1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka mitano tangu maelfu ya wakimbizi walipoingia Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Gakuba, Daniel
31 Agosti 2020

Miaka mitano baadaye kauli maarufu ya kansela Angela Merkel ya "Wir Schaffen Das" yaani "Tutaweza" imesababisha hisia tofuati kwa raia wa Ujerumani juu ya zoezi la kuwapokea wakimbizi mnamo mwaka 2015.

Deutschland Flüchtling macht Selfie mit Merkel in Berlin-Spandau
Picha: Reuters/F. Bensch

Baadhi ya raia wa Ujerumani walikuwa na matumaini ya kulimudu zoezi hilo na wengine walikuwa na hofu na wasi wasi. Jee hali sasa ikoje baada ya miaka mitano kupita. Jee wakimbizi hao walitoka wapi? walikuwa na elimu ya kiwango gani na Jee watapata ajira na makaazi, maswali hayo yalijadiliwa nchini Ujerumani wakati huo, ambapo wakimbizi zaidi walikuwa wanamiminikia nchini humu mnamo mwaka 2015. Miaka mitano baada ya wakimbizi  hao kuwasili watu wanaijadili kauli iliyotolewa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.

Merkel alisema wakati huo kwamba serikali yake ilikuwa na uwezo wa kuimudu idadi kubwa ya wakimbizi zaidi ya milioni moja walioingia nchini Ujerumani. Mjadala huo unafanyika kwa mihemko lakini hakuna haja ya kuwapo hofu na tuhuma. Idadi kubwa miongoni mwa watu hao walitoka Syria, Afghanistan na Iraq yaani nchi ambazo migogoro ya kivita na ugaidi ni mambo ya maisha ya kila siku. Hata hivyo haina maana kwamba watu wote walioomba hifadhi ya ukimbizi walikubaliwa.

Wafuasi wa chama cha AfD kinachopinga wahamiaji nchini Ujerumani.Picha: Reuters/W. Rattay

Je! Inawezekana kuwa Ujerumani ilihitaji wakimbizi ili kukabiliana na uhaba wa wafanyikazi wenye ujuzi? Au Wakimbizi ni mzigo mzito kwa mifuko ya usalama wa jamii nchini Ujerumani? Wajerumani mpaka sasa bado wamegawanyika juu ya suala hili. Chama cha mrengo mkali wa kulia kinachojiita chama mbadala kwa Ujerumani (AfD) hakikubaliani na suala hili la wakimbizi kwa sababu kinaona kwamba nchi inajiongezea gharama, sababu hii ni miongoni mwa mambo mengine kadhaa yanayopingwa na chama hicho na vyama vingine vya kisiasa vinavyowakilishwa bungeni pamoja na vyama vya waajiri vinasisitiza umuhimu wa wakimbizi katika soko la ajira.

Watu wanaokuja Ujerumani kama wakimbizi wanaotafuta hifadhi nchini humu wanahitaji kupata mafunzo kwanza ili kuwawezesha kupata kazi. Kiwango cha elimu kinatofautiana kulingana na nchi ya asili alikotoka mkimbizi.

Jambo moja ni wazi kwamba idadi ya watu wanaoomba hifadhi ya ukimbizi nchini Ujerumani imepungua kabisa tangu mwaka 2015. Mnamo mwaka huo jumla ya watu milioni moja waliomba hifadhi ya ukimbizi nchini Ujerumani. Miaka mitano baada ya wakimbizi kuwasili nchini Ujerumani ni asilimia 11 tu ya wajerumani wanaounga mkono wazo la kuwapokea wakimbizi zaidi. Idadi ya wale wanaopinga imeongezeka tangu mwaka 2015.

Chanzo:/DW

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW