1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michango mingi kwa msaada wa maendeleo

Petra Stein19 Julai 2006

Shirika la kusaidia maskini duniani la makanisa ya Kiinjili ya Ujerumani, liitwalo „Chakula kwa Wote“ jana lilitoa taarifa ya shughuli zake za mwaka 2005 mjini Berlin. Shirika hilo linaendesha miradi yake ya misaada kwa kushirikiana na washirika katika nchi wapokeaji misaada za Afrika, Asia, Latin America na Ulaya Mashariki.

Shirika la "Chakula kwa wote" linakusanya michango ya msaada wa maendeleo
Shirika la "Chakula kwa wote" linakusanya michango ya msaada wa maendeleoPicha: AP

Katika hotuba yake ya kutambulisha taarifa ya mwaka uliopita kwenye mkutano na waandishi habari mkurugenzi wa shirika hilo amelaumu upelekaji wa vikosi vya nchi za Magharibi katika sehemu za migogoro kwa shabaha ya kuleta amani.

Shirika la misaada ya makanisa ya kiprotestanti ya Ujerumani liitwalo “Chakula kwa Wote” lilipata michango ya fedha cha Euro milioni 54,6 mnamo mwaka jana kwa ajili ya miradi ya maendeleo jumla ya 1.100 katika Afrika, Asia, Latin America na Ulaya Mashariki. Mkurugenzi wa shirika hilo, Bibi Cornelia Füllkrug-Weitzel ameonyesha furaha yake akitoa takwimu hii ambayo ni ongezeko la Euro 620 elfu kulinganishwa na mwaka 2004.

Miradi ya kupambana na umaskini kwa njia ya kujisaidia wenyewe, na kujenga jamii ya raia wanaojiamini na kujua haki zao inapewa uzito katika kazi ya shirika la „Chakula kwa Wote“. Hii ndiyo misingi ya kufanikisha mapambano dhidi ya umaskini na kuleta amani ya kudumu katika sehemu za migogoro, kama mkurugenzi Füllkrug-Weitzel alivyosisitiza na akaendelea kwa kutoa mwito kwa serikali kuu ya Ujerumani itilie mkazo zaidi katika kuwaimarisha wananchi katika sehemu hizo na harakati zao za kuleta amani na maridhiano. Ni ndoto – mama huyo ameonya – kufikiri kwamba madola ya Magharibi yangeweza kusuluhisha migogoro yenye vyanzo vingi tofauti kwa njia ya kufanya uvamizi mfupi wa kijeshi. Hata! Bibi Füllkrug Weitzel amesema:

"Katika migogoro yote ndiyo jamii ya wananchi inayotoa mchango muhimu kabisa katika kukomesha mabavu na kutafuta njia za kuleta amani. Ni juu ya wananchi kuhalalisha serikali na kuidhibiti."

Kwa kutoa mfano wa Congo mkurugenzi wa shirika hilo la misaada ya maendeleo la makanisa ya kiinjili ameeleza zaidi umuhimu wa kuimarisha wananchi. Amesema: Washirika wetu nchini Congo wanakaribisha kufanyika kwa uchaguzi huru baada ya miaka mingi. Lakini wana mashaka makubwa kwamba katika hali kama ilivyo nchini mwao kupelekwa kwa vikosi vya Umoja wa Ulaya kwa muda mfupi tu kutakuwa na faida yoyote."

Wanapenda kuona kwamba Umoja wa Ulaya uchukue hatua kamambe za kudumisha amani, kujenga uchumi na demokrasia, kupambana na rushwa, kuwaadilisha askari watoto na kuwaingiza tena katika jamii pamoja na kuleta maridhiano kati ya vikundi mbalimbali vinavyopigana. Muhimu pia ni kuhakikisha kuwa maliasili zitumiwe kwa manufaa ya wananchi. Shirika la “Chakula kwa Wote” linaiomba serikali ya shirikisho la Ujerumani itumie uzito wake kwa ajili hii katika mwaka ujao itakapokuwa na uenyekiti wa Umoja wa Ulaya.