1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 3 tangu apinduliwe, Bazoum bado yuko kizuizini

1 Aprili 2026

Muda wa urais wa kiongozi aliyeondolewa madarakani wa Niger, Mohamed Bazoum, unamalizika rasmi leo, lakini hana matumaini yoyote ya kuachiwa kutoka kizuizini au hata kufikishwa mahakamani.

Mohamed Bazoum akiwa Paris wakati akiwa bado madarakani
Rais Mohamed Bazoum alipowasili kwa chakula cha jioni katika Jumba la Elysee, kando ya Mkutano Mpya wa Mkataba wa Fedha wa Kimataifa, jijini Paris, mnamo Juni 22, 2023.Picha: Stevens Tomas/ABACA/IMAGO

Bazoum, mwenye umri wa miaka 66, aliapishwa kuwa rais Aprili 2, 2021 baada ya kushinda uchaguzi wa kidemokrasia kwa asilimia 55 ya kura. Lakini tangu Julai 26, 2023, amekuwa akishikiliwa katika sehemu ya ikulu ya rais mjini Niamey pamoja na mke wake baada ya jeshi linaloongozwa na Jenerali Abdourahamane Tiani kupindua serikali yake. Tangu kupinduliwa hajawahi kukubali kujiuzulu.

Mawakili wake wanasema Aprili 2 haipaswi tena kuchukuliwa kuwa mwisho rasmi wa muhula wake wa urais kwa kuwa hakuruhusiwa kutekeleza majukumu yake kwa karibu miaka mitatu.

Lakini mtafiti wa siasa Valery Ntwali, anayejikita katika mapinduzi ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, alisema kwamba kwa mujibu wa sheria za Niger, kiongozi aliyeondolewa madarakani "amepoteza uhalali wake kwa kuwa katiba iliyomchagua ilisitishwa.”

Wafuasi wa mapinduzi wakiandamana mbele ya makao makuu ya chama tawala nchini NigerPicha: Fatahoulaye Hassane Midou/AP Photo/picture alliance

Watawala wa kijeshi Niger walisitisha katiba na kuibadilisha kwa katiba mpya iliyoidhinishwa Machi mwaka jana, inayowawezesha kubaki madarakani kwa miaka mingine mitano inayoweza kurefushwa. Hakujawa na uchaguzi wowote tangu mapinduzi.

Haijafahamika wazi ni sheria gani inapaswa kutumika kama ni ile ya jeshi lililotwaa madaraka kwa nguvu, au ile ya kabla ya mapinduzi.

‘Kushindwa'

Ingawa utawala wa kijeshi wa Niger kama ilivyo kwa majirani zake Burkina Faso na Mali umeweka suala la uhuru wa nchi hiyo kama kipaumbele chake na kuwa na uhasama na baadhi ya mataifa ya Magharibi, lakini haijatengwa kabisa kimataifa.

Hivi karibuni imeanza tena mawasiliano na Marekani kuhusu ushirikiano wa kiusalama, miaka miwili baada ya kuwalazimisha wanajeshi wa Marekani wanaopambana na wanamgambo kuondoka Niger, wakati huo huo ikizidisha ushirikiano na Urusi.

Kiongozi wa kijeshi wa Niger Abdourahamane TianiPicha: Télé Sahel/AFP

Uhusiano wake na Ufaransa umeendelea kuwa dhaifu, iliyokuwa ya kwanza kutoa wito kwa Bazoum aachiwe, kama ilivyokuwa kuwa kwa Umoja wa Ulaya.

Bunge la Ulaya mapema mwezi huu lilipitisha azimio linalotaka kuachiwa mara moja kwa Bazoum, hatua iliyozua hasira kwa watawala wa kijeshi wa Sahel na maandamano mjini Niamey na kiasi kidogo mjini Ouagadougou.

"Tunathibitisha kwa nguvu na bila kusita kukataa azimio hili, ambalo tunaliona kama uingiliaji usiokubalika katika masuala ya ndani ya mamlaka ya taifa mwanachama wa Shirikisho la Nchi za Sahel" alisema mwandamanaji mmoja.

Umoja wa Ulaya hufadhili miradi ya maendeleo na vita dhidi ya wanamgambo wa itikadi kali ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakifanya mashambulizi katika nchi za Sahel, ikiwa ni pamoja na Niger.

Mawakili wake wanasema baada ya karibu miaka mitatu, Bazoum "bado anashikiliwa mahali pale pale na katika mazingira yaleyale” bila madirisha, milango, au wageni isipokuwa daktari wake.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW