1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michuano ya Kombe la Dunia 2022 yazinduliwa rasmi

20 Novemba 2022

Michuano ya kombe la dunia imefunguliwa rasmi hii leo nchini Qatar katika hafla ya kihistoria kwa taifa hilo. Hii ni mara ya kwanza kwa taifa la Mashariki ya Kati kuandaa michuano ya kombe la dunia.

Fußball-WM Katar | Eröffnungsfeier
Picha: Ken Satomi/Yomiuri Shimbun/picture alliance

Shamrashamra zimehanikiza kwenye sherehe hizo za ufunguzi, wakati mamia ya mashabiki wakiendelea kumiminika nchini humo. Vilabu vya pombe na vya usiku vilionekana kufurika mashabiki na meza nyingi zikiwa tayari zimechukuliwa kabla ya ufunguzi na sababu kubwa ikiwa ni kutokana na zuio la kunywa pombe ndani ya viwanja.

Soma Zaidi: Infantino:Mizozo ikome wakati wa kombe la dunia

Siku na saa chache kuelekea michuano hiyo, baadhi ya wachezaji wameripotiwa kwamba hawataweza kushiriki kutokana na kuwa majeruhi, hali inayochangia kupunguza msisimko wa michuano hiyo.

Mapema, kocha wa Ufaransa Didier Deschamps amesema hatoliziba pengo la mshambuliaji majeruhi Karim Benzema kwenye kikosi chake kinachotetea ubingwa na sasa kinasalia na wachezaji 25. Benzema aliyefanya mazoezi kwa mara ya kwanza jana Jumamosi na kikosi hicho huko Qatar, alilazimika kuondoka mapema kutokana na maumivu ya paja na matokeo ya uchunguzi yaliyonyesha hataweza kucheza. Taarifa hizi zimewashtua mashabiki na Ufaransa waliokiri kuwa ni mbaya na zilizowakatisha tamaa ya kutetea ubingwa.

Ufaransa haitaongeza mchezaji wa kuliziba pengo la Karim Benzema.Picha: Francois Mori/AP/picture alliance

Alipoulizwa na kituo cha utangazaji cha Ufaransa cha TeleFoot iwapo ataziba pengo la mshindi huyo wa tuzo ya kimataifa ya Ballon d'Or, Deschamps alijibu "hapana". Alisema ana imani na timu yake inayofanya kila kitu kwa viwango vya juu wanapokuwa ndani na nje ya uwanja

Benzema ni mchezaji wa pili wa Ufaransa kwenye orodha ya majeruhi akiungana na Christopher Nkunku ambaye nafasi yake imechukuliwa na Randal Kolo Muani. Paul Pogba a N'Golo Kante pia waliachwa kwenye michuano hiyo. Ufaransa itaanza kwa kukutana na Australia siku ya Jumanne.

Van Virgil asikitishwa na taarifa za Mane, azichukulia kama fursa

Na kutoka kikosi cha Uholanzi, nyota wa kikosi hicho Virgil van Dijk amekiri kusikitishwa na taarifa za Sadio Mane, aliyewahi kucheza naye katika kikosi cha Liverpool ya England, kwamba hatoweza kucheza kutokana na majeraha, ingawa kwa upande mwingine anakiri hatua hiyo inaiongezea matumaini timu yake.

Wawili hao huenda wangekutana wakati Uholanzi inapopambana na Senegal kwenye mechi ya kwanza ya Kundi A kesho Jumatatu, lakini Mane anayeichezea Bayern Munich ya Ujerumani hatakuwepo kutokana na maumivu ya mguu.

Vitambaa vyenye rangi hii vimezuiwa kuvaliwa kwenye michuano hiyo.Picha: Frank Hoermann/Sven Simon/IMAGO

Muda mfupi kabla ya michezo hiyo kufunguliwa rasmi, kulikuwa bado hakujafikiwa makubaliano kuhusiana na iwapo makapteni wa timu wataruhusiwa kuvaa vitambaa ama "armband" zenye rangi nyingi zinazoashiria kuunga mkono mapenzi ya jinsia moja.

Kulingana na rais wa Shirikisho la Soka la Ujerumani, DFB, Bernd Neuendorf, hakuna suluhu iliyofikiwa katika mazungumzo yaliyofanyika hii leo kati ya mashirikisho ya soka ya Ulaya, UEFA na la ulimwengu, FIFA, ingawa Neuendorf amesisitiza kwamba watavaa vitambaa hivyo. Mlinda lango wa Bayern Munich na kapteni wa timu ya taifa ya Ujerumani Emmanuel Neuer amenukuliwa akisisitiza kwamba atavaa kitambaa hicho, licha ya vizuizi vilivyotangazwa dhidi ya yoyote atakayevivaa kwenye michuano hiyo.

Viongozi mbalimbali wahudhuria Ufunguzi.

Viongozi mbalimbali wamekwenda Qatar kushuhudia ufunguzi huo. Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman amewasili Doha mapema leo na kuwa miongoni mwa viongozi wa kisiasa waliokwenda kushuhudia ufunguzi wa michuano hiyo mikubwa kabisa ya soka ulimwenguni, kabla ya mechi ya kwanza baina ya wenyeji Qatar na Ecuador.

Ikumbukwe Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Misri waliwahi kukata mahusiano ya kidiplomasia na Qatar kwa kipindi cha miaka mitatu, wakiishutumu kwa kufadhili ugaidi, ingawa Qatar inakana madai hayo. Hata hivyo walirejesha mahusiano hayo mwaka jana.

Kuonyesha mahusiano mazuri baada ya mvutano huo, rais wa Algeria Abdel Fattha al-Sissi pia amekwenda Qatar kwenye ufunguzi wa michuano hiyo, pamoja na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Tizama Zaidi

Mashirika: AFP/RTRE/DPA/

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW