wakati umekuwa wa manufaa kwa Assad. Petillo ameongeza kuwa uwajibikaji sio diplomasia na kuongeza kuwa matumaini yake sasa yako katika mkondo wa kisiasa unaoongozwa kimataifa.

Assad atembelea Ghouta Mashariki

Katika taarifa kabla ya maadhimisho hayo ya miaka kumi mwaka huu, Laila Kiki, mkurugenzi mtendaji wa shirika lisilokuwa na kiserikali, The Syria Campaign lenye makao yake nchini Marekani, linalowaunga mkono wanaharakati nchini humo, anahofia kuwa kila wakati kuna athari kwamba watashuhudia kurudiwa kwa maasi makubwa nchini Syria na kwingineko.