1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UgaidiKimataifa

9/11: Al-Qaeda imedhoofika, lakini haijatoweka

11 Septemba 2026

Miaka 25 baada ya mashambulizi ya 9/11, Al-Qaeda si tena mtandao wa kigaidi wa kimataifa uliokuwa zamani. Uongozi wake umedhoofika, lakini matawi yake Afrika na Asia yanaendelea kuimarika kupitia migogoro ya ndani.

Afghanistan Helmand 1998 | Osama bin Laden akizungumza na waandishi wa habari milimani
Osama bin Laden aliitikisa dunia kupitia mashambulizi ya kigaidi, hasa ya Septemba 11, 2001; kuuawa kwake mwaka 2011 kuliidhoofisha al-Qaeda na kuisukuma kutawanyika zaidi kupitia matawi ya kikanda.Picha: AP

Abdullah al-Muhaysini hahitaji tena kuhofia vikwazo vya Marekani. Mwishoni mwa Agosti 2026, Wizara ya Fedha ya Marekani ilimwondoa mhubiri huyo wa zamani wa itikadi kali katika orodha ya SDN.

Orodha hiyo inajumuisha watu na mashirika ambao mali zao nchini Marekani huzuiwa na ambao raia na kampuni za Marekani kwa kawaida hawaruhusiwi kufanya nao biashara.

Wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, al-Muhaysini aliwahi kuwa mshauri wa masuala ya dini wa Al-Nusra Front, kundi lililotokana na Al-Qaeda. Pia alisaidia kuandikisha wapiganaji na kuunda mfumo wa utawala ulioongozwa na kundi hilo.

Kuondolewa kwake katika orodha kunahusishwa na sera mpya ya Marekani kuhusu Syria. Washington pia iliondoa Al-Nusra, ambayo baadaye ilijulikana kama Hayat Tahrir al-Sham, HTS, katika orodha ya mashirika ya kigaidi na kuifutia vikwazo vya SDN.

Wapiganaji wa al-Qaeda wakiwa wamebeba bunduki aina ya AK-47 katika video iliyotolewa kabla ya mashambulizi ya Septemba 11.Picha: AFP/Getty Images

Al-Qaeda imebadilikaje?

Miaka 25 baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001, hatua hiyo inaonyesha mabadiliko makubwa ya kisiasa na kiusalama. Al-Qaeda haijatoweka, lakini si tena shirika lilelile lililokuwa wakati wa mashambulizi ya 9/11.

Uongozi wake mkuu umedhoofika, huku matawi yake ya kikanda katika sehemu za Afrika na Asia yakiendelea kuwa na uwezo mkubwa wa kufanya mashambulizi. Uhusiano kati ya makao makuu na matawi hayo pia umekuwa legevu zaidi.

Mtaalamu wa masuala ya Uislamu Rüdiger Lohlker anasema ni muhimu kuacha kuitazama Al-Qaeda kwa mtazamo unaojikita zaidi Ulaya na Marekani. Makundi yenye itikadi kali yameendelea kuwa na ushawishi mkubwa nje ya maeneo hayo kuliko inavyoonekana kutoka nchi za Magharibi.

Hali hiyo inaonekana wazi zaidi barani Afrika. Katika eneo la Sahel, muungano wa Jama'at Nusrat al-Islam wal-Muslimin, JNIM, umeibuka kuwa moja ya makundi yenye nguvu zaidi yanayohusishwa na Al-Qaeda.

Nchini Somalia, Al-Shabaab bado ina nguvu, huku Al-Qaeda katika Rasi ya Arabia, AQAP, ikiendelea kufanya shughuli zake nchini Yemen. Afghanistan nayo bado inatajwa kuwa eneo la kujificha na kujipanga upya kwa wanachama wa mtandao huo.

Kwanini Al-Shabab inawatia hofu wasomali?

01:30

This browser does not support the video element.

Vita dhidi ya ugaidi viliidhoofisha

Al-Qaeda inazidi kupunguza matumizi ya jina lake katika maeneo mbalimbali. Lars Berger, mtaalamu wa masuala ya usalama na ugaidi, anasema hali hiyo ni matokeo ya juhudi za kupambana na ugaidi zilizoanzishwa baada ya mwaka 2001.

Operesheni za kijeshi nchini Afghanistan, pamoja na ushirikiano wa mashirika ya ujasusi na polisi, ziliudhoofisha sana mtandao huo. Berger anaona mashambulizi ya Septemba 11 kuwa kushindwa kwa mkakati wa Al-Qaeda.

Kundi hilo lilitarajia mashambulizi yangechochea kuenea kwa itikadi kali katika ulimwengu wa Kiarabu na kusaidia kuangusha serikali za eneo hilo. Malengo hayo hayakufikiwa.

Badala yake, Al-Qaeda ilipoteza viongozi wengi, maeneo ya kujificha na uwezo wa kupanga mashambulizi makubwa kutoka makao makuu.

Baada ya hapo, ilibadili mfumo wake wa shughuli. Matawi yake yalianza kutafuta maeneo ambako yangeweza kujenga ushawishi wa kudumu, hasa katika sehemu za Afrika na Yemen.

Mataifa yenye serikali dhaifu, vikosi vya usalama visivyo na uwezo wa kutosha na migogoro ya ndani isiyotatuliwa yaliweka mazingira mazuri kwa makundi hayo kuenea.

Rais Barack Obama na timu yake ya usalama wakifuatilia operesheni ya dhidi ya Osama bin Laden katika Ikulu ya White House House, Mei 2011.Picha: Pete Souza/White House/AP/picture alliance

Sahel yageuka kitovu muhimu

Katika eneo la Sahel, makundi yenye itikadi kali yamepanua maeneo yao ya kujificha na kufanya mashambulizi. JNIM na tawi la kundi la Dola la Kiislamu katika Sahel, ISSP, yanashindania ardhi, wapiganaji na rasilimali.

Uchambuzi wa Critical Threats Project unaonyesha jinsi ushindani huo unavyoendelea nchini Niger. Mwezi Juni 2026, JNIM ilishambulia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Niamey.

Lohlker anasema mafanikio ya makundi hayo hayawezi kuelezwa kwa itikadi peke yake. Yanaunganishwa pia na uchumi unaotegemea ghasia.

Utekaji nyara, biashara haramu na uporaji huyaingizia fedha makundi yenye silaha. Katika maeneo ambayo matumizi ya nguvu yanaweza kuleta faida, makundi hayo yana uwezo wa kuandikisha wanachama, kuunda mitandao na kuwafanya baadhi ya watu wategemee shughuli zao.

Udhaifu wa serikali nao una mchango mkubwa. Ambako mamlaka za dola hazipo au zina uwezo mdogo, makundi kama Al-Qaeda yanaweza kutumia migogoro ya jamii na ombwe la uongozi kujijenga.

Kanda ya Sahel sasa inaelezwa kuwa kitovu cha ugaidi dunianiPicha: AFP

Mkakati mpya wa kuanzia chini

Mkakati wa Al-Qaeda pia umebadilika. Zamani, lengo lake kuu lilikuwa kumshambulia kile ilichokiita "adui wa mbali”, hasa Marekani na washirika wake.

Sasa matawi yake yanajikita zaidi katika kujenga ushawishi katika maeneo yanakofanya shughuli. Badala ya kusubiri maagizo kutoka uongozi mkuu kwa ajili ya mashambulizi makubwa, yanatumia operesheni ndogo zinazopangwa ndani ya maeneo husika.

Katika Sahel, mkakati huo unahusisha kujenga ushirikiano na makundi ya wenyeji, kutumia migogoro ya kikabila na kijamii, kuingia katika jamii na hatimaye kudhibiti maeneo.

JNIM imejikita katika migogoro ya kikabila na kijamii ya Sahel, huku Al-Shabaab ikitumia migawanyiko katika mfumo wa koo nchini Somalia. Lengo la kimataifa la itikadi ya kijihadi linabaki, lakini mapambano halisi yanaendeshwa katika mazingira ya eneo husika.

Mabadiliko hayo, yanayoelezwa kama kujikita katika masuala ya ndani, yameisaidia Al-Qaeda kuendelea kuwapo licha ya kupoteza ushawishi wake wa kimataifa.

Mtandao wa al-Qaeda umeendelea kujiimarisha katika eneo la Sahel kwa kutumia udhaifu wa serikali, migogoro ya kisiasa na hali mbaya ya usalama.Picha: AFP

Ushindani na Dola la Kiislamu

Al-Qaeda pia inakabiliwa na ushindani kutoka kundi la Dola la Kiislamu, IS. Mtaalamu wa ugaidi Behnam Heidenreuter-Said anasema vijana wengi wanaovutiwa na itikadi kali wameelekea zaidi katika IS.

Kundi la IS limewahi kufanya mashambulizi makubwa na kutumia kwa ufanisi zaidi propaganda katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Tofauti na Al-Qaeda, IS ilijaribu kupata mafanikio ya haraka, kujitangaza na kupanua maeneo yake kwa kasi. Ilifanikiwa kuteka maeneo makubwa nchini Iraq na Syria, lakini upanuzi huo ulifuatiwa na kuvunjika kwa dola yake ya kujitangazia.

Al-Qaeda, kwa upande mwingine, imechagua mkakati wa muda mrefu zaidi. Imepoteza umaarufu wake kama chapa ya kimataifa, lakini imeendelea kuwapo kupitia matawi yanayojikita katika migogoro ya ndani.

Hata hivyo, haijulikani ikiwa mtandao huo utaweza kulibadilisha kizazi chake cha viongozi wanaozeeka. Katika sehemu za Ulaya, itikadi ya kijihadi yenye kutumia silaha imepoteza mvuto, na Al-Qaeda haina tena uwezo uleule wa kuwaandikisha vijana wengi.

Rais Donald Trump na maafisa wake wakifuatilia operesheni ya Marekani dhidi ya kiongozi wa ISIS, Abu Bakr al-Baghdadi, nchini Syria mwaka 2019.Picha: Shealah Craighead/The White House/Getty Images

Taarifa kuhusu Al-Qaeda ni chache

Ni vigumu kutathmini kwa usahihi kiwango cha hatari inayotolewa na Al-Qaeda leo. Heidenreuter-Said anasema kuna taarifa chache sana kuhusu shughuli za sasa za uongozi mkuu wa kundi hilo.

Tangu mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel ya Oktoba 7, 2023, Al-Qaeda haijaonekana sana katika migogoro mikubwa ya Mashariki ya Kati. Hamas, Hezbollah, Wahouthi na Iran ndizo zimetawala uwanja wa kisiasa na kijeshi.

Lakini kutokuonekana kwa Al-Qaeda hakumaanishi kuwa matawi yake hayana nguvu. JNIM, Al-Shabaab na AQAP bado yana uwezo wa kufanya mashambulizi na kujenga ushawishi katika mataifa yenye serikali dhaifu.

Miaka 25 baada ya 9/11, Al-Qaeda imepoteza kwa kiasi kikubwa jukwaa lake la kimataifa, lakini imejifunza kuishi kupitia migogoro ya ndani.

Hatari ni kwamba matawi yake yanaweza kujikita kwa muda mrefu katika mataifa dhaifu, hadi kutoka kuwa makundi ya kigaidi na kugeuka kuwa nguvu za kudumu za kijeshi na kisiasa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW