1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 30 tangu ukuta wa Berlin kuporomoka

Oumilkheir Hamidou
2 Januari 2019

Nusu muhula wa Rais wa Marekani Donald Trump, suala kama ahadi za kiongozi wa Korea ya Kaskazini Kim Jong Un zinaweza kuaminika au la na miaka 30 tangu ukuta wa Berlin ulioporomoka magazeti

Deutschland Besucher in der Mauergedenkstätte in Berlin
Picha: picture-alliance/dpa/J. Büttner

 

Tunaanzia Marekani ambako nusu mhula haujawadia tayari homa ya uchaguzi mwengine wa rais imeshaanza kupanda. Gazeti la Münchner Merkur linaandika :"Januari 20 inayokuja Rais Donald Trump atasherehekea nusu mhula tangu alipokabidhiwa hatamu za uongozi. Hata hivyo kinyang'anyiro cha kuania kiti cha urais kimeshaanza miaka miwili kabla ya tarehe halisi ya uchaguzi kuwadia. Seneta wa jimbo la Massachusetts, Elizabeth Warren amekuwa mdemokrat wa kwanza kutangaza azma ya kushindana na Donald Trump uchaguzi utakapoitishwa mwaka 2020. Huo ni mwanzo wa kinyang'anyiro tete na ambacho matokeo yake hakuna anaeweza kuyakadiria.

Wakati huu tulio nao hakuna anaeweza kukadiria matokeo yake kwasababu wademokrats wamo katika kutafakari mwongozo wa aina gani waufuate. Na zaidi ya hayo mpaka wakati huu bado hawana mshika bendera mwenye kuwekewa matumaini. Yote hayo ndio chanzo cha nafasi nzuri anayowekewa rais Trump. Hakuna lakini kilicho na uhakika. Mustakbali wa kisiasa hauaminiki. Na binafsi Trump hakuna  mdadisi yeyote aliyeweza kuashiria kama angekuwa rais miaka miwili kabla ya uchaguzi."

Amani katika raasi ya Korea yahitaji subira

 Mwaka uliomalizika wa 2018 umeshuhudia tukio la aina yake: Mkutano wa kilele kati ya rais wa Marekani Donald Trump na kiongozi wa Korea ya kaskazini Kim Jong Un. Gazeti la "Märkische Oderzeitung linajiuliza eti ahadi zilizotolewa na Kim Jong Un ni za kuaminika? "Imani ya Kim Jong Un kwa Marekani si kubwa hivyo kuweza  kuachia msaada wa kiuchumi umfutie hadhi yake, bima ya maisha yake  kama kiongozi wa dola la kinuklea. China na Korea ya Kusini wameshatambua: amani ya kudumu katika raasi ya Korea itapatikana tu kufuatia utaratibu wa muda mrefu wa kujongeleana. Kwa kiongozi kama Trump  mwenye kupenda kujionyesha utaratibu kama huo ni wa usumbufu. Lakini bila ya usumbufu ufumbuzi hautoweza kupatikana."

Wajerumani washukuria yaliyotokea miaka 30 iliyopita

Ripoti yetu ya mwisho magazetini inatufikisha Berlin ambako ukuta wa chuma uliporomoka msimu wa mapukutiko mwaka 1989 na kusababisha kumalizika pia enzi za vita baridi. Gazeti la Hannoversche Allgemeine Zeitung, linaandika: "Eti kweli mwaka 2019 Wajerumani tutajipiga vifua kwa fakhari: Miaka 30 tangu ukuta wa Berlin ulipoporomoka: Sherehe kubwa kubwa zinapangwa kuandaliwa. Lakini badala ya fakhari tunabidi tushukurie. Sera ya kimataifa ya kusaka maridhiano iliyokuwepo wakati ule, haipo tena katika zama hizi za leo za Vladimir Putin na Donald Trump wanaopigania uzalendo."

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW