Miaka 50 tangu ukandamizaji wa vuguvugu la mageuzi Prague
21 Agosti 2018Miaka 50 iliyopita vifaru vya iliyokuwa Umoja wa Kisovieti viliingia mjini Prague kuzima mageuzi ya kidemokrasia ya serikali ya kikomunist ya Czechoslovakia, na kuzusha umwagaji damu katika hatua ya kuikalia nchi hiyo ambapo somo lililopatikana Waczech wengi wanalihofia limesahaulika.
Kumbukumbu hiyo ikifanyika kwa sherehe, maonesho na filamu juu ya vuguvugu la mapinduzi ya Prague pamoja na ukandamizaji wake wa kikatili ambao ulianza Agosti 21, 1968, inakuja katika wakati kuna ushawishi unaorejea tena katika chama ambacho kwa muda mrefu kiliwekwa kando cha kikomunist cha Czech katika siasa za taifa hilo.
Babis, ambaye aliwahi kuwa mwanachama wa chama cha Kikomunist cha Czechoslovakia, alikuwa akizungumza katika kumbukumbu hiyo wakati maneno yake yalimezwa na kelele za kumzomea na kulele za "aibu" kutoka kwa kundi la watu waliokuwa wakisikiliza hotuba hiyo. Babis alisema.
"Watu hawakutaka tena udikteta wa aina ya Kisovieti. Walitaka tu kuishi maisha ya kawaida, ya jamii huru. Uvamizi wa majeshi ya mkataba wa warsaw yalizuwia hatua za mageuzi na ubinafsishaji."
Babis ambaye ni muasisi wa chama cha ANO , amekuwa waziri mkuu mwaka jana. Amekabiliana na ukosoaji mkubwa unaohusiana na chama chake cha zamani cha kikomunist. Akizungumza katika kumbukumbu hiyo katika jengo la redio ya Czech, eneo ambalo machafuko makubwa yalitokea wakati wa uvamizi wa mwaka 1968, Babis alitoa heshima zake kwa wale waliofariki.
Ukandamizaji wa nguvu
Miezi michache ya kuchukua madaraka kama kiongozi wa chama cha kikomonisti cha iliokuwa Czechoslovakia mwanzoni mwa mwaka 1968, Alexander Dubcek alifuta ukaguzi wa kisiasa, na kujaribu kuleta mageuzi ya kiuchumi. Vikosi vya kisovieti yaani Urusi ya zamani, Poland, Hungary na Bulgaria viliingia katika mji mkuu wa Czechoslovakia -Prague wakati wa usiku wa Agosti 20-21 mwaka huo na kufanya ukandamizaji wa kikatili katika kile walichokiona ni kitisho kikubwa kwa ushawishi wa kisiasa wa Urusi. Wanahistoria wanasema raia 137 waliuawa katika ukandamizaji huo kati ya Agosti na Desemba mwaka 1968.
Wakati huo huo kukumbuka tukio hilo la miaka 50 iliopita, Mamia ya waandamanji walikusanyika nje ya ubalozi wa Urusi mjini Prague jana jioni ili kupinga hatua ya Urusi wanaoiona kuwa ya ukandamizaji mwengine baada ya kulitwaa eneo la Crimea kutoka nchi jirani ya Ukraine mwaka 2014.
Wanasiasa maarufu wa Umoja wa Ulaya wamesema kumbukumbu hiyo pia inaeleza haja ya kulinda uhuru na demokrasi leo katika bara ambalo linakabiliwa na wimbi jipya la tawala za ukandamizaji katika Ulaya mashariki, pamoja na Urusi ambayo inajaribu kuweka ushawishi wake katika maeneo yake ya zamani.
"Agosti 21 , 1968 ilikuwa sawa na konde lililovurumushwa usoni," alisema Vladimir Hanzel, akikumbuka ghasia mpya zilizotokea wakati huo ambapo wanajeshi 200,000 wa kile kilichofahamika kama mkataba wa Warsaw , wengi wao kutoka iliyokuwa Umoja wa Kisovieti lakini pia Poland, Hungary na Bulgaria, waliingia katika nchi hiyo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman