Michelle Obama ampigia debe Barack Obama
26 Agosti 2008Siku ya mwanzo ya mkutano huo ilikamilishwa kwa hotuba ya Michelle Obama aliechukua fursa hiyo kuwaeleza wajumbe mkutanoni kwanini mume wake Barack Obama achaguliwe rais katika uchaguzi ujao.Hotuba hiyo ilituwama zaidi juu ya maisha yake na Barack Obama na hasa alieleza kule walikotokea.Amemsifu mume wake kama baba na mume muadilifu ambae siasa zake zinatokana na mila na tamaduni za Kimarekani. Akizungumza mbele ya zaidi ya wajumbe 4,000 waliokusanyika Denver kutoka kila pembe ya Marekani,Michelle Obama alieleza jinsi yeye na mume wake walivyokulia katika mazingira ya kawaida.Kwa hivyo amesema,yeye na Barack Obama wanaelewa vizuri shida zinazokabiliwa na umma katika maisha yao ya kila siku.Amesema,ni imani na jitahada za wazazi wao zilizowasaidia kufika pale walipo hii leo.Kwa hivyo anajua kuwa kila Mmarekani anaweza kutimiza ndoto yake.Akaongezea:
"Ninaamini kuwa kila mmoja wetu bila ya kujali umri,mazingira au kule tulikotokea-kila mmoja ana uwezo wa kutoa mchango wake katika maisha ya taifa hili."
Kwa kweli hotuba yake ilijaribu kuwaeleza wapiga kura zaidi kuhusu Barack Obama aliewasili katika uwanja wa kisiasa baada ya kuchaguliwa seneta miaka minne iliyopita tu.
Lakini mbali na hotuba hiyo ya kusisimua,mkutano wa chama cha Demokrat hiyo jana ulifikia kilele chake,pale Seneta Edward Kennedy mwenye miaka 74 alipojitokeza bila ya kutazamiwa.Kennedy anaeumwa saratani ya ubongo amesema,hakuna kilichoweza kumzuia kufika katika mkutano muhimu kama huo.Amesema,kuteuliwa kwa Obama kugombea urais ni ishara ya matumaini mapya kwa Marekani.Edward Kennedy ni seneta mwenye ushawishi mkubwa katika chama cha Demokratik.