Michuano ya kombe la Shirikisho la kandanda la Ujerumani.
16 Agosti 2010Katika michuano ya kombe la Shirikisho la kandanda la Ujerumani DFB, miongoni mwa matukio ya kushangaza ni kuyaaga mashindano mapema kwa kilabu ya St Pauli iliopanda daraja kucheza ligi kuu bundesliga msimu huu. St Pauli ilitandikwa bao moja kwa bila na kilabu ya daraja la nne Chemnitz .
Kilabu nyengine ya ligi kuu iliyopata pigo na kuyaaga mashindano haya mapema ni Hannover baada ya kutolewa na kilabu inayocheza ligi ya mkoa ya Eversberg kwa mikwaju ya Penalty mabao 5-4 baada ya kumaliza dakika za kawaida za nyongeza zikiwa bado sare bila kwa bila .
Lakini mvua ya magoli iliwakumba wachezaji wa ridhaa kutoka Torgelower mbele ya Hamburg iliyowamiminia mabao 5-1 . Mdachi Ruud van Nisrelrooy aliuona wavu mara tatu.
Bremen haikua na kazi ngumu na hivyo ikaiondoa timu ya daraja la tatu Rot Weisse 4-0, huku Wolfsburg na kocha wao Muingereza Steve McClaren ikilazimika kutoka jasho jembamba hadi dakika mbili kabla ya mchezo kumalizika ndipo ilipopata ufuweni kwa bao la ushindi la Mbrazil Grafite na pambano lao kumalizika kwa magoli 2 kwa 1.
Leo katika mashindano ya kombe hilo la shirikisho la kandanda la Ujerumani Bayern Munich, mabingwa wa Ujerumani wataumana na Schalke.
Akizungumzia mpambano huo mchezaji wa Bayern Munich Thomas Müller alikuwa na haya ya kusema.
Itakumbukwa kuwa Müller aliibuka mojawapo ya wachezaji bora katika mashindano yaliomalizika ya kombe la dunia nchini Afrika kusini.
Mwandishi Maryam Dodo Abdalla
Mpitiaji:Abdul-Rahman, Mohammed