1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Miaka mitatu ya vita Sudan raia waendelea kuteseka

Zainab Aziz AP/RTRE/AFP
15 Aprili 2026

Vita vya nchini Sudan vimetimiza miaka mitatu. Vita hivyo vimewatumbukiza raia wengi wa nchi hiyo kwenye mgogoro wa kibinadamu huku njaa ikiwa imekithiri na bila kupatikana ufumbuzi wa kuvimaliza vita hivyo.

Sudan Milima ya Nuba | Vita | Wakimbizi wa ndani wakisubiria misaada
Wakimbizi wa ndani wa Sudan wakisubiria misaada kwenye eneo la milima ya Nuba katika jimbo la Kusini la KodorfanPicha: Marco Simoncelli

Mapigano hayo yamewatumbukiza Wasudan wengi kwenye baa la njaa, yamesababisha mgogoro mkubwa wa wakimbizi huku zaidi ya watu milioni 30 wakihitaji msaada. Pande zote mbili zinazopigana yaani jeshi la taifa chini ya Mwenyekiti wa Baraza la Kijeshi la Mpito, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na Vikosi vya RSF vinavoongozwa na Jenerali Muhammad Hamdan Dagalo zimeshutumiwa kwa kufanya ukatili kama vile mauaji ya kiholela na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya raia.

Shirika la Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa (WFP) limesema watu wa Sudan bado wanalazimika kukabiliana na mapigano makali, kuhama makazi yao na kutumbukia kwenye umaskini huku mamilioni wakikosa chakula, mazingira safi, maji na makazi, WFP imesema watu milioni 21.2 wanakabiliwa na njaa kali. Carl Skau, Naibu Mkurugenzi wa WFP amesema: "Miaka mitatu ya vita nchini Sudan imesababisha mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu duniani. Mgogoro huo umeharibu maisha ya watu na umesababisha mamilioni ya watu kukumbwa na baa la njaa. Wafanyakazi wa misaada wanashambuliwa, malori na maghala ya chakula pia yanaendelea kushambuliwa, hali hiyo inayaweka maisha ya wenzetu hatarini na kuvuruga jitihada zetu za kutoa misaada. Kwa mamilioni ya watu nchini Sudan, WFP ndiyo njia pekee ya kuokoa maisha yao."

Kushoto: Mwenyekiti wa Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan. Kulia: Kiongozi wa vikosi vya RSF, Jenerali Muhammad Hamdan DagaloPicha: SNA/IMAGO/Mahmoud Hjaj/IMAGO

Wafadhili wakutana Berlin

Wakati ambapo Sudan inashuhudia vita kwa miaka mitatu tangu kuanza kwa mgogoro huo na sasa vinaingia katika mwaka wa nne, wafadhili watakusanyika mjini Berlin kwa ajili ya mkutano wa kimataifa unaolenga kufufua mazungumzo ya amani na pia kuhamasisha misaada kwa ajili ya watu wa Sudan wanaokabiliwa na mmoja kati ya migogoro mibaya zaidi ya kibinadamu duniani.

Wizara ya Maendeleo ya Ujerumani katika taarifa yake imesema nchi hiyo itatoa Euro milioni 20 za ziada kwa Sudan mwaka huu wa 2026 huku ahadi zaidi za ufadhili zikitolewa. Ujerumani inalenga kukusanya ahadi za wafadhili angalau Euro bilioni 1 katika mkutano huo.

Waaziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Yvette Cooper katika mkutano wa kimataifa mjini Berlin kuhusu SudanPicha: Odd Andersen/AFP

Waziri wa Mambo ya Nje Johann Wadephul, amesema lengo hilo linaweza kufikiwa alipozungumza na kituo cha redio cha Deutschlandfunk.

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Mahamoud Ali Youssouf, yupo mjini Berlin kwa ajili ya mkutano huo. Amesema wakati dunia nzima inaitazama mizozo ya Iran na Ukraine pamoja na migogoro mingine, anathamini sana kwamba Ujerumani imeweka ajenda hii mezani ili dunia isipoteze mtazamo kuhusu mateso ya watu wa Sudan.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW