Miaka 70 ya kukombolewa kwa kambi ya mateso Buchenwald
11 Aprili 2015Manusura wa kambi hiyo ya mateso ya Buchenwald ilioko karibu na mji wa mashariki wa Ujerumani wa Weinmar wamekusanyika kwa kumbukumbu ya kukombolewa kwa kambi hiyo na wanajeshi wa Marekani hapo tarehe 11 mwezi wa Aprili mwaka 1945.
Washiriki wa kumbukumbu hiyo walikaa kimya kwa dakika moja katika uwanja mkuu wa kambi hiyo kuwakumbuka wafungwa wenzao waliouwawa ambapo baadae washiriki hao wakiwemo maveterani wa kijeshi wa Marekani walihudhuria tukio jengine la kumbukumbu katika Ukumbi wa Taifa wa Tamthiliya katika mji huo wa Weinmar.
Manusura walifika kwenye kambi hiyo ya mateso ya zamani wakitokea nchi mbali mbali duniani ikiwa ni pamoja na Israel, Australia Marekani,Canada na mataifa kadhaa ya Ulaya. Manusura hao walikuwa ni wafungwa wa kwanza nchini Ujerumani kuachiliwa huru kutoka mikono ya utawala wa Wanazi.
Hapo mwaka 1945 kambi hiyo ya mateso ya Buchenwald ilikuwa ndio kambi kubwa kabisa ya mateso ilioko kwenye ardhi ya Ujerumani.
Kumbukumbu za manusura
Mmojawapo wa manusura wa kambi hiyo ni Henry Oster ambaye anakumbuka kwamba alidhani mfungwa mwenzake kwenye kambi hiyo alikuwa amepagawa wakati aliposema miaka 70 iliopita kwamba kambi hiyo ya mateso ilikuwa ikikombolewa na kukomesha mateso ya wafungwa 21,000 waliokuwa bado wako haki kwenye kambi hiyo.
Oster mwenye umri wa miaka 86 aliitembelea kambi hiyo ilio karibu na mji wa Weinmar kwa mara ya kwanza tokea kukombolewa kwake hapo tarehe 11 mwezi wa Aprili mwaka 1945.Buchenwald ni kambi kubwa ya mateso ya kwanza kabisa kuingiliwa na vikosi vya Marekani mwishoni mwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Amekaririwa akisema "Kile nilichokiona hapa ni kwamba kulikuwako na kambi za wanajeshi na katika kila kambi kulikuwa na mrundiko wa maiti,jambo hilo linabakia kwenye kumbukumbu yako milele."
Oster ameongeza kusema " Wakati anapoulizwa mambo yalikuwa vipi katika kambi hiyo ya Buchenwald,mara moja inakuja tena sura za maiti hizo."
Tajiriba za wahanga
Oster ambaye ni Myahudi aliyezaliwa Ujerumani alipelekwa eneo la kimaskini la madongo poromoka la Lodz nchini Poland wakati nchi hiyo ilipokuwa ikikaliwa kwa mabavu na Manazi wa Ujerumani hapo mwaka 1941 na baadae akapelekwa kambi ya kifo cha Auschwitz-Birkenau.Baba yake alikufa kwa njaa na mama yake alikufa kwa kunyunyuziwa gesi siku waliowasili katika kambi ya Auschwitz.
Hapo mwezi wa Januari mwaka 1945 alipelekwa kuungana na kile kilichokuwa kikijulikana kama "msafara wa kifo " kuelekea kambi ya mateso ya Bchenwald wakati utawala wa Wanazi ulipokuwa ukiwalazimisha wafungwa wao kwenda upande wa magharibi kutokana na kuelemewa na vikosi vya Urusi.
Oster baadae alipelekwa kwenda kuishi kwenye kituo cha mayatima nchini Ufaransa na halafu akahamia Marekani mwaka 1946 ambapo hivi sasa anaishi Woodland Hills,Carlifonia.
Yaliyotokea hayasahauliki
Buchenwald pia imeacha kumbukumbu zisizofutika kwa wakombozi wake.James Anderson mwenye umri wa miaka 91 kutoka Indianapollis nchini Marekani alikwenda akiwa kama mfanyakazi wa tiba na anakumbuka wafungwa wengi walikuwa dhaifu mno kiasi cha kushindwa hata kutembea.
Takriban wafungwa 250,000 walishikiliwa katika kambi hiyo ya mateso ya Buchenwald kuanzia kufunguliwa kwake hapo mwaka 1937 hadi wakati wa kukombolewa kwake.Watu wanaokadiriwa kufikia 56,000 wameuwawa kwenye kambi hiyo ikiwa ni pamoja na wafungwa wa kisiasa,watu waliotajwa na Manazi kama sio watu wa kawaida, wafungwa wa kivita wa iliokuwa muungano wa Kisovieti,watu wa jamii ya Waroma na Wasinti wa Ulaya na Wayahudi kama 11,000.
Eneo la kambi hiyo hivi sasa linatumika kama kituo cha kumbukumbu chenye kuonyesha historia ya kambi hiyo.
Mwandishi : Mohamed Dahman / AP/DW/dpa
Mhariri : Daniel Gakuba