Miaka 30 baada ya azimio la haki za mtoto
20 Novemba 2019Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyochapishwa Jumatatu hii imeelezea utafiti uliofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF unaotoa mwito kwa mataifa kuangazia upya wajibu wao chini ya azimio hilo lililoadhinishwa miaka 30 iliyopita.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alipotoa ujumbe wake kwenye maadhimisho haya amesema azimio hilo lilikuwa na hatua ya kwanza iliyoyakutanisha mataifa pamoja na kuwa na msimamo mmoja kuhusu wajibu wao katika kufanikisha upatikanaji wa haki kwa kila watoto.
Amesema, tangu wakati huo kumefikiwa hatua kadhaa, lakini akisisitiza kuunganishwa nguvu zaidi na kuhakikisha kila mmoja anawajibika ipasavyo katika utekelezwaji wa makubaliano hayo, kwa kuwa bado watoto wanakabiliwa na vitisho.
"Vifo vya watoto vimepungua kwa zaidi ya nusu. Lakini bado mamilioni ya watoto wanateseka na vita, umaskini, ubaguzi na magonjwa. Ulimwenguni kote, watoto wanatuonyesha nguvu na uongozi wakitetea ulimwengu endelevu kwa wote. Tunapokumbuka miaka 30 ya azimio hili muhimu, nawasihi nchi zote kutimiza ahadi zao kwao." amesema Guterres.
UNICEF yaelezea wasiwasi juu ya vitisho vinavyomkabili mtoto.
Mkurugenzi mkuu wa UNICEF Henrietta Fore amenukuliwa akisema ingawa kuna ongezeko la idadi ya watoto wanaoishi maisha bora na wakiwa na afya njema lakini kundi jingine linaloishi katika hali ya umasikini bado linakabiliwa na kitisho kikubwa.
Amesema, katika miongo mitatu baada ya azimio hilo, kumeonekana mafanikio makubwa katika kupunguza idadi ya watoto wanaoshindwa kujiunga na masomo ya shule za msingi kwa karibu asilimia 40 huku idadi ya watoto wa chini ya miaka mitano wanaodumaa ikipungua kwa zaidi ya milioni 100.
Amesema, hata ugonjwa wa polio uliowasababishia watoto karibu 1,000 kupooza kila siku katika miongo mitatu iliyopita hii leo asilimia 99 ya visa hivyo imeondolewa. Hata hivyo bado ameonya kuhusu mabadiliko ya tabianchi ambayo yanatishia mafanikio hayo changamoto za lishe, elimu, afya kwa ujumla na hata unyanyasaji kupitia mitandao ya kijamii.
Aidha, amesema umasikini, kukosekana kwa usawa ubaguzi na umbali pia vimeendelea kuwanyima mamilioni ya watoto haki zao kila mwaka huku watoto 15,000 walio chini ya miaka mitano wakiwa wanafariki dunia kila siku na wengi miongoni mwao kutokana na magonjwa yanayotibika na vyanzo vinavyoweza kuzuilika kama uzito uliopitiliza kwa watoto na wasichana wanaopata tatizo la upungufu wa damu.
Siku ya mtoto duniani ilianzishwa mwaka 1954 kufuatia Azimio la Ulimwengu la siku ya mtoto na hudhimishwa kila Novemba 20 ya mwaka kuhamasisha ustawi wa watoto duniani.
(UN/UNICEF)