1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 60 ya UNESCO

Helle Jeppesen / Maja Dreyer16 Novemba 2005

Miaka 60 iliyopita, tarehe 16 Novemba 1945, shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO, liliasisiwa. Mwaka ule ule tu, Vita vya Pili vya Dunia vilimalizika na watu wengi duniani kote walijitahidi kuendesha maisha yao ya kila siku. Je, dunia kama hiyo, inaweza kumudu utamaduni?

Kwenye sherehe ya miaka 60 ya UNESCO
Kwenye sherehe ya miaka 60 ya UNESCOPicha: Montage/dpa

Waasisi wa UNESCO walibadilisha swali hilo, wakauliza: Je, tunaweza kumudu kutoufikiria utamaduni? Kwa maoni yao, vita huweza kuzuiliwa tu katika akili za watu. Dibaji ya katiba ya UNESCO inasema: “Kwa kuwa vita vinasababishwa na akili ya watu, lazima kujenga wazo la amani katika akili za watu.”

Bado vita vinaendelea katika nchi nyingi duniani, na kama rais wa Ujerumani, Horst Köhler, aliposisitiza katika hotuba yake ya kusherehekea miaka 60 ya UNESCO mjini Paris, heshima ya watu inatishiwa na hatari nyingi, kama vile umaskini, maendeleo yasiyotosha, ugaidi na ukosefu wa uhuru.

Hata hivyo, kwa mujibu wa rais wa Ujerumani, akili za watu zimebadilika. Köhler alisema: “Mashirika ya Kimataifa kama UNESCO yanapigania kulinda heshima ya watu na yanasaidia tamaduni mbali mbali ziishi pamoja kwa amani. Pamoja na hayo, umma wa kimataifa unaonyesha masikitiko kwa maisha ya kila mmoja na maisha ya mataifa mbali mbali yanayopitia mateso ya nguvu, madhara, ubaguzi na umaskini.”


Ukiwauliza watu wa kawaida, jina la UNESCO linamaanisha nini, wengi wanajibu ni kitu kinachohusiana na Umoja wa Mataifa ama kinachohusiana na utamaduni. Ni wachache tu wanaojua yote, yaani elimu, sayansi na utamaduni. Hata hivyo, UNESCO lilianzisha kampeni kubwa ya kuwafundisha watu kusoma na kuandika duniani kote. Kwenye mkutano mjini Dakar, Senegal, mwaka 2000, nchi wanachama wa UNESCO zilikubali kujitahidi kufikia malengo manane ya elimu hadi mwaka 2015 – kama ni kutoa bure elimu ya msingi kwa wavulana na wasichana, kupunguza nusu idadi ya watu wasioweza kusoma wala kuandika, na kuondoa ubaguzi wa wanawake katika mfumo wa elimu.

Ripoti kuhusu hali ya elimu duniani iliyochapishwa wiki iliyopita mjini London, Uingereza, ilionyesha kwamba tatizo la nchi nyingi hasa ni kuendeleza elimu ya msingi ili kupunguza idadi ya watu wasioweza kusoma wala kuandika. Idadi hii kwa jumla ni watu milioni 770.

Kwa mujibu wa mkuu wa ripoti hiyo, Nicholas Burnett, ni lazima zichukuliwe hatua sasa hivi kupambana na tatizo hilo badala ya kusubiri jitihada za kuneemesha elimu ya msingi zitakazoleta mafanikio. Bw. Burnett anasema: “Njia hiyo haifai kwa sababu inamaanisha kutowajali watu milioni 770 wasioweza kusoma wala kuandika. Tatizo hilo linahusu kila mtu wa tano kati ya watu wazima duniani. Kwa kufanya hivyo tusingewajali asilimia 20 ya watu. Haya hayawezekani kabisa!”


Bw. Burnett lakini pia alieleza juu ya mafanikio yaliosfikiwa, kama kwa mfano nchini China ambapo idadi ya watu wasioweza kusoma wala kuandika ilipungua kwa milioni 100. Kwa upande wa sayansi, UNESCO liliunda mfumo wa kuonya hatari za Tsunami katika Bahari ya Pazifiki. Shughuli ya UNESCO inayojulikana vizuri zaidi, bila shaka, ni orodha ya maeneo ya urathi wa dunia. Zaidi ya mahala 700 katika kila pembe ya dunia palichaguliwa kupewa ulinzi maalum kutokana na umuhimu wao wa kiutamaduni.

Siyo tu majengo yanayoorodheshwa, kama vile miji mikongwe ya Zanzibar na Lamu, makaburi ya wafalme wa Buganda ya Kasubi, Uganda, hekalu la mjini Cologne, Ujerumani, au Taj Mahal, nchini India, bali pia maeneo mazima kama mbuga za taifa za wanyama na misitu mbali mbali katika nchi za Afrika Mashariki kama vile Serengeti, Ngogongoro ama Mlima Kenya.

Jengo jingine linalohifadhiwa na UNESCO ni daraja kongwe katika mji wa Mostar, nchini Bosnia-Herzegowina. Daraja hilo lililovunjika katika vita vya Yugoslavia lilijengwa upya na likazinduliwa mwaka uliyopita na mkuu wa UNESCO, Kaichiro Matsuura. Katika hotuba yake Bw. Matsuura alilinganisha daraja la Mostar na jitihada za kujenga daraja baina ya watu, yaani kazi kuu shirika la UNESCO linajishughulisha nayo: “Mwishowe nataka kusisitiza kwamba jitihada za kujenga daraja baina ya watu na jumuiya hazimalizi. Ukiangalia jengo lenyewe, kulijenga upya inawezekana. Lakini kwa kweli, kazi ni kujenga amani inayobaki. Daraja kongwe la Mostar liwe dalili kwa changamoto hiyo.”