1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka mitatu baada ya mripuko wa bandari ya Beirut

4 Agosti 2023

Leo hii Lebanon inaadhimisha miaka mitatu tangu kutokea kwa mripuko mkubwa zaidi katika historia ya taifa hilo uliolitikisa jijiji la Beirut na kuuwa watu zaidi ya 220.

Libanon | 2. Jahrestag der Beiruter Hafenexplosion
Picha: Houssam Shbaro/AA/picture alliance

Hata hivyo tangu wakati huo, hakuna aliyefikishwa katika mikono ya kisheria huku shinikizo la kisiasa na kisheria likisimamisha uchunguzi wake.Ikumbukwe tu, kwamba Agosti  Agosti 4, 2020, mripuko mkubwa katika bandari ya Beirut uliharibu maeneo mengi ya mji mkuu wa Lebanon, na kuua zaidi ya watu 220 na kujeruhi wengine takriban 6,500.

Mamlaka ilisema maafa hayo yalisababishwa na moto katika ghala ambapo hifadhi kubwa ya kemikali ya viwandani ilikuwa imehifadhiwa kiholela kwa miaka kadhaa.Miaka mitatu baadaye, uchunguzi umesalia katika mkwamo hali ambayo imewaacha manusura wakiwa bado na hamu ya kupata majibu.

Tangazo la maandamano ya mjini Beirut.

Eneo la mji wa Beirut karibu na bandari ya mji huo.Picha: Houssam Shbaro/AA/picture alliance

Mchana wa leo (04.08.2023) kundi kuu la wanaharakati wanaowakilisha familia za waliouawa limeitisha maandamano ambayo yatakusanya watu katika eneo la bandari ya Beirut. Sandra Wahabi ni mkaazi wa jiji la Beirut. "Mambo yanaanza kurudi kama yalivyokuwa, lakini hakuna hisia za  furaha. Unapata hisia ya kama kila mtu anajifanya kuwa na furaha. Nadhani bado tunahitaji muda. Ingawa miaka mitatu imepita lakini jambo lenyewe ni kama jipya. Bado tunakumbuka kila mara wakati mgumu tuliopitia."

Sandra kama ilivyo kwa wakazi wengi wa jiji hilo ana kumbukumbu nzuri ya namna mkasa wa Agosti 4 ulivyotokea."Kusema kweli nazungumza kwa uzoefu binafsi, nilikuwa karibu na eneo la  mripuko, nilikuwa naishi mbele tu, ya bandari, umbali wa mita 600, nyumba iliharibika na vitu vya ndani vilivunjika lilikuwa jambo gumu sana na bado nahisi uchungu wake. "

Changamoto ya upatikanaji haki Lebanon.

Tangu mwanzoni kabisa mwa tukio hilo, uchunguzi wake umekuwa ukizongwa na changamoto nyingi za kisiasa na kisheria. Itakumbukwa Desemba mwaka 2020 mkuu wa timu ya upelelezi Fadi Sawan alifungua mashtaka ya uzembe dhidi ya waziri mkuu wa zamani Hassan Diab na mawaziri wengine wa zamani watatu. Lakini baada ya kuongezeka kwa shinikizo la kisiasa Sewan aliondolewa katika kesi hiyo.

Nae mrithi wake, Tarek Bitar hakuweza kufanikiwa katika takwa la kulitaka bunge kuwaondolea kinga wabunge ambao pia waliwahi kuwa mawaziri. Hatua hiyo ilichangizwa na kundi lenye nguvu la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran baada ya kuanzisha kampeni dhidi ya Bitar, likimtuhumu kuwa anafanya upendeleo na kutaka afukuzwe kazi.

Desemba 2021, Bitar alisimamisha uchunguzi wake baada ya kupata mapingamizi ya kisheria kutoka kwa washtakiwa. Lakini pia katika hatua ya kushangaza ya mapema Januari hii kiongozi huyo wa upelelezi, ikiwa ni zaidi ya miezi 13, aliwafungulia mashtaka washukiwa wapya wanane wakiwemo maafisa wa ngazi za juu wa usalama na mwendesha mashtaka mkuu wa Lebanon, Ghassan Oueidat.

Soma zaidi:Gavana wa Benki Kuu ya Lebanon kujiuzulu

Na jana Alhamisi, watu 300 na mashirika ya utetezi wa haki za binaadamu la Human Rights Watch na Amnesty International yalirejelea wito wao kwa Umoja wa Mataifa kuanzisha timu ya ujumbe wa kutafuta ukweli jambo ambalo limepingwa mara kwa mara na serikali ya Lebanon.

Chanzo: AFP

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW