Miaka 50 ya uhuru wa Ghana
6 Machi 2007Chini ya uongozi wa hayati Kwame Nkurumah Ghana ilikuwa huru mwezi Marchi,6 mwaka 1957 na hivyo kuwa taifa la kwanza barani Afrika kujitoa katika minyororo ya wakoloni.
Akitangaza kwa mara ya kwanza kwamba Ghana iko huru,Kwameh Nkurumah alisema..
“Hatimaye mapambano yamekwisha, na kwa hivyo Ghan nchi yenu mnayoipenda iko huru daima.’’
Ghana ikiwa chini ya Kwameh Nkurumah ilipata uhuru wake mwaka 1957 na kuwa taifa la kwanza katika eneo la Afrika kusini mwa jangwa la sahara kuwatikisa wakoloni wake Uingereza.
Tukio hilo liliibua jazba za harakati za ukombozi katika bara zima la Afrika ambalo wakati huo nchi nyingi zilikuwa bado ziko chini ya wakoloni.
Katika kipindi cha muongo mmoja mfano huo wa Nkurumah uliibadili Afrika na kuweka msingi wa mataifa mengine huru barani humo na viongozi ambao walitikia mwito wa kuwa na Afrika huru yenye mshikamano,udugu,na usawa.
Waliovutiwa na kiongozi huyo walimtaja kama nyota ya Afrika wakati wengine wengi wakisema alikuwa mfano wa kuigwa na viongozi katika bara hilo la Afrika.Hassan Nassor Moyo mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania aliwahi kukutana na Nkurumah katika miaka ya 60 anasema alikuwa kiongozi aliyejitolea kuiona Afrika imejikomboa…
Lakini nyota ya Nkurumah ilianza kufifia katika muongo huohuo kwani siasa yake ya ukandamizaji ilitawala na kuutumbukiza uchumi wa Ghana katika hali mbaya.
Mwaka 1966 aliangushwa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi wakati alipokuwa ziarani nje ya taifa lake.
Hatua hiyo iliwafanya waghana washerehekee majiani mjini Accra ,wakipasua picha za kiongozi huyo kuanzia maofisini hadi mabango ya barabarani.
Nkurumah alikimbilia uhamishoni nchini Guinea na baadae kufariki huko Bucharest mwaka 1972.
Kinyume lakini na matumaini ya Umoja wa Afrika ambao ulichipuka kwa kuharibu tawala za wakoloni, sasa mapinduzi ya umwagaji damu yalianza kushuhudiwa huko Togo mnamo mwaka 1963 na kuenea kama moto wa kichakani katika eneo zima,na kuangushwa kwa tawala zilizodhoofishwa na ubinafsi na rushwa.
Miongo kadhaa imepita na wengi wanasema kwamba bara hilo maskini la Afrika linaendelea kujitahidi kupata Umoja,amani na maendeleo ambayo yalikuwa katika ndoto ya Nkurumah ya kuwa siku moja na United States of Afrika.
Hata hivyo wenye kutilia shaka wanasema hadi sasa bara la Afrika licha ya kupata uhuru wake wa kisiasa limebakia katika hali ya ufukara, vita vya kikabila,pamoja na mfarakano mambo ambayo yamezuia maendeleo kwa muda mrefu.