Ufadhili wa mabadiliko ya tabianchi wazidi kupungua
6 Oktoba 2023Ahadi zilizotolewa na mataifa mbalimbali kwa ajili ya kutunisha wakfu wa Umoja wa Mataifa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, katika mkutano unaofanyika Bonn, magharibi mwa Ujerumani zimeshindwa kufikia lengo, hii ikiwa ni kulingana na mamlaka.
Ahadi hizo zimetolewa Alhamisi hii zinalenga kuutunisha mfuko huo uliotengwa kwa ajili ya miradi ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi, katika nchi zinazoendelea, lakini pia hali mbaya ya hewa kati ya 2024 na 2027.
Ahadi hizo zilifikia dola bilioni 9.3 (€ 8.8 bilioni), zikiwa chini ya lengo la dola bilioni 10, na chini ya dola bilioni 200 hadi bilioni 250 ambazo zilikadiriwa kwenye Mkataba wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa juu ya Mabadiliko ya Tabianchi kwamba zingehitajika kila mwaka, hadi itakapofika 2030.
Kiasi gani kilihitajika
Nchi 25 ziliahidi kutoa msaada kwenye Wakfu wa Hali ya Hewa, wakati Ujerumani pekee ikiahidi kutoa yuro bilioni 2. Nchi nyingi, ikiwa ni pamoja na Ujerumani, Austria na Ufaransa, ziliongeza ahadi zao, wakati Denmark, Ireland na Liechtenstein zikiongeza ahadi zao mara mbili zao.
Soma pia:Azimio la Nairobi la hali ya hewa kutiwa saini
Nchi tano, ikiwa ni pamoja na Australia, Italia na Sweden hazikutoa michango yoyote katika mkutano huo wa Alhamisi ingawa ziliahidi kufanyia kazi suala hilo.
Marekani na China, mataifa yenye uchumi mkubwa zaidi duniani ambao pia ni wachafuzi wakubwa wa hali ya hewa hazikuahidi kabisa kutoa fedha.
Washington ilijitetea kwamba iko katika msukosuko wa kifedha kutokana na mkwamo wa bajeti baada ya Chama cha Republican kutaka kulazimisha kufungwa kwa shughuli za serikali, ingawa pia mwakilishi mmoja alisema watalishughulikia hilo.
Soma pia:UNICEF: Watoto milioni 43.1 wayahama makazi yao kufuatia mabadiliko ya tabianchi
China bado haijakubali kujiunga na wakfu huo wa Umoja wa Mataifa.
Ukosoaji juu ya ukosefu wa fedha
Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani pamoja na ya ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo hata hivyo zimesema katika taarifa ya pamoja kwamba "Kiasi kilichokusanywa kinaweza kuwa kikubwa zaidi."
Waziri wa maendeleo ya kiuchumi wa Ujerumani Svenja Schulze, aliyekuwa mwenyeji wa mkutano wa Bonn, alisema nchi zaidi zinahitaji kutoa "mgao wao wa usawa."
"Mbali na mataifa mengine yaliyoendelea kiviwanda, ninadhani mataifa ambao sio wafadhili wa muda mrefu wanatakiwa kuwajibika katika hili. Kwa mfano, mataifa ya Ghuba ambayo yalipata utajiri kutokana na nishati ya mafuta, au mataifa yanayoinukia kama vile China ambayo kwa sasa yanazalisha kaboni kwa kiasi kikubwa," alisema Schulze.
Hata hivyo, mashirika yasiyo ya kiserikali na mashirika ya kiraia yalisema ufadhili ulioahidiwa hauwezi kutosha kugharamia mahitaji ya nchi hizo zinazokabiliwa na adha ya mabadiliko ya tabianchi.
Soma pia: Wanaharakati wa hali ya hewa waanza maandamano makubwa
"Wakfu wa Hali ya Hewa, unatazamiwa kufungua njia kuelekea hatua za kuyaokoa mataifa yanayoendelea na balaa litokanalo na mabadiliko ya tabianchi, ingawa jitihada hii inarudishwa nyuma na mataifa tajiri yasiyojali," amesema Harjeet Singh, Mkuu wa Mkakati wa Kisiasa wa Kimataifa wa Mtandao wa Climate Action Network. Mtandao huu wa kimataifa unajumuisha asasi zaidi ya 1900 za kiraia za mazingira katika zaidi ya nchi 130.
Mkutano wa kilele wa kimataifa wa masuala ya hali ya hewa wa COP28 unatarajiwa kufanyika Dubai, mwishoni mwa mwezi Disemba.