Michezo ya Olimpiki kufunguliwa Rio
5 Agosti 2016Mji wa Rio de Janeiro umeahidi kuandaa sherehe za "aina pekee kwa dunia" .Muziki ya Samba itahanikiza katika ufunguzi wa michezo hiyo ya kwanza kuandaliwa katika nchi ya Amerika Kusini. Makundi 207,yakipepea bendera za nchi zao yataanza kuuzunguka uwanja wa michezo wa Maracana kuanzia saa sita za usiku kwa saa za Afrika Mashariki au mbili za usiku kwa saa za Brazil.
Sherehe za ufunguzi zitatoa picha ya ubunifu wa wabrazil kwa walimwengu-amesema hayo msimamizi mkuu wa sherehe za ufunguzi Marco Balich: "Hapajajitokeza tatizo lolote kati ya tume kubwa ya kimataifa na wabunifu wa Brazil. Kwa hivyo mtakachoona kinatoka Brazil,ubunifu wa kuvutia kutoka Brazil ,utakao kuliwaza moyo."Anasema Marco Balich.
Kwa mujibu wa waandalizi,sherehe za ufunguzi zinatoa picha ya mambo matatu:Bustani,tamaduni za aina tofauti na furaha.
Askari polisi na wanajeshi 85 elfu wanapiga doria
Hatua za usalama zimeimarishwa katika jiji hilo la Rio de Janeiro lenye wakaazi milioni sita na laki tano. Vikosi vya polisi na askari kanzu wanapiga doria katika kila pembe ya mji huo. Jumla ya askari polisi na wanajeshi 85 elfu wametawanywa katika mji huo. Kitisho cha mashambulio kama yale yaliyotokea Ulaya kiko ,hata hivyo maashabiki wanasema:" Nnajisikia vizuri sana,sina wasi wasi kuhusu hatua za usalama wakati wa michezo ya Olympik,hasa watu wakitilia maanani yaliyotokea Ulaya na Marekani. Na nnahisi niko salama kwasababu polisi wako kila mahala na usalama unadhibitiwa pia. Niko sawa tu."Anasema hayo Melanie ambae ni mtaalii kutoka Uingereza.
Maoni sawa na hayo yametolewa pia na maripota na mashabiki wengine wanaohudhuria michezo ya Olympic ya Rio de Janeiro.
Wauza vinjwaji waondolewa majiani
Mbali na hatua za usalama kuimarishwa, wachuuzi pia ambao kawaida huuza vinywaji na vyakula majiani, wamezuwiliwa kufanya hivyo wakati wote wa michezo ya Olympic itakayoendelea hadi Agosti 21. Wale tu waliopatiwa kibali ndio watakaoruhusiwa kuuza vinywaji na vyakula vyao tena katika maeneo maalum.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Agenturvideo/AFP
Mhariri:Yusuf Saumu