1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 50 ya urafiki wa Ujerumani na Ufaransa

21 Desemba 2012

Maadui wakubwa wageuke kuwa marafiki, hilo ndilo lengo la mkataba wa Elysée uliotiwa saini mwaka 1963 kati ya Ujerumani na Ufaransa ili kuzipatanisha nchi hizo mbili baada ya kupigana vita viwili vikuu vya dunia.

Kansela Konrad Adenauer [kushoto) na rais Charles de GaullePicha: picture-alliance/dpa

Kilichoandikwa katika mkataba kati ya shirikisho la jamhuri ya Ujerumani na jamhuri ya Ufaransa kuhusu urafiki kati ya nchi hizo mbili hakijajaza hata kurasa sita.

Baridi ilikuwa kali kupita kiasi pale rais wa Ufaransa Charles de Gaule na kansela wa Ujerumani Konrad Adenauer walipokutana katika kasri la Elysée mjini Paris.Mji mkuu huo wa Ufaransa ulikuwa kiza,magharibi ya January 23 mwaka 1963.Viongozi hao wa serikali na wajumbe waliofuatana nao walikuwa katika ukumbi unaong'ara kwa taa za rangi mbali mbali,kuta zenye rangi ya kisamli na milango ya viyooo iliyochogwa na kupakwa maji ya dhahabu.Maelezo ya mwisho mwisho yakatolewa kabla ya Konrad Adenauer na Charles de Gaulle kutia saini makubaliano kuhusu ushirikiano kati ya Ujerumani na Ufaransa-Mkataba wa Elysée kama unavyoitwa.Lilikuwa tukio la kihistoria na la kusisimua.

Wanasiasa wote wawili walikumbatiana.De Gaulle akambusu Adenauer juu ya shavu.Wametambua kwamba kwa kutia saini mkataba huo wamefungua pia ukurasa mpya katika historia ya Ujerumani na Ufaransa pamoja pia na kuzidisha juhudi za kuimarisha mshikamano barani ulaya.Matumaini ya kulifikia lengo hilo,yalishadidiwa na kansela Konrad Adenauer wakati wa mkutano na waandishi habari aliposema kwa kifaransa-lugha ya majirani zake:"Bila ya mkataba huu,hakutakuwepo na Umoja barani Ulaya.Mbinu zinaweza kubadilika,lakini muhimu zaidi ni kutopoteza imani ya marafiki."

Charles de Gaulle na kansela Adenauer wanakumbatiana baada ya kusaini mkataba wa ElyséePicha: Getty Images

Mkataba wa Elysée ambao muda mfupi baadae ukatajwa kuwa "mkataba wa urafiki kati ya Ujerumani na Ufaransa" ni hatua muhimu katika historia ya uhusianao kati ya nchi hizi mbili.Makubaliano ya kujongeleana Ujerumani na Ufaransa yamechangia pakubwa kuwafanya mahasimu hao wawili wa zamani kuwa washirika wakubwa na muhimu barani Ulaya.Katika mkataba huo serikali za nchi hizi mbili zimeahidi kushauriana katika masuala yote muhimu yanayohusu siasa ya nje,usalama,vijana na utamaduni.Wamekubaliana pia mazungumzo yawe yakifnyika kati ya wawakilishi wa serikali za nchi hizi mbili na kwa wakati maalum .

Suluhu hiyo imejitokeza kuwa ni muhimu pia kwasababu imebainisha kwamba Ulaya inaweza kuishi kwa amani,anasema muasisi wa jarida la "Dokumente"linalohimiza majadiliano kati ya Ujerumani na Ufaransa,Gérard Foussier:"Mapema katika miaka ya sitini bado kulikuwa na watu waliokuwa wakizungumzia kuhusu maadui.Na ilikuwa muhimu sana kuona kwamba anglao madola mawili yenye wakaazi wengi zaidi barani Ulaya yanajikuta katika hali ya kutozungumzia tena kuhusu uadui na badala yake wanazungumzia kuhusu urafiki na ushirikiano."

Uhusiano kati ya Ujerumani na Ufaransa unasifiwa kuwa mfano mwema wa kuigizwa.Mataifa mengine ya Ulaya na hasa mataifa jirani daima yamekuwa yakikumbusha "mfano mzuri wa kuigizwa" wa masikilizano.Mada hiyo hiyo inachambuliwa katika kitabu kilichochapishwa na Stefan Seidendorf wa taasisi ya Ujerumani na Ufaransa mjini Ludwigsburg.Kitabu hicho kinachoitwa "Uhusiano wa Ujerumani na Ufaransa- ndio wa kuigizwa katika utaratibu mpya wa Amani-kinazungumzia sababu zinazoweza kujitokeza katika mizozo mingine na pia katika uhusiano wa pande mbili.Stefan Seidendorf anakitaja kifungu cha mkataba wa Elysée kinachozungumzia kuhusu mikutano ya mara kwa mara inayowaleta pamoja wawakilishi wa kisiasa wa daraja tofauti kuwa ni mfano unaoweza kuigizwa."Hakuna hata mmoja kati ya wawakilishi hao anaeweza kukwepa kushiriki katika mkutano kama huo na kwa namna hiyo unapewa umuhimu mkubwa hata wakati wa mizozo,pale ambapo watu wangependelea pengine wasionane au kila mmoja angependelea kufuata njia yake."

Mara kadhaa mikutano imekuwa ikifanyika ambapo washirika hawakuwa na mengi ya kuambiana au hawakuwa na chochote cha kuambiana,anasema Seidendorf:""Hata hivyo daima ilikuwa fursa ya kuujua msimamo wa upande wa pili,na kuwa na uhakika kwamba nje ya ukumbi wa mikutano,waandishi habari wanasubiri matokeo ya mazungumzo.Inazuka hisia kwamba kuna watu wanaotegemea kujua zaidi na kwa namna hiyo kuzidisha shinikizo la kufikia maridhiano na makubaliano."

Shule ya chekechea ya Ujerumani na ufaransa mjini ParisPicha: DW/M. Stegemann

Mikutano kama hiyo ya mara kwa mara iliyokubaliwa na kudhaminiwa na makubaliano maalum,inaweza pia kutumika katika nchi nyengine zinazokabwa na mizozo. Mbali na mshikamano wa kisiasa,Seidendorf anausifu pia ushirikiano miongoni mwa mashirika ya huduma za jamii kuwa ni mfano mwema wa kuigiza.Kipeo cha kuona mbali anahisi ni pale rais wa Ufaransa Carles de Gaulle na kansela wa Ujerumani Kondard Adenauer walipowatanguliza vijana kama msingi wa kuimarisha imani kati ya nchi mbili.

Katika mkataba wa Elysée kuna kifungu kinachozungumzia kuhusu " wakala wa vijana wa Ujerumani na Ufaransa" ulioundwa July 5 mwaka huo huo wa 1963.Wakala huo wa vijana umerahisha kukutana mara kadhaa vijana wa nchi hizi mbili.Tangu ulipoundwa karibu vijana milioni nane wa kutoka Ujerumani na Ufaransa wameshiriki katika maandalizi zaidi ya laki tatu ya mijadala na kubadilishana maoni nasema Stefan Seidendorf:"Cha kuvutia zaidi ni ile hali kwamba wakala huo wa vijana kwanza ulikuwa na sura ya jumuia ya kimataifa.Inamaanisha kulikuwa na kanuni ambazo hazihusiani na serikali na hakuna serikali hata moja kati ya hizi mbili inayoweza kuzibatilisha.Inamaanisha wakala huo wa vijana ni kama " taasisi ya wadau wenye haki sawa na serikali" na dio maana waliweza kuleta matokeo ya aina yake."

Kabla ya kupatikana ufanisi,mkataba wa Elysée ulikuwa nusra uvunjike.Bunge la shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Bundestag ambalo lilibidi kuidhinisha mkataba huo,lililazimisha iingizwe dibaji katika mkataba huo inayoshadidia kuwepo uhusiano wa dhati wa kisiasa,kiuchumi na ulinzi pamoja na Marekani,Uingereza pia na jumuia ya kujihami ya NATO.Serikali ya Ufaransa lakini ililenga kupitia msaada wa Ujerumani kuimarisha msimamo wa Ulaya,dhidi ya Marekani.

Rais wa zamani wa Ufaransa Nicolas Sarkozy na kansela Angela Merkel walipokutana katika kasri la Elysée machi 19 mwaka 2011Picha: dapd

Akikasirishwa na uamuzi huo,inasemekana rais Charles de Gaulle alisema katika kikao kimoja cha washauri wake waaminifu tunanukuu"mikataba ni sawa na mawardi na wasichana....wana wakati wao."Mwisho wa kumnukuu .De Gaulle alipofanya ziara rasmi mjini Bonn July mwaka 1963,mwenyewake kansela Adenauer walipokuwa katika katika karamu ya chakula cha usiku alimjibu mgeni wake na kumwaambia "Mawardi na wasichana bila ya shaka wana wakati wao lakini bustani ya mawardi hudumu milele ikiwa itatunzwa-na hivyo ndivyo utakavyokuwa mkataba tuliotia saini."Mwisho wa kumnukuu kansela wa Ujerumani wa wakati ule Konrad Adenauer.

Na hivyo ndivyo unavyoonekana kuwa mkataba wa urafiki kati ya Ujerumani na Ufaransa-miaka 50 baada ya kutiwa saini katika kasri la rais mjini Paris-Elysée.

Mwandishi:Bosen,Ralf/Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi