Michezo yacheleweshwa na mabango ya matusi
2 Machi 2020Watangazaji wa uwanjani mjini Dortmund na Berlin walitishia kuvunja michezo hiyo hadi pale mabango hayo yatakapoondolewa, wakati mchezo wa Bayern Munich dhidi ya wenyeji Hoffenheim ulimalizika katika hali ambayo si ya kawaida wakati wachezaji kutoka pande zote walipokuwa wakipeana mpira ili kukamilisha dakika 10 za mwisho.
Uingiliaji huo ni ishara pana ya mjadala mkali katika soka la Ujerumani kati ya mashabiki wa vilabu vya kitamaduni na timu zile mpya ambazo zimekuwa zikipata fedha kutoka kwa wawekezaji na wamiliki binafsi.
Mashabiki waliokuwa wakionesha upinzani wao walililenga shirikisho la kandanda la Ujerumani DFB na uamuzi wake wa kutoa adhabu ya miaka miwili kwa mashabiki wa Borussia Dortmund kusafiri kwa ajili ya michezo ya klabu hiyo dhidi ya Hoffenheim, baada ya mashabiki wa Dortmund kuweka mabango yenye kashfa .
Hatua hiyo hata hivyo ilisaidia tu kuwaamsha mashabiki wa timu nyingine kuchukua hatua kuhusiana na kile walichosema ni adhabu kwa mashabiki wote wa Dortmund. Mashabiki walipata uungwaji mkono wa nahodha wa FC Koln Jonas Hector baada ya ushindi wa timu hiyo siku ya Jumamosi dhidi ya Schalke 04 , wakati alipohoji kwa nini watu 20,000 ambao wamekuwa wakituunga mkono kwa dakika zote 90 waadhibiwe kwa matendo ya wachache?
Shutuma nyingi zilielekezwa kwa mfadhili ya Hoffenheim Dietmar Hopp, ambaye amekuwa akikosolewa na mashabiki baada ya kukwepa sheria ya ligi ya umiliki na kuwekeza zaidi ya euro milioni 350 katika klabu hiyo ya kijijini kwake, na kuifikisha katika daraja la kwanza.
Mabango hayo yenye kashfa yakimkosoa Hopp yamepenyezwa katika majukwaa ya uwanjani katika maeneo mbali mbali ya mashabiki katika wiki za hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kuweka sura ya Hopp, pamoja na kumuita kuwa ni mtoto wa malaya.
Rummenigge asikitishwa
Mwenyekiti wa Bayern Munich Karl-Heinz Rummenigge alisimama pamoja na Hopp wakati wa mchezo wa Jumamosi , akitikisa kichwa kwa masikitiko na kuwaomba mashabiki wa timu yake kuliondoa bango hilo. Baada ya mchezo huo Rummenigge alisema ametiwa aibu sana na mashabiki wake. "Naomba msamaha kwake Hopp, lakini hakuna kisingizio cha mashabiki hao kufanya kile walichokifanya."
Alipokuwa akizungumza kuhusiana na mauaji ya chuki ya mjini Hanau , rais wa shirikisho la kandanda nchini Ujerumani Fritz Keller amesema kuwa chuki haina nafasi ndani na nje ya uwanja.
"Katika soka , nje na ndani ya uwanja, wakati wa mchezo na ndani ya uwanja, kila mahali kile kinachohusika na jamii, chuki na kuwatenga watu wa jamii nyingine , haina nafasi. Hii ni njia ya kijinga kabisa , ambayo mtu anaweza kujivika, na ndio sababu hakuna nafasi kwa ubaguzi, hakuna nafasi kwa chuki ndani ya viwanja."
Fritz Keller aliyasema hayo kabla ya matukio ya wiki hii , ambayo yameliweka kandanda la Ujerumani njia panda, wakati viongozi wakijaribu kuzuwia chuki , lakini mashabiki wakiungana kote Ujerumani na kuonesha chuki yao dhidi ya mfadhili na mmiliki wa timu ya daraja la kwanza hapa Ujerumani.
Chuki haina nafasi katika michezo
Mchezaji wa klabu ya Union Berlin raia wa Austria Christopher Trimmel alipoulizwa maoni yake kuhusu upinzani wa mashabiki kwa hatua ya DFB kuwazuwia mashabiki wa Borussia Dortmund kutosafiri kwenda Hoffenheim, alisema
"Mimi pia napendelea sana , kujiunga na upinzani wa manbo mbali mbali, lakini inapokuwa watu wanamtukana mtu binafsi moja kwa moja, hapo sikubaliani. Hiyo hauhusiki kabisa na upinzani. tumewasiliana wazi, kwamba mabango haya hatutaki kuyaona."
Pamoja na hayo Bayern Munich baada ya kuikandika timu ya Dietmar Hopp, Hoffenheim kwa mabao 6-0 siku ya Jumamosi ilijiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi, ambapo timu inayofuata ya RB Leipzig iliridhika na sare ya bao 1-1 dhidi ya Bayer Leverkusen. Bayern imefungua sasa mwanya wa pointi 3 dhidi ya Leipzig, ambayo imejikingia pointi 49, ikifuatiwa na Borussia Dortmund yenye pointi 48.
Mchezaji wa kati wa Bayer Leverkusen Kai Havertz baada ya sare dhidi ya Leipzig alikuwa na haya ya kusema.
"Haukuwa mchezo mzuri kwetu. Ulikuwa mchezo ovyo ovyo na chapwaa kabisa , kutoka kila upande, bila kasi na hela heka za mchezo. nafikiri , iwapo timu moja ingeweza kucheza kwa nguvu kwa muda wa dakika tano, ingeweza kushinda. na mwishowe hakukuwa na chochote mbali ya pointi moja tu."