1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 55 ya kuanza kujengwa Ukuta wa Berlin

13 Agosti 2016

Ujerumani Jumamosi (13.08.2016) imekuwa na kumbukumbu ya miaka 55 tokea kuanza kujengwa kwa Ukuta wa Berlin iliougawa mji huo takriban miongo mitatu watu 138 walipoteza maisha yao wakati wa kujaribu kuvuka ukuta huo.

Deutschland
Picha: picture-alliance/dpa/J.Carstensen

Meya wa mji wa Berlin Michael Mueller aliweka shada la mauwa katika kituo kikuu cha kumbukumbu kwenye mtaa wa Bernauer na kuhudhuria misa katika Kanisa la Upatanisho la Kiprotestanti ambalo limejengwa katika eneo la zamani la mpaka.

Ujenzi wa ukuta huo ulianza tarehe 13 mwezi wa Augusti mwaka 1961 kwa kuongozwa na Walter Ulbricht kiongozi wa kikomunisti ya Ujerumani ya Mashariki iliokuwa chini ya ushawishi wa Muungano wa Kisovieti wakati huo ikijulikana kama Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani (GDR).

Suala la Berlin lilikuwa maalum ukiwa kama mji mkuu uliogawiwa katika kanda nne chini ya ushawishi wa washindi wa vita vikuu vya pili vya dunia.

Kimaumbile Ukuta wa Berlin ulikuwa umegawiwa katika kanda tatu za magharibi mwa mji huo ambapo vikosi kutoka Marekani,Uingereza na Ufaransa bado vimewekwa hapo kwa upande wa kanda ya mashariki kulitengwa eneo ndani ya sekta kubwa ya Muungano wa Kisovieti.

Ukuta umedumu miaka 28

Takriban ukiwa na urefu wa kilomita 155 ukuta huo uligawa Berlin kwa zaidi ya miaka 28."Hakuna mtu mwenye nia ya kujenga ukuta." alitamka hayo Walter Ulbricht mkuu wa Baraza la Taifa la Ujerumani Mashariki katika mkutano wa kimataifa Ujerumani Mashariki hapo tarehe 15 Juni mwaka 1961. Katika kipindi kisichozidi miezi miwili baadae alfajiri ya Augusti 13 wafanyakazi wa shughuli za ujenzi walianza kutandaza waya za senyen'ge kupitia barabara zote kuelekea maeneo ya Berlin Magharibi.

Alama ya upanisho katika Kituo cha Kumbukumbu cha Ukuta wa Berlin katika mtaa wa Bernauer mjini Berlin.Picha: picture-alliance/dpa/J. Carstensen

Ilikuwa ni siku mbaya kwa wananchi wa Ujerumani kwa miaka 28 Ukuta wa Berlin uliutenganisha mji huo kati ya mashariki na magharibi.

Wakaazi wa Berlin walikuwa katika fadhaa.Aliyekuwa meya wa mji huo na baadae kuwa kansela Willy Brandt alisema masaa machache baadae akiwa mbele ya jengo la bunge mjini humo kwamba "uzio wa kambi ya mateso" umetandazwa hadi katikati ya mji wa Berlin.

Alama ya Vita Baridi

Ukuta huo wa Berlin ulikuja kusimama kwa siku 10,315 na kuwa alama ya Vita Baridi vilivyoigawa dunia katika makundi mawili hasimu : magharibi kwa mabepari na mashariki kwa ukomunisti.

Ukuta wa Berlin ukijengwa 1961.Picha: picture-alliance/dpa

Kugawika kwa Ujerumani kulimalizika rasmi hapo Novemba 9 mwaka 1989 na kwa mujibu wa data ziliopo hivi sasa takriban watu 138 walipoteza maisha wakati wakijaribu kuuvuka Ukuta wa Berlin akiwemo Peter Fechter mwenye umri wa miaka 18 ambaye alikuwa mmojawapo wa wahanga wa mwanzo kuuwawa kwa kupigwa risasi na walinzi wa mpakani wa GDR wakati akijaribu kukimbilia Berlin Magharibi mwaka mmoja baada ya kujengwa kwa ukuta huo.

Idadi ya wahanga waliouwawa pembezoni mwa ukuta huo ambao ulitenganisha Ujerumani ya Mashariki na magharibi bado inaendelea kuchunguzwa.

Mwandishi : Mohamed Dahman /dpa/DW

Mhariri : Sylvia Mwehozi