1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rekodi ya haki za binadamu yaigubika michezo ya olimpiki

3 Februari 2022

China yakosolewa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya jamii za walio wachache

China Schnee Peking 2022
Picha: Anna Ratkoglo/Sputnik/dpa/picture alliance

Michezo ya  Olimpiki ya majira ya baridi  inaanza rasmi kesho Ijumaa ambapo rais wa kamati ya michezo hiyo duniani Thomas Bach amesema mashindano ya mwaka huu huko Bejing yatabadilisha kabisa  sura ya ukubwa wa mashindano hayo. Japokuwa tayari mashindano hayo yanaandamwa na wasiwasi kuhusu suala la haki za binadamu miongoni mwa mengine.

Mashindano ya Olimpiki ya msimu wa baridi yanang'oa nanga kesho Ijumaa na yataendelea kwa kipindi cha jumla ya siku 18 huko Beijing China yakigubikwa na mashaka kuhusu haki za binadamu pamoja na janga la virusi vya Corona. Chama tawala cha kikomunisti cha China kinataraji kwamba michezo hiyo ya kimataifa itakuwa silaha bora ya kuleta mafanikio licha ya kushuhudiwa hatua za kususiwa na baadhi ya nchi kufuatia mivutano ya kidiplomasia. Khofu iliyoko kuhusu usalama wa mchezaji Tennis Peng Shuai sambamba na tahadhari zilizotolewa juu ya watu kufuatiliwa na athari za kimazingira zinazoweza kusababishwa na michezo hiyo.

Picha: Ng Han Guan/AP Photo/picture alliance

Itambulike kwamba sherehe za ufunguzi wa michezo hiyo kesho ijumaa itafanyika katika uwanja wa taifa wa michezo mjini Beijing ambao pia unafahamika kama uwanja wa kiota cha ndege  na michezo hiyo itafanyika katika moja ya maeneo makavu kabisa ya China ambako theluji ya kutengenezwa ndiyo itakayotumika viwanjani kufanikisha michezo mbali mbali itakayoshuhudiwa. Hata hivyo yapo mengi yanayosikika kimataifa yakionesha mitizamo ya mwelekeo unaotowa sura ya michezo hiyo kuandamwa kisiasa.

Picha: Valery Sharifulin/TASS/imago images

Rais wa Urusi Vladmir Putin amevikosoa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya nchi yake kuhusiana na madai ya wachezaji wake kutumia madawa ya kuongeza nguvu misuli katika michezo. Rais Putin amekosoa vikwazo hivyo katika wakati ambapo anakutana na rais wa China Xi Jinping huko Beijing kwenye michezo hiyo.Putin amekanusha kwamba serikali yake ilisimamia mpango wa kutoa madawa ya kuongeza nguvu misuli kwa wachezaji wake katika Olimpiki ya majira ya baridi ya  mnamo mwaka 2014 iliyofanyika nchini Urusi. Kufichuka kwa kadhia hiyo itakumbukwa kulisababisha msururu wa hatua za Urusi kuchukuliwa hatua ya kupigwa marufuku  na mashirika mbali mbali ya michezo ya kimataifa.

Lakini pia suala la haki za binadamu limetamalaki michezo hiyo ya Beijing na hasa jicho likimulikwa katika suala la namna China inavyowashughulikia jamii ya Uighur na jamii nyingine za wachache nchini humo. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameipachika  jina michezo hiyo na kuiita ni michezo ya maangamizi ya halaiki.

Marekani na nchi nyingine kadhaa za dunia  zimechukua uamuzi wa kuisusia kutokana na vitendo vya ukiukaji haki za binadamu vinavyoripotiwa katika taifa hilo.Shirika la Human Rights Watch limesema wanaharakati wa haki za binadamu wanakabiliwa na vitisho,kuhojiwa na kuonywa na maafisa usalama wa serikali kujiweka kando na michezo hiyo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW