1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoUfaransa

Michuano ya Michezo ya Olimpiki Paris 2024 yaendelea

1 Agosti 2024

Mashindano ya Olimpiki Paris 2024 yanaendelea nchini Ufaransa. Jumla ya medali 18 za dhahabu zilishindaniwa siku ya Jumatano katika mashindano ya michezo mbalimbali.

Michezo ya Olimpiki Paris 2024
Michezo ya Olimpiki Paris 2024Picha: Marcus Brandt/dpa/picture alliance

Tukianza na mchezo wa kuogelea, mchina Pan Zhanle alijishindia medali yake ya kwanza ya dhahabu ya Olimpiki katika mchuano wa kuogelea. Pan Zhanle alivunja rekodi yake kwa kuogelea mita 100 katika muda usiozidi sekunde 48.

Ushindi huu wa hali ya juu haukuwa wa kipekee katika uwanja wa Arena La Défense mjini Paris ambako kulishuhudiwa mambo kemkem. Mfaransa Léon Marchand aliibuka mshindi mara mbili katika michuano tofauti ya kuogelea mita 200.

Katika mchuano wa kuogolea mita 1500, Mmarekani Katie Ledecky aliondoka pia na medali ya dhahabu, ikiwa ni ushindi wa  medali ya Olimpiki  kwa mara ya nane na hivyo kuwa mwanamke wa pili aliyefaulu zaidi katika historia ya michezo hiyo, baada ya mwanamke wa Kisovieti Larissa Latynina aliyejikusanyia medali tisa za Olimpiki kati ya mwaka 1956 na 1964.

Mchezo wa mpira wa kikapu na soka la wanawake

Mechi ya mpira wa kikapu kati ya Australia na New ZealandPicha: Kevin Manning/Action Plus/IMAGO

Timu ya Marekani ikiongozwa na LeBron James imefuzu kuingia robo-fainali ya Michezo ya Olimpiki baada ya kuiburuza Sudan Kusini kwenye uwanja wa Pierre-Mauroy kwa alama 103 dhidi ya 86.

Marekani ni timu pekee iliyoshinda mechi zake mbili za kwanza katika Kundi C baada ya kuicharaza Serbia kwa alama 110 dhidi ya 84 na hivyo kujihakikishia nafasi ya tobo fainali hata kabla ya kumenyana na Puerto Rico siku ya Jumamosi.

Soma pia: Mashindano ya Olimpiki katika mto Seine yaahirishwa

Sasa tuliangazie soka la wanawake, hapo jana mjini Lyon, Ufaransa iliishinda New Zealand mabao 2-1 na kufuzu katika hatua ya robo fainali ya mashindano hayo ya Olimpiki, sambamba na Canada, Uhispania na Marekani. Mabao mawili ya Ufaransa yalipachikwa nyavuni na Marie-Antoinette Katoto katika dakika ya 22 na 49, na hivyo The Blues wakimaliza katika nafasi ya kwanza katika Kundi A na watamenyena na Brazil.

Mechi ya soka la wanawake katika michezo ya Olimpiki ya Tokyo mwaka 2020Picha: Edgar Siu/REUTERS

Canada, ambayo iliyoadhibiwa kwa kupokonywa pointi sita kwa kosa la kupeleleza mazoezi ya timu ya New Zealand mwanzoni mwa mashindano, imefanikiwa kusonga mbele na kuingia robo fainali baada ya kujishindia mechi zote tatu.

Siku ya Jumatano,  Canada waliwashinda Colombia 1-0 na sasa watamenyana na Ujerumani, ambao wanashikilia nafasi ya pili katika Kundi B. Colombia, iliyoorodheshwa kati ya timu mbili bora zilizoshika nafasi ya tatu, itachuana na Uhispania mjini Lyon katika mzunguuko unaofuata. Katika Kundi B, Marekani ilitetea hadhi yake ya timu bora kwa kuicharaza Australia 2-1.

Soma pia: Mwanaharakati akamatwa kuhusiana na hujuma kabla ya ufunguzi wa Olimpiki, Ufaransa

Ujerumani iliyochapwa vikali na Marekani (4-1) ilitoa kichapo cha mabao hayo hayo kwa Zambia (4-1) na kuambulia nafasi ya pili. Zambia wameyaaga mashindano huku Ujerumani wakitarajiwa kumenyana na Canada.

Hadi sasa China inaongoza kwa medali 9 za dhahabu ikifuatiwa Ufaransa yenye medali 8 na Japan inashikilia nafasi ya tatu. Ujerumani iko katika nafasi ya kumi na jumla ya medali 2 za dhahabu.