1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 5 bila Magufuli: Urithi wa maamuzi magumu na maendeleo

17 Machi 2026

Ni miaka mitano kamili tangu kifo cha Rais wa awamu ya tano Tanzania, John Magufuli. Viongozi na wananchi wanamkumbuka kwa mchango wake katika miundombinu, uwajibikaji na uzalendo, huku urithi wake ukiendelea kujadiliwa.

Rais wa zamani wa Tanzania hayati John Magufuli
Rais Magufuli alifariki Machi 17, 2021, akiacha urithi mchanganyiko na kumbukumbu za muda mrefu.Picha: AFP

Machi 17 imetimia miaka mitano tangu kufariki kwa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli, tukio lililoacha pengo kubwa katika siasa za Tanzania na bara la Afrika. Katika kipindi hiki, kumbukizi za maisha na uongozi wake zimeendelea kuibua hisia mchanganyiko za majonzi, fahari na tafakari juu ya mwelekeo wa taifa.

Magufuli, aliyefariki mwaka 2021 akiwa madarakani, alijipatia umaarufu kwa mtindo wake wa uongozi ulioelezwa kuwa wa vitendo, nidhamu na uthubutu. Kauli yake maarufu, "Najua mtanikumbuka… lakini mtanikumbuka kwa mazuri,” imeendelea kunukuliwa na wengi wanaoenzi mchango wake katika maendeleo ya nchi.

Maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka mitano yamefanyika nyumbani kwake Chato mkoani Geita, ambako viongozi wa serikali, wanasiasa, viongozi wa dini na wananchi wameungana katika misa maalum ya kumuenzi. Ibada hiyo iliongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara, Mhashamu Severine Niwemugizi, aliyesisitiza umuhimu wa uzalendo na utumishi kwa taifa.

Kifo cha Magufuli kiliitikisa kanda nzima ya Afrika Mashariki, Maziwa Makuu na bara zima la Afrika.Picha: Khalil Senosi/AP/picture alliance

Makamu wa Rais Dk Emmanuel Nchimbi, pamoja na viongozi wengine waandamizi wa sasa na wa zamani, walihudhuria hafla hiyo. Pia viongozi wa vyama vya upinzani na wanadiplomasia walishiriki, ishara ya jinsi urithi wa Magufuli unavyogusa makundi mbalimbali ya kisiasa na kijamii.

Urithi wa miundombinu na uwajibikaji

Katika kipindi chake cha uongozi kuanzia mwaka 2015, Magufuli alijikita katika miradi mikubwa ya miundombinu, ikiwamo ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, upanuzi wa viwanja vya ndege, miradi ya umeme kama Bwawa la Julius Nyerere na uboreshaji wa barabara. Alijulikana pia kwa kampeni kali dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya fedha za umma, jambo lililompatia jina la "Mtumbua Majipu.”

Wachambuzi wa siasa wanasema sera zake zilijenga taswira ya kiongozi aliyekuwa tayari kuchukua maamuzi magumu kwa lengo la kuharakisha maendeleo. Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Profesa Wetengere Kitojo, anaeleza kuwa hatua alizochukua zimeacha alama kubwa katika historia ya taifa.

John Pombe Magufuli azikwa

01:05

This browser does not support the video element.

Hata hivyo, pamoja na sifa, uongozi wa Magufuli uliwahi kukosolewa kwa baadhi ya maamuzi yaliyodaiwa kubana uhuru wa kisiasa na vyombo vya habari. Miaka mitano baada ya kifo chake, mjadala kuhusu mizani kati ya nidhamu ya maendeleo na uhuru wa kiraia bado unaendelea.

Kwa wengi, urithi wa Magufuli unabaki kuwa somo la uongozi wenye msukumo wa matokeo, uzalendo na uwajibikaji. Kama alivyosema mchambuzi wa siasa Dk Richard Mbunda, maono yake ya miundombinu na maendeleo yanaendelea kuwa sehemu ya urithi wa taifa.

Hayati John Pombe Magufuli alizikwa Machi 26, 2021 nyumbani kwake Chato. Leo, miaka mitano baadaye, jina lake linaendelea kutajwa katika mijadala ya kitaifa kuhusu maendeleo, siasa na mustakabali wa Tanzania.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW