1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 25 ya Shirika la GIZ Afrika Mashariki

Veronica Natalis
19 Desemba 2024

Shirika la misaada la Ujerumani GIZ limeadhimisha miaka 25 ya ushirikiano na Jumuiya ya Afrika Mashariki, likisema limefanikiwa kuelimisha wafanyakazi wa umma takriban laki tano na raia zaidi ya milioni mbili.

Kaffeebohnen in Kenia
Picha: Ute Grabowsky/photothek/picture alliance

Msimamizi wa miradi ya GIZ Afrika Mashariki, Bjorn Richt, amesema miradi yao imejikita katika teknolojia, mabadiliko ya tabianchi, biashara, afya, na mbinu za kukabiliana na magonjwa ya miripuko.

Shirika la GIZ, ambalo lilianza shughuli zake rasmi nchini Tanzania mwaka 1982, linaeleza kujivunia ushirikiano wa miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya mpya ya Afrika Mashariki. Kupitia miradi yake mbalimbali, shirika hilo limefanikiwa kusaidia wanachama wa Jumuiya hiyo katika nyanja tofauti. Mbali na miradi inayohusu mabadiliko ya tabianchi na afya, GIZ pia limewekeza zaidi katika kuwasaidia vijana kupitia ubunifu, uvumbuzi, na teknolojia kwa ujumla katika nchi zote za Afrika Mashariki. 

Happyness Alexander, mhitimu wa shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mandela kilichopo Arusha, Kaskazini mwa Tanzania, ni mmoja wa wanufaika wa miradi hiyo. Akiwa na utaalamu katika mifumo ya simu na teknolojia mwambata, Happyness alipata ufadhili kupitia mradi wa kituo cha umahiri cha tehama, unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Ujerumani GIZ. Miradi hii inalenga kuinua uwezo wa vijana wa Afrika Mashariki na kuimarisha maendeleo ya teknolojia katika kanda hiyo.

Wanafunzi wa Ujerumani na wenzao wa Tanzania kutoka Shule ya Sekondari ya Tembo Forest mkoani ManyaraPicha: Veronica Natalis/DW

Msimamizi wa miradi ya  GIZ Afrika Mashariki Bjorn Richt, anaeleza kuwa Jumuiya hiyo imeweza kupiga hatua kubwa katika kipindi cha miaka 25 na mchango wa Ujerumani na Umoja wa ulaya kwa ujumla ni mkubwa. GIZ inasaidia utekelezaji wa itifaki za Jumuiya ya Afrika Mashariki hasa katika biashara, soko la pamoja na ushirikiano wa forodha. "Tunafanya kazi kwa pamoja katika ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda, kwenye soko la pamoja, ambapo kwa sasa ukuaji wa biashara za ndani ya kanda umefikai asilimia 12 ikiwa ni ongezeko kutoka chini ya asilimia 10 ya wali. Ukilinganisha na maeneo mengine ya Afrika, kanda hii ya Jumuiya ya Afrika mashariki, inaongoza kwa kuwa na makubaliano ya biashara huru.”

Dr. Kisangiri Michael mhadhiri mkuu wa chuo kikuu cha sayansi na teknolojia cha Mandela, na msimamzi wa mradi wa teknolojia chuoni hapo unaofadhiliwa na GIZ, anakiri kwamba mradi huo umewavumbua vijana wengi katika masuala ya teknolojia na kuwasaidia kutimiza ndoto zao.

Hayo ni miongoni mwa mafanikio mengi ambayo GIZ inajivunia katika ushirikiano wake na Jumuiya ya Afrika Mashariki, tangu ilipoanzishwa upya miaka 25 iliyopita. Ushirikiano huu unafanywa kupitia uratibu wa serikali za Afrika Mashariki, taasisi za kikanda, sekta binafsi na asasi za kiaraia. 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW