1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 50 ya habari na teknolojia ya mawasiliano Kenya

11 Desemba 2013

Kenya inaadhimisha miaka 50 ya uhuru ikizingatiwa kuwa na maendeleo makubwa katika sekta ya habari na teknolojia za mawasiliano, licha ya hatua za hivi karibuni za serikali kuonekana kutishia maendeleo hayo.

Teknolojia ya simu za mikononi imeimarika sana nchini Kenya.
Teknolojia ya simu za mikononi imeimarika sana nchini Kenya.Picha: Getty Images

Tokea mwaka 2010, Kenya inaongozwa katika msingi wa katiba mpya ya kidemokrasia, huku licha ya ufisadi, ustawi wa uchumi ni wa juu, unaovuuka asilimia 5.

Zaidi ya asilimia 60 ya Wakenya ni watu wenye umri wa chini ya miaka 24. Tulikutana na baadhi yao katika mkahawa mmoja wa intaneti jijini Nairobi wakiyatafakari maendeleo ya nchi yao miaka 50 baada ya uhuru. Walionekana kuwa na mchanganyiko wa wasiwasi, matumaini na fahari juu ya yaliyofikiwa nchini mwao.

"Idadi kubwa ya watu bado wanaishi katika umasikini. Watu hawana mahala pakuishi na wala hakuna nafasi za ajira za kutosha kwa ajili ya vijana. Natamani kuwa na viongozi wazuri wasiokuwa mafisadi," alisema mmoja wao aliyetwambia anaitwa Sibyle Munika.

Kijana mwengine, Joane Ochieng Onyango, alisema anasomea taaluma ya vyombo vya habari, ambapo anaiona Kenya "inasonga mbele katika tekinolojia lakini bado pana changamoto kubwa, kwa sababu bado haijaendelea vizuri."

Kukuwa kwa teknolojia

Teknolojia ya simu za mikononi imeimarika sana nchini Kenya.Picha: Getty Images

Kulikuwa pia na Samuel aliyejitambulisha kuwa anashughulika na mambo ya utengenezaji wa programu za komyputa. Kwake, hali ya vijana wa leo ni nzuri kuliko ya wale wa miaka 50 iliyopita kwa sababu wa sasa "wananufaika na teknolojia ya kisasa na zana za kileo za kupatia habari."

Ni kweli kwamba sekta ya tekinolojia ya mawasiliano na habari inastawi nchini Kenya. Wakenya ni wabunifu. Wanatayarisha programu za kompyuta kukidhi mahitaji ya wakulima, kwa ajili ya kutoa habari juu ya mambo ya afya au za kuwezesha kufanya miamala ya fedha kwa njia ya simu, maarufu kama M-Pesa.

Kiasi ya khumusi moja ya pato jumla la ndani inahawilishwa kwa njia ya simu za mikononi. Karibuni tu Kenya itakuwa kituo kikuu cha tekinolojia, Silicon Savannah ya Afrika, mithili ya Silicon Valley ya Carlifonia.

Wakati wa machafuko ya baada ya uchaguzi mwaka 2008, watengezaji wa programu za kompyuta katika taasisi ya Ushahidi waliazindua jukwaa la mawasiliano ili kutoa habari juu ya matukio ya umwagikaji damu katika sehemu za mizozo .

Habari hizo ziliwasilishwa kwa watu kupitia ujumbe wa simu za mkononi. Wakati huo watu walihisi kwamba hawakupata habari za kutosha kutoka kwenye vyombo vya habari vya kawaida.

Kwa hivyo, ni sahihi kusema kwamba Kenya ina mawanda mapana katika mandhari ya vyombo vya habari.

Uhuru wa habari kitanzini

Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto, akielekea mjini The Hague, kukabiliana na mashitaka ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu.Picha: Reuters

Hata hivyo, wakati taifa hilo likiadhimisha miaka 50 ya uhuru wake, uhuru wa habari unaingia kwenye mtihani mzito. Tayari bunge limepitisha mswaada wa sheria unayoipa mamlaka makubwa serikali katika kuvidhibiti vyombo vya habari.

Victor Bwire, ambaye ni makamu mwenyekiti wa Baraza la Vyombo vya Habari nchini Kenya, amekasirishwa na mswada huo kwa sababu uhuru wa vyombo vya habari ni jambo lililowekwa katika katiba ya Kenya.

"Tunasema kwamba mswadaa huo una vipengele vinavyokiuka katiba. Vipengele hivyo vinaigeuza kazi yetu kuwa ya kihalifu, vinawatisha waandishi na kuwazuia kufanya uchunguzi na kufanya kazi ya uandishi nchini," anasema Bwire.

Lakini Rais Kenyatta bado hajautia saini mswada huo alioukataa kwa mara ya kwanza ulipoüpitishwa na Bunge mwezi Oktoba na akaurudisha tena ukiwa na masahihisho kadhaa yaliyofanywa na ofisi yake, ambayo nayo yanakosolewa na wanahabari kuwa hayakubadilisha mantiki yake ya kuminya uhuru wa kujieleza.

Kwa sasa ametingwa na kesi inayomkabili kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya The Hague. Kwa kuvitumia vidokezo dhidi ya ubeberu, Kenyattta anawahamasisha watu barani Afrika kusimama dhidi ya Mahakama hiyo na anajaribu kufanya juhudi ili kesi yake iakhirishwe au ikiwezekana aweze kuikwepa kabisa.

Rais Kenyatta pamoja na Makamu wake, William Ruto, wanakabiliwa na mashtaka ya kutenda uhalifu dhidi ya ubinadamu kuhisiana na matukio ya umwagikaji damu yaliyofuatia uchaguzi wa mwaka wa 2007 nchini Kenya.

Mwandishi: Andrea Schmidt
Tafsiri: Abdu Mtullya
Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi