Wachezaji kuwakumbuka wahanga wa Paris
16 Novemba 2015Timu hizo zitaungana katika kuonesha mshikamano siku nne baada ya mashambulizi ya kigaidi mjini Paris. Mashambulio ya Ijumaa yamegusa hususan kandanda kwa karibu, baada ya washambuliaji watatu wa kujitoa muhanga kujiripua nje ya uwanja wa stade de France wakati Ufaransa ikicheza na Ujerumani.
Binamu yake mchezaji wa kati wa timu ya Ufaransa Lassana Diarra ni mmoja kati ya watu 129 waliouwawa , wakati dada yake mchezaji mwenzake Antoine Griezmann alinusurika bila madhara yoyote kutoka katika shambulio hilo katika ukumbi wa burudani wa Bataclan mjini Paris.
Lakini shirikisho la kandanda la Ufaransa FFF, limesisitiza kwamba mchezo huo wa kesho uendelee na kwa sasa unaonekana kama fursa ya kuonesha mshikamano, na huku kampeni katika mitandao ya kijamii inawahimiza mashabiki wa Uingereza kujiunga na kuimba wimbo wa taifa la Ufaransa "La marseillase" , kabla ya mchezo huo kuanza.
"Mchezo huo utakuwa na kila ushindani, lakini pia utakuwa unatoa ishara kwamba ulimwengu wa kandanda uko pamoja dhidi ya mauaji," amesema kocha wa Uingereza Roy Hodgson.
Wakati huo huo kansela Angela Merkel wa Ujerumani na baraza lake la mawaziri watahudhuria mchezo wa kirafiki kati ya Ujerumani na Uholanzi mjini Hannover kesho ili kuonesha mshikamano na wahanga wa shambulio la kigaidi mjini Paris.
Shirikisho la kandanda la Ujerumani DFB lilifikiria kuufuta mchezo huo wa kirafiki mjini Hannover , lakini likaamua kuendelea na mchezo huo ili kutoa ujumbe wa wazi wakati Ufaransa itapambana na Uingereza usiku huo mjini London. Rais wa muda wa shirikisho la kandanda la Ujerumani Reinhard Rauball amesema ujumbe ni wazi: "hatutatishwa na ugaidi."
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe / dpae
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman