1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani atatawazwa mfalme wa soka la Ulaya mwaka huu?

4 Juni 2021

Michuano ya mataifa ya Ulaya Euro 2020 itang'oa nanga kuanzia Juni 11 hadi Julai 11 mwaka huu wakati timu 24 zikiingia uwanjani kusaka ubingwa. Je, nani atatawazwa mfalme wa soka la Ulaya mwaka huu?

UEFA Euro 2020 Symbolbild
Picha: Jane Barlow/empics/picture alliance

Michuano ya mataifa ya Ulaya Euro 2020 itang'oa nanga kuanzia Juni 11 hadi Julai 11 mwaka huu wakati timu 24 zikiingia uwanjani kusaka ubingwa. Je, nani atatawazwa mfalme wa soka la Ulaya mwaka huu? 

Timu 24 zitakazoshiriki katika michuano ya mataifa ya Ulaya Euro 2020 zitakagawanya katika makundi sita kuanzia kundi A hadi F huku kila kundi likiwa na timu nne.

Katika kundi B, zipo timu za taifa za Ubelgiji, Urusi, Denmark na Finland.

Ubelgiji ambayo imewahi kushiriki michuano hiyo mara sita kuanzia fainali za mwaka 1972, 1980, 1984, 2000, 2016 na mwaka huu inatajwa kuwa miongoni mwa timu zenye nafasi kubwa ya kushinda taji hilo. Wachambuzi wa soka wanakitaja kikosi cha sasa kuwa "kikosi cha dhahabu" na kilimaliza katika nafasi ya tatu katika michuano ya kombe la Dunia.

Kocha Roberto Martinez ana wachezaji nyota wakiwemo nahodha Eden Hazard wa Real Madrid, Romelu Lukaku wa Inter Milan na Kevin de Bruyne wa Manchester City.

Wachezaji wa Ubelgiji Axel Witsel na Kevin De BruynePicha: picture-alliance/dpa/NurPhoto/M. Kireev

Katika safu ya kati, Axel Witsel anatajwa kuwa mchezaji mzoefu na huenda akaisaidia sana timu hiyo katika michuano ya Ulaya. Ubelgiji ina kila sababu ya kuwa na matumaini ya kufanya vyema katika michuano ya mwaka huu.

Urusi imewahi kushiriki michuano ya mataifa ya Ulaya mara 12 kuanzia mwaka 1960, 1964, 1968, 1972, 1988, 1992, 1996, 2004, 2008, 2012, 2016 na mwaka huu.

Timu hiyo ilikuwa katika fomu mbaya kabla ya mechi za kombe la dunia la mwaka 2018 zilizoandaliwa nchini humo, lakini kufika kwao katika hatua ya robo fainali ya kombe la dunia kulibadilisha hali ya wachezaji na walianza tena kujiamini.

Timu ya taifa ya UrusiPicha: Sergei Fadeichev/imago images

Timu hiyo inayotiwa makali na Stanislav Cherchesov ilifuzu kwa urahisi kwa michuano ya mataifa ya Ulaya japo kibarua kigumu kinawasubiri katika kundi B.

Aleksandr Golovin anayeichezea klabu ya Monaco ya Ufaransa na nahodha Artem Dzyuba wa Zenit St Petersburg ndio wachezaji wanaomulikwa zaidi katika timu hiyo. Katika michuano ya Ulaya ya mwaka 2008, Urusi ilifika hadi katika hatua ya nusu fainali. Je, timu ya sasa ina uwezo wa kufikia mafanikio ya timu ya muungano wa Kisovieti ya mwaka 1960 iliyoshinda taji la Ulaya?

Denmark inashiriki michuano hii kwa mara ya tisa sasa kuanzia 1964, 1984, 1988, 1992, 1996, 2000, 2004, 2012 na 2021.

Timu hiyo ilikuwa na wakati mgumu katika mechi zake za kutafuta tiketi ya kufuzu kwa michuano ya mwaka huu. Denmark itategemea uzoefu wa mlinda lango wake Kasper Schmeichel wa Leicester City ambaye anataraji kuiga mafanikio ya babake Peter Schmeichel ya mnamo mwaka 1992.

Mashabiki wa Denmark hawana makubwa ila wanataraji kuwa angalau mwaka huu watafuzu katika hatua ya makundi. Mchezaji mwengine nyota ni Christian Eriksen pamoja na mshambuliaji wa RB Leipzig Yussuf Poulsen.

Finland inashiriki michuano hii kwa mara ya kwanza katika historia ya michuano ya mataifa ya Ulaya. Kocha wake Markkz Kanerva ana uzoefu mdogo katika soka la kimataifa. Timu hiyo itawategemea sana mshambuliaji wa Norwich City Teemu Pukki, na mlinda lango Lukas Hradecky anayechezea klabu ya Bayer Leverkusen inayoshiriki ligi kuu ya kandanda ya Ujerumani, Bundesliga.

Finland inaingia katika michuano hii ikiwa bila ya shinikizo ya aina yoyote, na hilo huenda likawasaidia kuimarisha kiwango chao cha mchezo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW