1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka miwili ya Buhari madarakani

29 Mei 2017

Miaka miwili iliyopita, Muhammadu Buhari wa Nigeria aliwaongoza wapigakura kukomesha miaka 16 ya kutawaliwa na PDP na kukiweka madarakani chama chake cha APC kwa matumaini ya usalama na uchumi imara.

Nigeria Muhammadu Buhari
Picha: picture alliance/AP Photo/S. Aghaeze

Kuja kwa rais huyu mpya madarakani kulichukuliwa kama ishara ya Wanigeria kutaka kuvunja maovu makuu mawili kwenye taifa hilo kubwa kabisa kwa idadi ya watu barani Afrika, nayo ni ufisadi na uasi wa kundi Boko Haram - yote mawili yakitishia misingi iliyolijenga taifa hilo. Ulikuwa pia ni uchaguzi wa kutaka kuiondoa nchi hiyo kwenye uchumi unaotegemea njia moja tu ya uzalishaji.

Miaka miwili baadaye, Wanigeria wana kila sababu ya kuyashangiria mafanikio yaliyopatikana chini ya Buhari, kwa mujibu wa waziri wa habari wa nchi hiyo, Lai Mohammed, angalau kwenye hili la kuwarejesha nyuma wapiganaji wa Boko Haram.

"Wakati rais anaapishwa tarehe 29 Mei 2015, kiasi cha serikali 20 za mitaa kati ya 27 jimboni Borno zilikuwa chini ya Boko Haram, nne huko Adamawa na tatu jimboni Yobe. Hivi sasa, hakuna hata serikali moja ya jimbo iliyo mikononi mwa Boko Haram. Hilo si jambo dogo", anasema waziri huyo wa habari.

Mbali kwenye hilo la kuwashinda nguvu wapiganaji wa Boko Haram, serikali ya APC inajisifia pia kwenye eneo la uchumi, ambako inadai kufanya makubwa katika vita dhidi ufisadi, ambapo kuna kesi mia kadhaa mahakamani, na kuna dalili ya kuutoa uchumi kwenye mserereko wake.

Wananchi walalamikia ugumu wa maisha

Wananchi wanalalamikia hali ngumu ya maisha, ukosefu wa ajira na mwendo hafifu wa kupambana na ufisadi.Picha: DW/S. Olukoya

Lakini majigambo haya ya serikali, hayaonekani kuaminiwa na watu wengine, ambao wanasema serikali inapaswa kufanya mengi zaidi. Mmoja wao ni Juliana Obolonye, raia wa kawaida, anayesema "watu hawawezi kulipa kodi za nyumba, ada za skuli, hawawezi hata kuwalisha watoto wao. Chini ya serikali hii, tunasikia taarifa za watu kuiba supu jikoni na mengine kama hayo. Huu ndio ukweli."

Kama maisha yalivyo magumu kwa Juliana Olobonye, hayana afadhali pia kwa Chesa Chesa, raia mwengine wa Nigeria anayeamini kuwa kuna mambo mengi bado yanapaswa kufanywa na utawala wa Buhari, ingawa naye anakiri kuwa kwenye suala la usalama, Buhari amefanya vizuri.

"Bei za bidhaa ziko juu, hasa vyakula ndivyo viko juu zaidi. Tupo kwenye mserereko wa kiuchumi. Ndio maana nikasema tumeumia. Kwa upande mwengine, ni kweli kwenye suala la usalama kajitahidi kidogo. Hivi sasa wanajihisi wako salama zaidi, ukiacha mapigano machache kati ya wakulima na wafugaji", anasema kijana huyu wa mjini Kano.

Ingawa sasa hali ya afya ya Buhari inaonekana kudhoofika siku hadi siku, Wanigeria wanapaswa kungojea miaka mingine miwili ijayo kupiga kura ya mwisho ya ama kumuonesha imani yao kwake, au kubadilisha kile walichokipigia kura miaka miwili iliyopita.

Mwandishi: Ubale Musa/Mohammed Khelef
Mhariri: Mohamed Abdulrahman 

 
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW